Mwanzo 6:1-22
Mwanzo 6:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Binadamu walipozidi kuongezeka duniani na kuzaa wasichana, watoto wa kiume wa Mungu waliwaona hao wasichana wa watu kuwa ni wazuri, wakawachukua wale waliowapenda kuwa wake zao. Hapo Mwenyezi-Mungu akasema, “Roho yangu haitakaa ndani ya binadamu milele, maana yeye ni wa kufa tu. Basi, hataishi zaidi ya miaka 120.” Nyakati hizo na hata baadaye, kulikuwa na majitu duniani ambao walikuwa wazawa wa watoto wa kiume wa Mungu na wasichana wa watu. Hao ndio watu waliokuwa mashujaa na wenye sifa enzi hizo, nao waliitwa Wanefili. Mwenyezi-Mungu alipoona wingi wa uovu wa binadamu duniani, na kwamba kila analokusudia binadamu moyoni mwake ni ovu daima, Mwenyezi-Mungu alisikitika sana kwa kumuumba binadamu duniani. Mwenyezi-Mungu alihuzunika sana moyoni mwake, hivyo akasema, “Nitamfuta kabisa duniani binadamu niliyemuumba; nitafutilia mbali pia wanyama wa porini, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Ninasikitika kwamba niliwaumba duniani.” Lakini Noa alipata fadhili mbele ya Mwenyezi-Mungu. Ifuatayo ni habari juu ya Noa ambaye alikuwa ndiye mwadilifu pekee na ambaye hakuwa na lawama nyakati zake. Alikuwa mcha Mungu. Noa alikuwa na watoto watatu wa kiume: Shemu, Hamu na Yafethi. Mungu aliiona dunia kuwa imeharibika na kujaa ukatili. Naam, Mungu aliiangalia dunia, akaona kuwa imeharibika kabisa, kwa maana kila mtu alifuata njia yake mbovu. Mungu akamwambia Noa, “Nimeamua kuwaangamiza binadamu wote kwa sababu wameijaza dunia ukatili. Naam, nitawaangamiza kabisa pamoja na dunia! Kwa hiyo, jitengenezee safina kwa mbao za mpingo. Gawa vyumba ndani yake na ipake lami ndani na nje. Utaitengeneza hivi: Urefu wake mita 139, upana wake mita 25 na kimo chake mita 15. Safina hiyo iwe ya ghorofa tatu na yenye mlango pembeni. Itengenezee paa, kisha acha nafasi ipatayo nusu mita kati ya paa na dari. Nitaleta gharika ili kuangamiza viumbe vyote hai duniani. Kila kiumbe hai duniani kitakufa. Lakini nitafanya agano nawe. Utaingia katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao. Nawe utaingiza katika safina jozi ya kila aina ya viumbe, wa kiume na wa kike, ili kuwahifadhi hai pamoja nawe. “Utaingiza kila aina ya ndege wa angani, kila aina ya mnyama, kila aina ya kiumbe kitambaacho, wawiliwawili, ili kuwahifadhi hai. Pia chukua aina zote za vyakula vinavyolika, uvihifadhi kwa ajili ya chakula chenu na viumbe hao.” Noa akafanya yote kama Mungu alivyomwamuru.
Mwanzo 6:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wowote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni mwili; basi siku zake zitakuwa miaka mia moja na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemwumba mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewaumba. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA. Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu. Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu. Nuhu akazaa wana watatu wa kiume, Shemu, na Hamu, na Yafethi. Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma. Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; maana kila mtu duniani amepotoka. Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila kiumbe umefika mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia maovu, basi nitawaangamiza pamoja na dunia. Jitengenezee safina ya mti wa mvinje; tengeneza vyumba ukaifunike kwa lami ndani na nje. Hivi ndivyo utakavyoifanya; dhiraa mia tatu urefu wa safina, dhiraa hamsini upana wake, na dhiraa thelathini kwenda juu. Uifanyie safina mwangaza, ukaumalize juu kiasi cha mkono mmoja; ukautie mlango wa safina katika ubavu wake; ukaifanyie dari tatu, ya chini, ya pili, na ya tatu. Tazama, nitaleta gharika ya maji juu ya nchi, niharibu kila kitu chenye mwili na pumzi ya uhai, kisiwepo chini ya mbingu; kila kilichoko duniani kitakufa. Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za wanao, pamoja nawe. Na katika kila kilicho hai chenye mwili, wawili wa kila namna utawaleta ndani ya safina, kuwahifadhi pamoja nawe; wawe mume na mke. Katika vyote virukavyo kwa jinsi yake, na kila namna ya mnyama kwa jinsi yake, kila kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake, wawili wa kila namna watakuja kwako ili uwahifadhi. Ukajitwalie chakula cha kila namna kinacholika, ukakusanye, nacho kitakuwa ni chakula chenu na chao. Ndivyo alivyofanya Nuhu, sawasawa na vyote alivyomwamuru Mungu, hivyo ndivyo alivyofanya.
Mwanzo 6:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA. Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu. Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu. Nuhu akazaa wana watatu wa kiume, Shemu, na Hamu, na Yafethi. Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma. Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; maana kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani. Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia. Ujifanyie safina ya mti wa mvinje; fanya na vyumba ndani ya safina, ukaifunike ndani na nje kwa lami. Hivi ndivyo utakavyoifanya; mikono mia tatu urefu wa safina, mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake. Uifanyie safina mwangaza, ukaumalize juu kiasi cha mkono mmoja; ukautie mlango wa safina katika ubavu wake; ukaifanyie dari tatu, ya chini, ya pili, na ya tatu. Na tazama, nitaleta gharika ya maji juu ya nchi, niharibu kila kitu chenye mwili na pumzi ya uhai, kisiwepo chini ya mbingu; kila kilichoko duniani kitakufa. Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za wanao, pamoja nawe. Na katika kila kilicho hai chenye mwili, wawili wa kila namna utawaleta ndani ya safina, kuwahifadhi pamoja nawe; wawe mume na mke. Katika vyote virukavyo kwa jinsi yake, na kila namna ya mnyama kwa jinsi yake, kila kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake, wawili wa kila namna watakuja kwako ili uwahifadhi. Ukajitwalie chakula cha kila namna kinacholika, ukakusanye, nacho kitakuwa ni chakula chenu na chao. Ndivyo alivyofanya Nuhu, sawasawa na vyote alivyomwamuru Mungu, hivyo ndivyo alivyofanya.
Mwanzo 6:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Watu walipoanza kuongezeka idadi katika uso wa dunia na watoto wa kike wakazaliwa kwao, wana wa Mungu wakawaona kuwa hao binti za wanadamu walikuwa wazuri wa sura, wakaoa yeyote miongoni mwao waliyemchagua. Ndipo BWANA akasema, “Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye ni wa kufa, siku zake zitakuwa miaka 120.” Wanefili walikuwako duniani siku hizo, na baadaye, hao wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu na kuzaa nao. Wanefili walikuwa mashujaa na watu waliojulikana wa zamani hizo. BWANA akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. BWANA akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. Kwa hiyo BWANA akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.” Lakini Noa akapata kibali machoni pa BWANA. Hivi ndivyo vizazi vya Noa. Noa alikuwa mtu wa haki, na mkamilifu miongoni mwa watu wa wakati wake, tena alitembea na Mungu. Noa alikuwa na wana watatu: Shemu, Hamu na Yafethi. Wakati huu dunia ilikuwa imejaa uharibifu na ukatili machoni pa Mungu. Mungu akaona jinsi dunia ilivyoharibika, kwa maana watu wote duniani walikuwa wameharibu njia zao. Kwa hiyo Mungu akamwambia Noa, “Nitawaangamiza watu wote, kwa kuwa dunia imejaa ukatili kwa sababu yao. Hakika mimi nitaangamiza watu pamoja na dunia. Kwa hiyo jitengenezee safina kubwa kwa mbao za mvinje, tengeneza vyumba ndani yake na uipake lami ndani na nje. Hivi ndivyo utakavyoitengeneza: Safina iwe na urefu wa dhiraa 300, upana wake dhiraa hamsini na kimo chake dhiraa thelathini. Itengenezee paa na umalizie safina kwa kuacha nafasi ya dhiraa moja juu. Weka mlango ubavuni mwa safina, na uifanye ya ghorofa ya chini, ya kati na ya juu. Nitaleta gharika ya maji juu ya nchi ili kuangamiza uhai wote chini ya mbingu, kila kiumbe chenye pumzi ya uhai ndani yake. Kila kitu juu ya nchi kitaangamia. Lakini Mimi nitaweka Agano langu na wewe, nawe utaingia ndani ya Safina, wewe pamoja na mke wako, wanao na wake zao. Utaingiza ndani ya Safina kila aina ya kiumbe hai wawili wawili, wa kiume na wa kike, ili kuwahifadhi hai pamoja na wewe. Wawili wa kila aina ya ndege, wa kila aina ya mnyama na wa kila aina ya kitambaacho ardhini watakuja kwako ili wahifadhiwe hai. Utachukua kila aina ya chakula kitakacholiwa, na ukiweke akiba kama chakula kwa ajili yako na yao.” Noa akafanya kila kitu kama vile Mungu alivyomwamuru.