Waebrania 11:32-40
Waebrania 11:32-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gideoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samueli na manabii. Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba, walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga, walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita, wakashinda majeshi ya kigeni. Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao wakiwa wamefufuliwa. Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi. Wengine walidhihakiwa na kupigwa mijeledi, na wengine walifungwa minyororo na kutupwa gerezani. Walipigwa mawe, walipasuliwa vipandevipande, waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa watu maskini, walioteswa na kudhulumiwa. Ulimwengu haukustahili kuwa na watu hao. Walitangatanga jangwani na milimani, wakaishi katika mashimo na mapango ya ardhi. Watu hawa wote walionekana kuwa mashujaa kwa sababu ya imani yao. Hata hivyo, hawakupokea yale ambayo Mungu aliwaahidi, maana Mungu alikuwa ameazimia mpango ulio bora zaidi kwa ajili yetu; yaani wao wangeufikia ukamilifu wakiwa pamoja nasi.
Waebrania 11:32-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka kutoka kwa makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa minyororo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizungukazunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizungukazunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi. Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi; kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
Waebrania 11:32-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi. Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi; kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
Waebrania 11:32-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii, ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini. Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.