Hagai 2:1-9
Hagai 2:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hao watu waliokuwa wamebaki, ukisema, Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu? Lakini sasa uwe jasiri, Ee Zerubabeli, asema BWANA; nawe uwe jasiri, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni jasiri, enyi watu wote wa nchi hii, asema BWANA; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema BWANA wa majeshi; kama ilivyo ahadi niliyowawekea mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope. Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Kwa mara nyingine, kitambo kidogo tu, nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu; nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema BWANA wa majeshi. Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema BWANA wa majeshi. Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema BWANA wa majeshi.
Hagai 2:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo siku ya ishirini na moja, mwezi wa saba mwaka huohuo, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Hagai. Alimwambia Hagai aongee na mkuu wa Yuda, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki na watu wote waliorudi kutoka uhamishoni awaambie hivi: “Je, kuna yeyote kati yenu asiyekumbuka jinsi hekalu hili lilivyokuwa la fahari? Sasa mnalionaje? Bila shaka sasa mnaliona kama si kitu! Hata hivyo, usife moyo, ewe Zerubabeli. Jipe moyo, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Jipeni moyo nanyi watu wote wa nchi hii. Fanyeni kazi, maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nipo pamoja nanyi. Mlipotoka Misri niliwaahidi kwamba daima nitakuwa pamoja nanyi. Basi, ningali pamoja nanyi, kwa hiyo, msiogope kitu. “Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema, hivi karibuni nitazitikisa mbingu na dunia, bahari na nchi kavu. Nitayatikisa mataifa yote na hazina zao zote zitaletwa humu, nami nitalifanya hekalu hili kuwa la fahari. Mimi nimesema. Fedha na dhahabu yote duniani ni mali yangu. Hekalu jipya litakuwa lenye fahari zaidi kuliko lile la awali, na mahali hapo ndipo nitakapowapa watu wangu fanaka.” Asema Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
Hagai 2:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema, Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hayo mabaki ya watu, ukisema, Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu? Lakini sasa uwe hodari, Ee Zerubabeli, asema BWANA; nawe uwe hodari, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni hodari, enyi watu wote wa nchi hii, asema BWANA; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema BWANA wa majeshi; kama neno lile nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope. Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu; nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema BWANA wa majeshi. Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema BWANA wa majeshi. Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema BWANA wa majeshi.
Hagai 2:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba, neno la BWANA lilikuja kupitia nabii Hagai, kusema: “Sema na Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, na mabaki ya watu. Uwaulize, ‘Ni nani miongoni mwenu aliyebaki ambaye aliiona hii nyumba katika utukufu wake wa mwanzo? Sasa inaonekanaje kwenu? Je, haionekani kwenu kama si kitu? Lakini sasa uwe imara, ee Zerubabeli,’ asema BWANA. ‘Kuwa imara, ee kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Mwe imara, enyi watu wote wa nchi,’ asema BWANA, ‘na mfanye kazi. Kwa kuwa mimi nipo pamoja nanyi,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. ‘Hili ndilo nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri. Pia Roho wangu anadumu katikati yenu. Msiogope.’ “Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: ‘Baada ya muda kidogo kwa mara nyingine nitazitikisa mbingu na nchi, bahari na nchi kavu. Nitatikisa mataifa yote, nacho kile kinachotamaniwa na mataifa yote kitakuja, nami nitaujaza utukufu katika nyumba hii,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. ‘Fedha ni mali yangu na dhahabu ni mali yangu,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. ‘Utukufu wa nyumba hii ya sasa utakuwa mkubwa kuliko utukufu wa ile nyumba ya mwanzoni,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. ‘Na mahali hapa nitawapa amani,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.”