Waebrania 4:1-7
Waebrania 4:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, kwa vile ahadi ya kuingia mahali pa pumziko bado ipo, na tuogope ili yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo. Maana Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale. Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani. Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi Mungu. Kama alivyosema: “Nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko.’” Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha malizika tangu alipoumba ulimwengu. Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba: “Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote.” Tena jambo hili lasemwa pia: “Hawataingia mahali pangu pa pumziko.” Basi, hiyo ahadi ya kuingia bado ipo, maana wale waliohubiriwa Habari Njema pale awali walishindwa kuingia humo kwa sababu walikosa kutii. Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa “Leo,” akasema baadaye kwa njia ya Daudi maneno yaliyokwisha tajwa: “Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiwe wakaidi.”
Waebrania 4:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, ikiwa ingalipo ahadi ya kuingia katika pumziko lake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa Habari Njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika pumziko lile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia pumzikoni mwangu: ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na tena kunena hapa napo, Hawataingia pumzikoni mwangu. Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo, kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mkisikia sauti yake, Msifanye mioyo yenu migumu.
Waebrania 4:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu: ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu. Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu.
Waebrania 4:1-7 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kwa hiyo, kwa kuwa bado ahadi ya kuingia rahani iko wazi, tujihadhari ili hata mmoja wenu asije akaikosa. Kwa maana sisi pia tumesikia Injili iliyohubiriwa kwetu, kama nao walivyosikia; lakini ujumbe ule waliousikia haukuwa na maana kwao, kwa sababu wale waliousikia hawakuuchanganya na imani. Sasa sisi ambao tumeamini tunaingia katika ile raha, kama vile Mungu alivyosema, “Kwa hiyo nikaapa katika hasira yangu, ‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’” Lakini kazi yake ilikamilika tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Kwa maana mahali fulani amezungumza kuhusu siku ya saba, akisema: “Katika siku ya saba Mungu alipumzika kutoka kazi zake zote.” Tena hapo awali amesema, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.” Kwa hiyo inabaki kuwa wazi kwa wengine kuingia, nao wale wa kwanza waliopokea Injili walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokutii. Kwa hiyo Mungu ameweka siku nyingine, akaiita “Leo”, akisema kwa kinywa cha Daudi baadaye sana, kwa maneno yaliyotangulia kunenwa: “Leo, mkiisikia sauti yake, msiifanye mioyo yenu migumu”.