Waebrania 2:5-13
Waebrania 2:5-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hamjaona vitu vyote kutiwa chini yake, ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake; akisema, Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu; Katikati ya kanisa nitakuimbia sifa. Na tena, Nitakuwa nimemtumaini yeye. Na tena, Tazama, mimi nipo hapa na watoto niliopewa na Mungu.
Waebrania 2:5-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake. Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko: “Mtu ni nini, hata umfikirie; mwanadamu ni nini hata umjali? Ulimfanya tu kidogo kuwa chini ya malaika; umemvika taji ya utukufu na heshima, ukaweka kila kitu chini ya miguu yake.” Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote, yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa. Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka. Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu. Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao, ndugu zake; kama asemavyo: “Ee Mungu, nitawasimulia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao.” Tena asema: “Nitamwekea Mungu tumaini langu.” Na tena: “Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu.”
Waebrania 2:5-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo kwa muda kuliko malaika, Umemvika taji la utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakubakiza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hamjaona vitu vyote kutiwa chini yake, ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo kwa muda kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji la utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake; akisema, Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu; Katikati ya kanisa nitakuimbia sifa. Na tena, Nitakuwa nimemtumaini yeye. Na tena, Tazama, mimi nipo hapa na watoto niliopewa na Mungu.
Waebrania 2:5-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mungu hakuuweka ulimwengu ujao ambao tunanena habari zake chini ya malaika. Lakini kuna mahali mtu fulani ameshuhudia akisema: “Mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria, binadamu ni nani hata unamjali? Umemfanya chini kidogo kuliko malaika; ukamvika taji ya utukufu na heshima, nawe umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Kwa kuweka vitu vyote chini yake, Mungu hakuacha kitu chochote ambacho hakukiweka chini ya mwanadamu. Lakini kwa sasa, hatuoni kwamba kila kitu kiko chini yake. Lakini twamwona Yesu, aliyefanywa chini kidogo kuliko malaika, sasa akiwa amevikwa taji ya utukufu na heshima kwa sababu alistahimili mauti, ili kwamba kwa neema ya Mungu apate kuonja mauti kwa ajili ya kila mtu. Ili kuwaleta wana wengi katika utukufu, ilifaa kwamba Mungu, ambaye ni kwa ajili yake na kupitia kwake kila kitu kimekuwepo, amkamilishe mwanzilishi wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Yeye awafanyaye watu kuwa watakatifu, pamoja na hao ambao hufanywa watakatifu, wote hutoka katika jamaa moja. Hivyo Yesu haoni aibu kuwaita ndugu zake. Yeye husema, “Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu; mbele ya kusanyiko nitaimba sifa zako.” Tena, “Nitaweka tumaini langu kwake.” Tena anasema, “Niko hapa, pamoja na watoto ambao Mungu amenipa.”