Waebrania 13:5-9
Waebrania 13:5-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?” Wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni neno la Mungu. Fikirini juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao. Yesu Kristo ni yuleyule jana, leo na milele. Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata.
Waebrania 13:5-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Msiwe na tabia ya kupenda fedha; muwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kamwe, wala sitakuacha. Hata tunathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.
Waebrania 13:5-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.
Waebrania 13:5-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema, “Kamwe sitakuacha, wala sitakupungukia.” Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri, “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini?” Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele. Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria.