Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 7:1-24

Mwanzo 7:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu akamwambia Noa, “Ingia ndani ya safina wewe pamoja na jamaa yako yote, kwa maana, kati ya watu wote wanaoishi nyakati hizi zako, nimekuona wewe peke yako kuwa mwadilifu mbele yangu. Chukua pamoja nawe wanyama wote walio safi, dume na jike, saba saba; lakini wanyama walio najisi, chukua dume na jike, wawiliwawili. Vilevile chukua ndege wa angani dume na jike, saba saba, ili kuzihifadhi hai aina zao duniani. Baada ya siku saba, nitanyesha mvua nchini siku arubaini mchana na usiku, na kila kiumbe hai nilichokiumba duniani nitakiangamiza.” Noa akafanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. Noa alikuwa na umri wa miaka 600 wakati gharika ilipotokea nchini. Noa, mkewe, wanawe na wake zao wakaingia ndani ya safina ili kuiepa gharika. Wanyama walio safi, wanyama walio najisi, ndege na viumbe vyote vitambaavyo, wawiliwawili, dume na jike, wakaingia ndani ya safina pamoja na Noa kama Mungu alivyomwamuru. Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaanza kuifunika nchi. Noa alipokuwa na umri wa miaka 600, mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, siku hiyo chemchemi zote za vilindi vya nchi zikabubujika maji, na madirisha ya mbinguni yakafunguka. Mvua ikanyesha nchini siku arubaini mchana na usiku. Siku hiyohiyo mvua ilipoanza kunyesha, Noa, mkewe na wanawe, Shemu, Hamu na Yafethi, pamoja na wake zao, waliingia ndani ya safina. Waliingia wao wenyewe pamoja na aina zote za wanyama wa porini, wanyama wafugwao, wanyama watambaao na ndege wa kila aina. Waliingia ndani ya safina pamoja na Noa wiliwawili wa kila aina ya viumbe hai. Kila aina yao waliingia, dume na jike, kama Mungu alivyomwamuru Noa. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaufunga mlango wa safina nyuma yake Noa. Gharika ilidumu nchini kwa muda wa siku arubaini. Maji yakaongezeka na kuiinua safina, ikaelea juu ya ardhi. Maji yakaendelea kuongezeka zaidi nchini na safina ikaelea juu yake. Maji hayo yakawa mengi sana juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu katika nchi. Yaliongezeka hata kuifunika milima kiasi cha mita saba na nusu. Viumbe wote hai katika nchi wakafa. Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama wa porini, makundi ya viumbe wote katika nchi kavu na wanadamu wote; naam, kila kiumbe hai katika nchi kavu kilikufa. Mungu akaangamiza kila kiumbe kilichokuwa hai duniani: Binadamu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Vyote viliangamizwa duniani. Noa tu ndiye aliyesalimika na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Maji hayo yalidumu katika nchi siku 150.

Shirikisha
Soma Mwanzo 7

Mwanzo 7:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki. Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, wa kiume na wa kike; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, wa kiume na wa kike. Tena katika ndege wa angani saba saba, wa kike na wa kiume; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote. Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arubaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali. Nuhu akafanya kama vile BWANA alivyomwamuru. Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi. Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika. Na katika wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi, wakaingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kike na wa kiume, kama vile Mungu alivyomwamuru Nuhu. Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi. Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka. Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arubaini mchana na usiku. Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye; wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yoyote. Waliingia katika safina alimokuwa Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake. Na walioingia, waliingia wa kike na wa kiume, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; BWANA akamfungia. Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arubaini; nayo maji yakazidi, yakaifanya safina ielee, ikaelea juu ya nchi. Maji yakaongezeka zaidi juu ya nchi; na safina ikaelea juu ya uso wa maji. Maji yakazidi kuongezeka sana sana juu ya nchi; hata milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikwa. Maji yakaongezeka hata milima ikafunikwa kiasi cha dhiraa kumi na tano. Wakafa watu wote waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu; kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu. Kila kilichokuwa hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali; mwanadamu, wanyama wa kufugwa, kitambaacho na ndege wa angani; vilifutiliwa mbali katika nchi, akabaki Nuhu tu, na hao waliokuwa pamoja naye katika safina. Maji yakapata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini.

Shirikisha
Soma Mwanzo 7

Mwanzo 7:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki. Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke. Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote. Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali. Nuhu akafanya kama vile BWANA alivyomwamuru. Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi. Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika. Na katika wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi, wakaingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, mume na mke, kama vile Mungu alivyomwamuru Nuhu. Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi. Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka. Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku. Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye; wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yo yote. Waliingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake. Na walioingia, waliingia mume na mke, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; BWANA akamfungia. Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arobaini; nayo maji yakazidi, yakaieleza safina, ikaelea juu ya nchi. Maji yakapata nguvu, yakazidi sana juu ya nchi; na ile safina ikaelea juu ya uso wa maji. Maji yakapata nguvu sana sana juu ya nchi; na milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa. Maji yakapata nguvu, hata ikafunikwa milima kiasi cha mikono kumi na mitano. Wakafa wote wenye mwili waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu; kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu. Kila kilicho hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali tangu mwanadamu hata mnyama wa kufugwa, na kitambaacho, na ndege wa angani; vilifutiliwa mbali katika nchi, akabaki Nuhu tu, na hao walio pamoja naye katika safina. Maji yakapata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini.

Shirikisha
Soma Mwanzo 7

Mwanzo 7:1-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo BWANA akamwambia Noa, “Ingia katika safina wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki. Uchukue wanyama saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, na wanyama wawili wawili wa kila aina walio najisi wa kiume na wa kike. Pia uchukue ndege saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, ili kuhifadhi aina zao mbalimbali katika dunia yote. Siku saba kuanzia sasa nitaleta mvua juu ya nchi kwa siku arobaini usiku na mchana, nami nitafutilia mbali kutoka uso wa nchi kila kiumbe hai nilichokiumba.” Noa akafanya yote kama BWANA alivyomwamuru. Noa alikuwa na miaka 600 gharika ilipokuja juu ya dunia. Noa na mkewe na wanawe na wake zao wakaingia katika safina ili waepuke ile gharika. Jozi ya wanyama walio safi na walio najisi, ndege na viumbe vitambaavyo, wa kiume na wa kike, walikuja kwa Noa wakaingia katika safina kama Mungu alivyomwamuru Noa. Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia. Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili mwaka wa 600 wa kuishi kwake Noa, siku hiyo ndipo chemchemi zote hata zilizo chini sana ya ardhi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa. Mvua ikanyesha juu ya nchi siku arobaini usiku na mchana. Siku hiyo Noa, na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao wakaingia katika ile safina. Nao walikuwa pamoja na kila mnyama wa mwituni kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa. Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai ndani yake vikaja kwa Noa viwili viwili, vikaingia katika safina. Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Noa, ndipo BWANA akamfungia ndani. Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani na maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka kwenye uso wa nchi. Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya nchi, na safina ikaelea juu ya uso wa maji. Maji yakazidi kujaa juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu chini ya mbingu yote. Maji yakaendelea kujaa yakaifunika milima kwa kina cha zaidi ya dhiraa kumi na tano. Kila kiumbe hai kitambaacho juu ya nchi kikaangamia: Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama pori, viumbe vyote juu ya nchi na wanadamu wote. Kila kiumbe juu ya nchi kavu chenye pumzi ya uhai kikafa. Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali, watu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Noa peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Maji yakaifunika dunia kwa siku 150.

Shirikisha
Soma Mwanzo 7