Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 13:1-19

Waebrania 13:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Endeleeni kupendana kindugu. Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika bila kujua. Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao. Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao. Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi. Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?” Wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni neno la Mungu. Fikirini juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao. Yesu Kristo ni yuleyule jana, leo na milele. Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata. Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi hawana haki ya kula vitu vyake. Kuhani mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa tambiko kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji. Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake. Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja. Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu tambiko ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa kwa midomo inayoliungama jina lake. Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo tambiko zinazompendeza Mungu. Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu. Mtuombee na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima. Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo.

Waebrania 13:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua. Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao wanaodhulumiwa, kwa vile ninyi nanyi mlivyo katika mwili. Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; muwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kamwe, wala sitakuacha. Hata tunathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida. Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiayo ile hema hawana ruhusa kula vitu vyake. Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi. Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango. Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutuma yake. Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao. Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamalo jina lake. Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu. Watiini viongozi wenu, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa huzuni; maana haitawafaa ninyi. Tuombeeni; maana tunaamini kwamba tuna dhamiri njema, tukitaka kuwa na mwenendo mwema katika mambo yote. Nami nawasihi zaidi sana kufanya hayo ili nirudishwe kwenu upesi.

Waebrania 13:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua. Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao wanaodhulumiwa, kwa vile ninyi nanyi mlivyo katika mwili. Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida. Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiao ile hema hawana ruhusa kula vitu vyake. Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi. Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango. Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake. Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao. Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake. Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu. Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi. Tuombeeni; maana tunaamini kwamba tuna dhamiri njema, tukitaka kuwa na mwenendo mwema katika mambo yote. Nami nawasihi zaidi sana kufanya hayo ili nirudishwe kwenu upesi.

Waebrania 13:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Endeleeni kupendana kama ndugu. Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua. Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa. Ndoa na iheshimiwe na watu wote, nayo malazi yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati wote. Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema, “Kamwe sitakuacha, wala sitakupungukia.” Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri, “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini?” Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele. Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria. Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaohudumu katika hema hawana haki ya kula vile vitu vilivyowekwa juu yake. Kuhani mkuu huchukua damu ya wanyama na kuiingiza Patakatifu pa Patakatifu, kama sadaka ya dhambi, lakini miili ya hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. Vivyo hivyo, Yesu naye aliteswa nje ya lango la mji ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe. Kwa hiyo, basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba. Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao. Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu. Watiini viongozi wenu na kujinyenyekeza chini ya mamlaka yao. Kwa maana wao wanakesha kwa ajili yenu kama watu watakaopaswa kutoa hesabu. Watiini ili wafanye kazi yao kwa furaha, wala si kama mzigo, maana hiyo haitakuwa na faida kwenu. Tuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia. Ninawasihi zaidi mniombee ili nipate kurudishwa kwenu upesi.