Mwanzo 6:1-8
Mwanzo 6:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Binadamu walipozidi kuongezeka duniani na kuzaa wasichana, watoto wa kiume wa Mungu waliwaona hao wasichana wa watu kuwa ni wazuri, wakawachukua wale waliowapenda kuwa wake zao. Hapo Mwenyezi-Mungu akasema, “Roho yangu haitakaa ndani ya binadamu milele, maana yeye ni wa kufa tu. Basi, hataishi zaidi ya miaka 120.” Nyakati hizo na hata baadaye, kulikuwa na majitu duniani ambao walikuwa wazawa wa watoto wa kiume wa Mungu na wasichana wa watu. Hao ndio watu waliokuwa mashujaa na wenye sifa enzi hizo, nao waliitwa Wanefili. Mwenyezi-Mungu alipoona wingi wa uovu wa binadamu duniani, na kwamba kila analokusudia binadamu moyoni mwake ni ovu daima, Mwenyezi-Mungu alisikitika sana kwa kumuumba binadamu duniani. Mwenyezi-Mungu alihuzunika sana moyoni mwake, hivyo akasema, “Nitamfuta kabisa duniani binadamu niliyemuumba; nitafutilia mbali pia wanyama wa porini, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Ninasikitika kwamba niliwaumba duniani.” Lakini Noa alipata fadhili mbele ya Mwenyezi-Mungu.
Mwanzo 6:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wowote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni mwili; basi siku zake zitakuwa miaka mia moja na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemwumba mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewaumba. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.
Mwanzo 6:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.
Mwanzo 6:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Watu walipoanza kuongezeka idadi katika uso wa dunia na watoto wa kike wakazaliwa kwao, wana wa Mungu wakawaona kuwa hao binti za wanadamu walikuwa wazuri wa sura, wakaoa yeyote miongoni mwao waliyemchagua. Ndipo BWANA akasema, “Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye ni wa kufa, siku zake zitakuwa miaka 120.” Wanefili walikuwako duniani siku hizo, na baadaye, hao wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu na kuzaa nao. Wanefili walikuwa mashujaa na watu waliojulikana wa zamani hizo. BWANA akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. BWANA akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. Kwa hiyo BWANA akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.” Lakini Noa akapata kibali machoni pa BWANA.