Waebrania 1:5-14
Waebrania 1:5-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: “Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa Baba yako.” Wala hakusema juu ya malaika yeyote: “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu.” Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae, mzaliwa wa kwanza, ulimwenguni alisema: “Malaika wote wa Mungu na wamwabudu.” Lakini kuhusu malaika, alisema: “Amewafanya malaika wake kuwa upepo, na wahudumu wake ndimi za moto.” Lakini kuhusu Mwana, Mungu alisema: “Kiti chako cha enzi, ee Mungu, chadumu milele na milele! Wewe wawatawala watu wako kwa haki. Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Ndiyo maana Mungu, Mungu wako, amekuweka wakfu na kukumiminia furaha kubwa kuliko wenzako.” Na tena: “Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo, mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima, zote zitachakaa kama vazi. Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayatakoma.” Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: “Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.” Malaika ni nini ila roho wanaomtumikia Mungu na ambao hutumwa kuwasaidia wale watakaopokea wokovu?
Waebrania 1:5-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu. Na kwa habari za malaika asema, Afanyaye malaika wake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa miali ya moto. Lakini kwa habari za Mwana asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio. Na tena, Wewe, Bwana, hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi, Na mbingu ni kazi za mikono yako; Hizo zitaharibika, bali wewe unadumu; Nazo zote zitachakaa kama nguo, Na kama mavazi utazizinga, nazo zitabadilika; Lakini wewe u yeye yule, Na miaka yako haitakoma. Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?
Waebrania 1:5-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa maana ni malaika yupi ambaye wakati wowote Mungu alipata kumwambia, “Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuzaa?” Au tena, “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu?” Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, anasema, “Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.” Anenapo kuhusu malaika asema, “Huwafanya malaika wake kuwa pepo, watumishi wake kuwa miali ya moto.” Lakini kwa habari za Mwana asema, “Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, kitadumu milele na milele, nayo haki itakuwa fimbo ya utawala ya ufalme wako. Umependa haki na kuchukia uovu; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuweka juu ya wenzako kwa kukupaka mafuta ya furaha.” Pia asema, “Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizo zitatoweka, lakini wewe utadumu; zote zitachakaa kama vazi. Utazikungʼutakungʼuta kama joho, nazo zitachakaa kama vazi. Lakini wewe hubadiliki, nayo miaka yako haikomi kamwe.” Je, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wowote, “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako”? Je, malaika wote si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?
Waebrania 1:5-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana ni kwa malaika yeyote yupi Mungu, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu. Na kuhusu malaika asema, Awafanya malaika wake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa miali ya moto. Lakini kuhusu Mwana asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya haki. Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio. Na tena, Wewe, Bwana, hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi, Na mbingu ni kazi za mikono yako; Hizo zitaharibika, bali wewe unadumu; Nazo zote zitachakaa kama nguo, Na kama mavazi utazikunjakunja, na kama mavazi zitabadilishwa; Lakini wewe u yeye yule, Na miaka yako haitakoma. Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wowote, Uketi mkono wa kulia Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?