Habakuki 1:5-11
Habakuki 1:5-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu akasema: “Yaangalie mataifa, uone! Utastaajabu na kushangaa. Maana ninatenda kitu ukiwa bado unaishi, kitu ambacho ungeambiwa hungesadiki. Maana ninawachochea Wakaldayo, taifa lile kali na lenye hamaki! Taifa lipitalo katika nchi yote, ili kunyakua makao ya watu wengine. Wao ni watu wa kuchukiza na kutisha; wao hujiamulia wenyewe nini haki na adhama. “Farasi wao ni wepesi kuliko chui; wakali kuliko mbwamwitu wenye njaa. Wapandafarasi wao wanatoka mbali, wanaruka kasi kama tai arukiavyo mawindo. “Wote wanakuja kufanya ukatili; kwa nyuso kakamavu wanasonga mbele, wanakusanya mateka wengi kama mchanga. Wanawadhihaki wafalme, na kuwadharau watawala. Kila ngome kwao ni mzaha, wanairundikia udongo na kuiteka. Kisha wanasonga mbele kama upepo, wafanya makosa na kuwa na hatia, maana, nguvu zao ndizo mungu wao!”
Habakuki 1:5-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni, kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa. Kwa maana, angalieni, nawachochea Wakaldayo, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao. Hao ni watu wa kutisha sana, wa kuogofya sana; hukumu yao na ukuu wao hutoka katika nafsi zao wenyewe. Farasi wao ni wepesi kuliko chui, ni wakali kuliko mbwamwitu wa jioni; na wapanda farasi wao hujitapa naam, wapanda farasi wao watoka mbali sana; huruka kama tai afanyaye haraka ale. Wanakuja wote ili kufanya udhalimu; nyuso zao zimeelekezwa kwa bidii yao kama upepo wa mashariki, nao hukusanya mateka kama mchanga. Naam, huwadhihaki wafalme, na wakuu ni kitu cha kudharauliwa kwake; huidharau kila ngome; kwa maana huirundikia udongo, na kuitwaa. Kisha atapita kwa kasi, kama upepo, atapita na kuwa ana hatia; yeye ambaye nguvu zake ni mungu wake.
Habakuki 1:5-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni, kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa. Kwa maana, angalieni, nawaondokesha Wakaldayo, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao. Hao ni watu wa kutisha sana, wa kuogofya sana; hukumu yao na ukuu wao hutoka katika nafsi zao wenyewe. Farasi zao ni wepesi kuliko chui, ni wakali kuliko mbwa-mwitu wa jioni; na wapanda farasi wao hujitapa naam, wapanda farasi wao watoka mbali sana; huruka kama tai afanyaye haraka ale. Waja wote ili kufanya udhalimu; nyuso zao zimeelekezwa kwa bidii yao kama upepo wa mashariki, nao hukusanya mateka kama mchanga. Naam, huwadhihaki wafalme, na wakuu ni kitu cha kudharauliwa kwake; huidharau kila ngome; kwa maana hufanya chungu ya mavumbi, na kuitwaa. Kisha atapita kwa kasi, kama upepo, atapita na kuwa ana hatia; yeye ambaye nguvu zake ni mungu wake.
Habakuki 1:5-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Yatazame mataifa, uangalie na ushangae kabisa. Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu ambacho hungeamini, hata kama ungeambiwa. Nitawainua Wakaldayo, watu hao wakatili na wenye haraka, ambao hupita dunia yote kuteka mahali pa kuishi pasipo pao wenyewe. Ni watu wanoogopwa na wanaotisha; wenyewe ndio sheria yao, na huinua heshima yao wenyewe. Farasi wao ni wepesi kuliko chui, na wakali kuliko mbwa mwitu wakati wa machweo. Askari wapanda farasi wao huenda mbio; waendesha farasi wao wanatoka mbali. Wanaruka kasi kama tai ili kurarua; wote wanakuja tayari kwa fujo. Makundi yao ya wajeuri yanasonga mbele kama upepo wa jangwani, na kukusanya wafungwa kama mchanga. Wanawabeza wafalme, na kuwadhihaki watawala. Wanaicheka miji yote iliyozungushiwa maboma; wanafanya malundo ya udongo na kuiteka hiyo miji. Kisha wanapita kasi kama upepo na kusonga mbele: watu wenye hatia, ambao nguvu zao ndio mungu wao.”