Hosea 1:1-5
Hosea 1:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Bwana lililomjia Hosea mwana wa Beeri, nyakati za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli. Mwenyezi-Mungu alipoanza kuongea na Waisraeli kwa njia ya Hosea, alimwambia hivi: “Nenda ukaoe mwanamke mzinzi, uzae naye watoto wa uzinzi, maana watu wa nchi hii wanafanya uzinzi mwingi kwa kuniacha mimi.” Basi, Hosea akaenda, akamwoa Gomeri, binti Diblaimu. Gomeri akapata mimba, akamzalia Hosea mtoto wa kiume. Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Yezreeli’, maana bado kitambo kidogo tu, nami nitaiadhibu jamaa ya Yehu kwa mauaji aliyoyafanya bondeni Yezreeli. Nitaufutilia mbali ufalme katika taifa la Israeli. Siku hiyo, nitazivunja nguvu za kijeshi za Israeli huko bondeni Yezreeli.”
Hosea 1:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hili ndilo neno la BWANA lililomjia Hosea, mwana wa Beeri, siku za Uzia, na Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli. Hapo kwanza BWANA aliponena kwa kinywa cha Hosea, BWANA alimwambia Hosea, Nenda ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi mwingi, kwa kumwacha BWANA. Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye akachukua mimba, akamzalia mtoto wa kiume. BWANA akamwambia, Mwite jina lake Yezreeli; kwa maana bado kitambo kidogo, nitaipatiliza nyumba ya Yehu damu ya Yezreeli, na kuukomesha ufalme wa nyumba ya Israeli. Tena itakuwa siku ile, nitauvunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli.
Hosea 1:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hili ndilo neno la BWANA lililomjia Hosea, mwana wa Beeri, siku za Uzia, na Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli. Hapo kwanza BWANA aliponena kwa kinywa cha Hosea, BWANA alimwambia Hosea, Enenda ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi mwingi, kwa kumwacha BWANA. Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye akachukua mimba, akamzalia mtoto mwanamume. BWANA akamwambia, Mwite jina lake Yezreeli; kwa maana bado kitambo kidogo, nitaipatiliza nyumba ya Yehu damu ya Yezreeli, na kuukomesha ufalme wa nyumba ya Israeli. Tena itakuwa siku ile, nitauvunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli.
Hosea 1:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Neno la BWANA lililomjia Hosea mwana wa Beeri wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na wakati wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi, mfalme wa Israeli. Wakati BWANA alipoanza kuzungumza kupitia Hosea, BWANA alimwambia, “Nenda ukajitwalie mwanamke wa uzinzi na watoto wa uzinzi, kwa sababu nchi ina hatia ya uzinzi wa kupindukia kwa kumwacha BWANA.” Kwa hiyo alimwoa Gomeri binti Diblaimu, naye akachukua mimba na kumzalia Hosea mwana. Kisha BWANA akamwambia Hosea, “Mwite Yezreeli, kwa kuwa kitambo kidogo nitaiadhibu nyumba ya Yehu kwa ajili ya mauaji ya kule Yezreeli, nami nitaukomesha ufalme wa Israeli. Katika siku ile nitavunja upinde wa Israeli katika Bonde la Yezreeli.”