Waebrania 12:4-11
Waebrania 12:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana katika kupambana na dhambi, nyinyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu. Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja nyinyi kuwa wanawe? “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya. Maana Bwana humpa nidhamu kila anayempenda, humwadhibu kila anayekubali kuwa mwanawe.” Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea nyinyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake? Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, nyinyi si wanawe, bali ni wana haramu. Zaidi ya hayo, sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili tupate kuishi. Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake. Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili.
Waebrania 12:4-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi; tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau maonyo ya Bwana, Wala usife moyo ukiadhibiwa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humuonya Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kuonywa mnastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyeonywa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawaheshimu; basi si ni afadhali zaidi kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoeshwa nayo matunda ya haki yenye amani.
Waebrania 12:4-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi; tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.
Waebrania 12:4-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu. Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema: “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usikate tamaa akikukemea, kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, na humwadhibu kila mmoja anayemkubali kuwa mwana.” Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi? Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake. Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.