Hagai 2:10-14
Hagai 2:10-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilimjia nabii Hagai, akamwambia: “Waambie makuhani watoe uamuzi juu ya jambo hili: Kama mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa vazi lake, kisha akagusa kwa upindo wa vazi hilo mkate au chakula kilichopikwa, au divai, au mafuta au chakula cha aina yoyote ile, je, chakula hicho kitakuwa kitakatifu?” Makuhani wakamjibu, “La, hasha.” Hagai akawauliza tena, “Je, mtu aliye najisi kwa kugusa maiti, akigusa baadhi ya vyakula hivi, chakula hicho kitakuwa najisi?” Makuhani wakamjibu, “Ndiyo, kitakuwa najisi.” Hapo Hagai akawaambia, “Mwenyezi-Mungu asema kwamba, hivyo ndivyo ilivyo kwa watu wa taifa hili na kila kitu wanachofanya; kadhalika na kila wanachotoa madhabahuni ni najisi.
Hagai 2:10-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani kuhusu sheria, mkisema, Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye kwa upindo wake akagusa mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula chochote, je, Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La. Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je, Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi. Ndipo Hagai akajibu, akasema, Hivyo ndivyo walivyo watu hawa, na hivyo ndivyo lilivyo taifa hili mbele zangu, asema BWANA; na hivyo ndivyo ilivyo kila kazi ya mikono yao; na kitu hicho wakitoacho sadaka huko ni najisi.
Hagai 2:10-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa kenda, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani katika habari ya sheria, mkisema, Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye akagusa kwa upindo wake mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula cho chote, je! Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La. Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je! Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi. Ndipo Hagai akajibu, akasema, Hivyo ndivyo walivyo watu hawa, na hivyo ndivyo lilivyo taifa hili mbele zangu, asema BWANA; na hivyo ndivyo ilivyo kila kazi ya mikono yao; na kitu hicho wakitoacho sadaka huko ni najisi.
Hagai 2:10-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario, neno la BWANA lilikuja kwa nabii Hagai: “Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: ‘Ulizeni makuhani jinsi sheria inavyosema: Kama mtu akibeba nyama iliyowekwa wakfu katika pindo la vazi lake, kisha lile pindo likagusa mkate au mchuzi, divai, mafuta au chakula kingine, je, kitu hicho kitakuwa kimewekwa wakfu?’ ” Makuhani wakajibu, “La hasha.” Kisha Hagai akasema, “Je, kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti akigusa mojawapo ya vitu hivi, kitu hicho kitakuwa kimetiwa unajisi?” Makuhani wakajibu, “Ndiyo, huwa kimenajisiwa.” Kisha Hagai akasema, “ ‘Basi ndivyo walivyo machoni pangu hawa watu na taifa hili,’ asema BWANA. ‘Lolote wafanyalo na chochote watoacho hapo ni najisi.