Mwanzo 50:15-21
Mwanzo 50:15-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya kifo cha baba yao, ndugu zake Yosefu walisemezana, “Huenda Yosefu atatuchukia na kutulipiza mabaya yote tuliyomtendea.” Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakisema, “Baba yako, kabla hajafariki, aliagiza hivi, ‘Mwambieni Yosefu kwa niaba yangu: Tafadhali uwasamehe ndugu zako makosa yao mabaya na maovu yote waliyokutendea.’ Sasa basi, tafadhali usamehe uovu tuliokutendea sisi watumishi wa Mungu wa baba yako.” Yosefu alipopata ujumbe huu, alilia. Kisha ndugu zake wakamjia, wakainama mpaka chini mbele yake, wakasema, “Tazama, sisi tu watumishi wako.” Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope, je, mimi ni badala ya Mungu? Nyinyi mlitaka kunitendea vibaya, lakini Mungu alikusudia mema ili watu wengi wapate kuwa hai kama mwonavyo leo. Haya, msiogope. Mimi nitawapeni chakula pamoja na watoto wenu.” Basi akawafariji na kusema nao vizuri.
Mwanzo 50:15-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakatuma watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwasamehe ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utusamehe kosa la watumishi wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Ndugu zake wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumishi wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.
Mwanzo 50:15-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.
Mwanzo 50:15-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndugu zake Yosefu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yosefu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?” Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya: ‘Hili ndilo mtakalomwambia Yosefu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yosefu akalia. Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.” Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu? Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi. Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawahakikishia na kusema nao kwa wema.