Waebrania 3:7-14
Waebrania 3:7-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: “Kama mkisikia sauti yake leo, msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasi kama wakati ule wa majaribio kule jangwani. Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, ingawa walishuhudia matendo yangu kwa miaka arubaini! Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, ‘Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu’. Basi, nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko.’ Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai. Maadamu hiyo “Leo” inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi. Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni.
Waebrania 3:7-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha, Siku ya kujaribiwa katika jangwa, Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arobaini. Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu; Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu. Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho
Waebrania 3:7-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mkisikia sauti yake, Msifanye mioyo yenu kuwa migumu, Kama wakati wa kuasi, Siku ya kujaribiwa katika jangwa, Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arubaini. Kwa hiyo nilichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu; Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu. Hadharini, ndugu zangu, usiwepo katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutoamini, ujitengao na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu inaitwa leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho
Waebrania 3:7-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa hiyo, kama Roho Mtakatifu asemavyo: “Leo, kama mkiisikia sauti yake, msiifanye mioyo yenu migumu, kama mlivyofanya katika uasi, wakati ule wa kujaribiwa jangwani, ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima ingawa kwa miaka arobaini walikuwa wameyaona matendo yangu. Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile, nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka, nao hawajazijua njia zangu.’ Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu, ‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ” Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai. Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Kristo, kama tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho.