Waebrania 13:7-13
Waebrania 13:7-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni neno la Mungu. Fikirini juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao. Yesu Kristo ni yuleyule jana, leo na milele. Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata. Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi hawana haki ya kula vitu vyake. Kuhani mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa tambiko kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji. Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake.
Waebrania 13:7-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida. Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiayo ile hema hawana ruhusa kula vitu vyake. Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi. Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango. Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutuma yake.
Waebrania 13:7-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida. Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiao ile hema hawana ruhusa kula vitu vyake. Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi. Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango. Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake.
Waebrania 13:7-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele. Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria. Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaohudumu katika hema hawana haki ya kula vile vitu vilivyowekwa juu yake. Kuhani mkuu huchukua damu ya wanyama na kuiingiza Patakatifu pa Patakatifu, kama sadaka ya dhambi, lakini miili ya hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. Vivyo hivyo, Yesu naye aliteswa nje ya lango la mji ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe. Kwa hiyo, basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba.