Hagai 2:15-19
Hagai 2:15-19 Biblia Habari Njema (BHN)
“Lakini sasa angalieni mambo yatakayotukia. Kabla ya kuanza kujenga upya hekalu langu, hali yenu ilikuwaje? Mliliendea fungu la nafaka mkitarajia kupata vipimo ishirini, lakini kulikuwa na vipimo kumi tu. Mliliendea pipa la divai mkitarajia kujaza vyombo hamsini, lakini mlikuta ishirini tu. Niliwapiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, nikaharibu kila mlichojaribu kupanda, lakini hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Leo ni siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, siku ambayo msingi wa hekalu umekamilika. Basi, ngojeni mwone yale yatakayotokea tangu leo. Ingawa sasa hamna nafaka ghalani, nayo mizabibu, mitini, mikomamanga na mizeituni haijazaa kitu, lakini tangu leo, nitawabariki.”
Hagai 2:15-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na sasa nawaomba, tafakarini; tangu siku hii na siku zilizopita; kabla jiwe halijatiwa juu ya jiwe katika nyumba ya BWANA; katika wakati huo wote, mtu alipofikia rundo la vipimo ishirini, palikuwa na vipimo kumi tu; na mtu alipofikia pipa kubwa apate kuteka divai ya vyombo hamsini, palikuwa na divai ya vyombo ishirini tu. Niliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la BWANA tafakarini haya. Je, Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki.
Hagai 2:15-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na sasa nawaomba, tafakarini; tangu siku hii na siku zilizopita; kabla halijatiwa bado jiwe juu ya jiwe katika nyumba ya BWANA; katika wakati huo wote, mtu alipofikia chungu ya vipimo ishirini, palikuwa na vipimo kumi tu; na mtu alipofikia shinikizo apate kuteka divai ya vyombo hamsini, palikuwa na divai ya vyombo ishirini tu. Naliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunielekea mimi, asema BWANA. Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kenda, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la BWANA tafakarini haya. Je! Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki.
Hagai 2:15-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“ ‘Sasa fikirini kwa uangalifu kuanzia leo na kuendelea: tafakarini jinsi mambo yalivyokuwa kabla halijawekwa jiwe moja juu ya lingine katika Hekalu la BWANA. Wakati mtu alipoendea lundo la nafaka la vipimo ishirini, kulikuwa na vipimo kumi tu. Wakati mtu alipoendea pipa la mvinyo ili kuchota vipimo hamsini, kulikuwa na vipimo ishirini tu. Kazi zenu zote za mikono nilizipiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, lakini hata hivyo, hamkunigeukia mimi,’ asema BWANA. ‘Tangu leo na kuendelea, kuanzia siku hii ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, tafakarini siku ambayo msingi wa Hekalu la BWANA uliwekwa. Tafakarini: Je, bado kuna mbegu iliyobakia ghalani? Mpaka sasa, hakuna mzabibu au mtini, mkomamanga wala mzeituni uliozaa tunda. “ ‘Kuanzia leo na kuendelea, nitawabariki.’ ”