Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 9:1-17

Mwanzo 9:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, muongezeke, mkaijaze nchi. Wanyama wote, ndege wote wa angani, viumbe wote watambaao juu ya nchi na samaki wote wa baharini watakuwa na hofu na kuwaogopa nyinyi. Wote wamewekwa chini ya mamlaka yenu. Wanyama wote hai watakuwa chakula chenu kama vile nilivyowapa mimea kuwa chakula chenu. Lakini msile nyama yenye damu, kwani uhai uko katika damu. Damu ya uhai wenu nitaidai; nitaidai kutoka kwa kila mnyama na binadamu. Atakayemuua binadamu mwenzake, nitamdai uhai wake. Amwagaye damu ya binadamu, damu yake itamwagwa na binadamu; maana binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu. Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni kwa wingi, mkaongezeke nchini.” Kisha Mungu akamwambia Noa na wanawe, “Ninaweka agano langu nanyi na wazawa wenu na viumbe vyote hai: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wa porini, wote waliotoka katika safina pamoja nanyi. Nathibitisha agano langu nanyi, kwamba, kamwe viumbe vyote hai havitaangamizwa kwa gharika, wala haitatokea tena gharika kuiharibu nchi.” Tena Mungu akasema, “Hii ndiyo alama ya agano ninalofanya kati yangu nanyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi kwa vizazi vyote vijavyo. Naweka upinde wangu mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano kati yangu na dunia. Kila nitakapoifunika dunia kwa mawingu, na huo upinde wa mvua utakapoonekana katika mawingu, nitalikumbuka agano langu nanyi na viumbe vyote hai. Kamwe maji hayatageuka kuwa gharika ya kuviangamiza viumbe vyote hai. Huo upinde utakapotokea mawinguni, nitauona na kulikumbuka agano hilo la milele kati yangu na viumbe vyote hai duniani.” Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya agano ambalo nimefanya na viumbe vyote hai duniani.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 9

Mwanzo 9:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi. Kila mnyama wa nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, na kila ndege wa angani: pamoja na vitu vyote vilivyojaa katika ardhi, na samaki wote wa baharini; vimetiwa mikononi mwenu. Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, kama nilivyowapa mboga za majani, kadhalika nawapa hivi vyote. Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile. Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu. Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni sana katika nchi, mkaongezeke ndani yake. Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, Tazama, nilithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi. Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi. Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni, nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili. Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi. Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara ya agano nililoliweka kati yangu na watu wote walioko katika nchi.

Shirikisha
Soma Mwanzo 9

Mwanzo 9:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi. Kila mnyama wa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, na kila ndege wa angani: pamoja na vitu vyote vilivyojaa katika ardhi, na samaki wote wa baharini; vimetiwa mikononi mwenu. Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, kama nilivyowapa mboga za majani, kadhalika nawapeni hivi vyote. Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile. Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu. Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni sana katika nchi, mkaongezeke ndani yake. Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi. Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi. Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni, nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili. Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi. Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara ya agano nililoliweka kati yangu na wote wenye mwili walioko katika nchi.

Shirikisha
Soma Mwanzo 9

Mwanzo 9:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia. Wanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu. “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai. Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake. “Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu, damu yake itamwagwa na mwanadamu, kwa kuwa katika mfano wa Mungu, Mungu alimuumba mwanadamu. Kuhusu ninyi, zaeni mwongezeke kwa wingi, mzidi katika dunia na kuijaza.” Ndipo Mungu akamwambia Noa na wanawe pamoja naye: “Sasa mimi ninaweka Agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu, pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wote wa porini, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi, kila kiumbe hai duniani. Ninaweka Agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika, kamwe haitakuwepo tena gharika ya kuangamiza dunia.” Mungu akasema, “Hii ni ishara ya Agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, Agano kwa vizazi vyote vijavyo: Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya Agano nifanyalo kati yangu na dunia. Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukijitokeza mawinguni, nitakumbuka Agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote. Wakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka Agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.” Hivyo Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya Agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 9

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha