Mwanzo 50:14-26
Mwanzo 50:14-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya kumzika baba yake, Yosefu alirudi Misri pamoja na ndugu zake na watu wote waliokuwa wameandamana naye kwenda kumzika baba yake. Baada ya kifo cha baba yao, ndugu zake Yosefu walisemezana, “Huenda Yosefu atatuchukia na kutulipiza mabaya yote tuliyomtendea.” Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakisema, “Baba yako, kabla hajafariki, aliagiza hivi, ‘Mwambieni Yosefu kwa niaba yangu: Tafadhali uwasamehe ndugu zako makosa yao mabaya na maovu yote waliyokutendea.’ Sasa basi, tafadhali usamehe uovu tuliokutendea sisi watumishi wa Mungu wa baba yako.” Yosefu alipopata ujumbe huu, alilia. Kisha ndugu zake wakamjia, wakainama mpaka chini mbele yake, wakasema, “Tazama, sisi tu watumishi wako.” Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope, je, mimi ni badala ya Mungu? Nyinyi mlitaka kunitendea vibaya, lakini Mungu alikusudia mema ili watu wengi wapate kuwa hai kama mwonavyo leo. Haya, msiogope. Mimi nitawapeni chakula pamoja na watoto wenu.” Basi akawafariji na kusema nao vizuri. Yosefu akaendelea kukaa katika nchi ya Misri pamoja na jamaa yote ya baba yake. Aliishi kwa muda wa miaka 110. Yosefu alijaliwa kuwaona watoto na wajukuu wa mwanawe Efraimu, na pia kuwapokea kama wanawe watoto wa Makiri mwana wa Manase. Baadaye Yosefu aliwaambia ndugu zake, “Mimi sasa ninakaribia kufa. Lakini Mungu hakika atawajia kuwasaidia. Atawatoa katika nchi hii na kuwapelekeni katika nchi aliyowaapia Abrahamu, Isaka na Yakobo.” Kisha Yosefu akawaapiza wana wa Israeli, akisema, “Mungu atakapowajia kuwasaidia, hakikisheni kwamba mmeichukua mifupa yangu kutoka huku.” Basi, Yosefu akafariki kule Misri, akiwa na umri wa miaka 110. Nao wakaupaka mwili wake dawa usioze, wakauweka katika jeneza kule Misri.
Mwanzo 50:14-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yusufu akarudi Misri, yeye na ndugu zake, na wote waliokwenda pamoja naye kumzika baba yake, baada ya kumzika baba yake. Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakatuma watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwasamehe ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utusamehe kosa la watumishi wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Ndugu zake wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumishi wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema. Yusufu Akakaa katika Misri, yeye na nyumba ya baba yake. Yusufu Akaishi miaka mia moja na kumi. Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu. Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Abrahamu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu. Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia moja na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.
Mwanzo 50:14-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yusufu akarudi Misri, yeye na ndugu zake, na wote waliyokwenda pamoja naye kumzika babaye, baada ya kumzika babaye. Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema. Akakaa Yusufu katika Misri, yeye na nyumba ya babaye. Akaishi Yusufu miaka mia na kumi. Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu. Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu. Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.
Mwanzo 50:14-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya Yosefu kumzika baba yake, akarudi Misri pamoja na ndugu zake na wale wote waliokuwa wamekwenda naye kumzika baba yake. Ndugu zake Yosefu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yosefu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?” Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya: ‘Hili ndilo mtakalomwambia Yosefu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yosefu akalia. Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.” Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu? Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi. Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawahakikishia na kusema nao kwa wema. Yosefu akakaa katika nchi ya Misri, yeye pamoja na jamaa yote ya baba yake. Akaishi miaka 110, naye akaona kizazi cha tatu cha watoto wa Efraimu. Pia akaona watoto wa Makiri mwana wa Manase, wakawekwa magotini mwa Yosefu walipozaliwa. Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ninakaribia kufa. Lakini kwa hakika Mungu atawasaidia na kuwachukueni kutoka nchi hii na kuwapeleka katika nchi aliyomwahidi kwa kiapo Abrahamu, Isaki na Yakobo.” Naye Yosefu akawaapisha wana wa Israeli na kuwaambia, “Hakika Mungu atawasaidia, nanyi ni lazima mhakikishe mmepandisha mifupa yangu kutoka mahali hapa.” Kwa hiyo Yosefu akafa akiwa na umri wa miaka 110. Baada ya kumtia dawa ili asioze, akawekwa kwenye jeneza huko Misri.