Waebrania 12:1-8
Waebrania 12:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotungangania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu. Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kuijali aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu. Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa. Maana katika kupambana na dhambi, nyinyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu. Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja nyinyi kuwa wanawe? “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya. Maana Bwana humpa nidhamu kila anayempenda, humwadhibu kila anayekubali kuwa mwanawe.” Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea nyinyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake? Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, nyinyi si wanawe, bali ni wana haramu.
Waebrania 12:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa subira katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi katika mkono wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili upinzani mkuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi; tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau maonyo ya Bwana, Wala usife moyo ukiadhibiwa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humuonya Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kuonywa mnastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyeonywa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.
Waebrania 12:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi; tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.
Waebrania 12:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa. Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu. Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema: “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usikate tamaa akikukemea, kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, na humwadhibu kila mmoja anayemkubali kuwa mwana.” Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali.