Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 48:1-22

Mwanzo 48:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, baada ya mambo hayo, Yusufu akaambiwa, Tazama, baba yako hawezi; akawatwaa wanawe wawili, Manase na Efraimu, pamoja naye. Naye akaarifiwa Yakobo ya kwamba, Angalia, mwanao Yusufu anakuja kwako. Israeli akajitia nguvu, akaketi juu ya kitanda. Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani, akanibariki, akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha, nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada yako, iwe milki ya milele. Basi sasa wanao wawili uliozaliwa katika nchi ya Misri kabla sijaja kwako Misri ni watoto wangu, yaani, Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama Reubeni na Simeoni. Na wazao wako utakaozaa baada ya hawa watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao. Na mimi nilipokuja kutoka Padan, Raheli akanifia katika nchi ya Kanaani, njiani, si mwendo mkubwa kabla ya kufika Efrathi. Nikamzika katika njia ya Efrathi, ndio Bethlehemu. Israeli akawaona wana wa Yusufu, akasema, Ni nani hawa? Yusufu akamwambia babaye, Hawa ni wanangu, Mungu alionipa hapa. Akasema, Tafadhali uwalete kwangu nami nitawabariki. Na macho ya Israeli yalikuwa mazito kwa uzee, wala hakuweza kuona. Akawaleta kwake, naye akawabusu, na kuwakumbatia. Israeli akamwambia Yusufu, Sikudhani ya kwamba nitakuona uso wako, na Mungu amenionyesha na uzao wako pia. Yusufu akawatoa katika magoti yake, naye akainama kifudifudi Yusufu akawaweka wote wawili, Efraimu katika mkono wake wa kuume, kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli; na Manase katika mkono wake wa kushoto, kuelekea mkono wa kuume wa Israeli, akawasogeza karibu naye. Israeli akanyosha mkono wake wa kuume akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, huku akijua atiavyo mikono; maana Manase ndiye aliyezaliwa kwanza. Akambariki Yusufu, akasema, Mungu ambaye baba zangu, Ibrahimu na Isaka, walienenda mbele zake, yeye Mungu aliyenilisha, maisha yangu yote, hata siku hii ya leo, naye Malaika aliyeniokoa na maovu yote, na awabariki vijana hawa; jina langu na litajwe juu yao, na jina la baba zangu, Ibrahimu na Isaka; na wawe wingi wa watu kati ya nchi. Yusufu alipoona kwamba babaye anaweka mkono wake wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, ikawa vibaya machoni pake. Akauinua mkono wa babaye auondoe katika kichwa cha Efraimu, ili auweke juu ya kichwa cha Manase. Yusufu akamwambia babaye, Sivyo, babangu, maana huyu ni mzaliwa wa kwanza; weka mkono wako wa kuume kichwani pake. Babaye akakataa, akasema, Najua, mwanangu najua, yeye naye atakuwa taifa, yeye naye atakuwa mkuu; lakini ndugu yake mdogo atakuwa mkubwa kuliko yeye, na uzao wake watakuwa wingi wa mataifa. Akawabariki siku ile akasema, Katika ninyi Waisraeli watabariki, wakisema, Mungu na akufanye kama Efraimu na Manase. Akamweka Efraimu mbele ya Manase. Israeli akamwambia Yusufu, Angalia, mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, naye atawarudisha mpaka nchi ya baba zenu. Nami nimekupa wewe sehemu moja zaidi kuliko ndugu zako, niliyoitwaa katika mikono ya Waamori, kwa upanga wangu na upinde wangu.

Shirikisha
Soma Mwanzo 48

Mwanzo 48:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya hayo, Yosefu alipewa habari kwamba baba yake ni mgonjwa. Hivyo, akawachukua wanawe wawili, Manase na Efraimu, akaenda nao kwa baba yake. Yakobo alipofahamishwa kwamba mwanawe Yosefu amefika kumwona, akajitahidi kuinuka, akaketi kitandani. Yakobo akamwambia Yosefu, “Mungu mwenye nguvu alinitokea nilipokuwa kule Luzu katika nchi ya Kanaani, akanibariki. Aliniambia, ‘Tazama, nitakufanya uwe na wazawa na uongezeke; nitakufanya uwe babu wa jamii kubwa za watu. Ardhi hii nitawapa wazawa wako, waimiliki milele.’” Yakobo akaendelea kusema, “Wanao wawili uliowapata hapa Misri kabla sijafika, ni wanangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu kama walivyo Reubeni na Simeoni. Lakini, watoto utakaopata baadaye watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao. Naamua hivyo kwa sababu ya mama yako, Raheli. Nilipokuwa narudi kutoka Padani yeye alifariki katika nchi ya Kanaani, tukiwa karibu kufika Efratha, akaniachia huzuni. Basi, nikamzika papo hapo, kando ya njia iendayo Efratha, yaani Bethlehemu.” Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akamwuliza, “Ni akina nani hawa?” Yosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wanangu alionijalia Mungu nikiwa huku.” Israeli akasema, “Tafadhali, walete karibu nipate kuwabariki.” Macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee. Basi, Yosefu akawasogeza wanawe karibu na baba yake, naye akawabusu na kuwakumbatia. Kisha Israeli akamwambia Yosefu, “Sikutazamia kuuona uso wako tena; lakini, kumbe, Mungu amenijalia hata kuwaona watoto wako!” Hapo Yosefu akawaondoa wanawe kwenye magoti ya baba yake, kisha akainama kwa heshima. Yosefu akawainua wanawe wawili, Efraimu katika mkono wake wa kulia, akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa baba yake, na Manase katika mkono wake wa kushoto, akimwelekeza kwenye mkono wa kulia wa baba yake, akawasogeza kwa babu yao. Lakini Israeli akaipishanisha mikono yake: Mkono wake wa kulia akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, aliyekuwa mzaliwa wa kwanza. Kisha Israeli akambariki Yosefu, akisema, “Mungu ambaye babu zangu Abrahamu na Isaka walimtii maishani mwao, Mungu ambaye ameniongoza maishani mwangu hadi leo, na malaika ambaye aliniokoa katika mabaya yote, na awabariki vijana hawa! Jina langu na majina ya wazee wangu, Abrahamu na Isaka, yadumishwe katika vijana hawa; nao waongezeke kwa wingi duniani.” Yosefu alipoona kwamba baba yake ameuweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Efraimu hakupendezwa. Basi, akaushika mkono wa baba yake, akitaka kuuondoa juu ya kichwa cha Efraimu auweke juu ya kichwa cha Manase. Akamwambia baba yake, “Sivyo, baba! Huyu hapa ndiye mzaliwa wa kwanza. Tafadhali, uweke mkono wako wa kulia juu ya kichwa chake.” Lakini baba yake akakataa, akisema, “Najua, mwanangu, najua. Wana wa Manase pia watakuwa taifa kubwa na mashuhuri. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, na wazawa wake watakuwa mataifa mengi.” Basi, Israeli akawabariki siku hiyo, akisema, “Waisraeli watayatumia majina yenu kubarikia, watasema, ‘Mungu akutendee mema kama Efraimu na Manase!’” Ndivyo Israeli alivyomweka Efraimu mbele ya Manase. Kisha Israeli akamwambia Yosefu, “Kama uonavyo, mimi niko karibu kufa. Hata hivyo, Mungu atakuwa pamoja nanyi, na kuwarudisheni katika nchi ya babu zenu. Zaidi ya hayo, nimekupa wewe, wala si ndugu zako, eneo moja milimani, nililowanyanganya Waamori kwa upanga na upinde wangu.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 48

Mwanzo 48:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, baada ya mambo hayo, Yusufu akaambiwa, Tazama, baba yako ni mgonjwa; akawatwaa wanawe wawili, Manase na Efraimu, pamoja naye. Naye Yakobo akaarifiwa ya kwamba, Angalia, mwanao Yusufu anakuja kwako. Israeli akajitia nguvu, akaketi juu ya kitanda. Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani, akanibariki, akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha, nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada yako, iwe milki ya milele. Basi sasa wanao wawili uliozaliwa katika nchi ya Misri kabla sijaja kwako Misri ni watoto wangu, yaani, Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama Reubeni na Simeoni. Na wazao wako utakaozaa baada ya hawa watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao. Na mimi nilipokuja kutoka Padan, Raheli akanifia katika nchi ya Kanaani, njiani, si mwendo mkubwa kabla ya kufika Efrata. Nikamzika katika njia ya Efrata, ndio Bethlehemu. Israeli akawaona wana wa Yusufu, akasema, Ni nani hawa? Yusufu akamwambia babaye, Hawa ni wanangu, Mungu alionipa nikiwa hapa. Akasema, Tafadhali uwalete kwangu nami nitawabariki. Na macho ya Israeli yalikuwa mazito kwa uzee, wala hakuweza kuona vizuri. Akawaleta kwake, naye akawabusu, na kuwakumbatia. Israeli akamwambia Yusufu, Sikudhani ya kwamba nitakuona uso wako, na Mungu amenionesha na uzao wako pia. Yusufu akawatoa katika magoti yake, naye akainama kifudifudi Yusufu akawaweka wote wawili, Efraimu katika mkono wake wa kulia, kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli; na Manase katika mkono wake wa kushoto, kuelekea mkono wa kulia wa Israeli, akawasongeza karibu naye. Israeli akanyosha mkono wake wa kulia akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, huku akijua atiavyo mikono; maana Manase ndiye aliyezaliwa kwanza. Akambariki Yusufu, akasema, Mungu ambaye baba zangu, Abrahamu na Isaka, walienenda mbele zake, yeye Mungu aliyenilisha, maisha yangu yote, hata siku hii ya leo, naye Malaika aliyeniokoa na maovu yote, na awabariki vijana hawa; jina langu na litajwe juu yao, na jina la baba zangu, Abrahamu na Isaka; na wawe wingi wa watu kati ya nchi. Yusufu alipoona kwamba babaye anaweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Efraimu, ikawa vibaya machoni pake. Akauinua mkono wa babaye auondoe katika kichwa cha Efraimu, ili auweke juu ya kichwa cha Manase. Yusufu akamwambia babaye, Sivyo, babangu, maana huyu ni mzaliwa wa kwanza; weka mkono wako wa kulia kichwani pake. Babaye akakataa, akasema, Najua, mwanangu najua, yeye naye atakuwa taifa, yeye naye atakuwa mkuu; lakini ndugu yake mdogo atakuwa mkubwa kuliko yeye, na uzao wake watakuwa mataifa mengi Akawabariki siku ile akisema, Katika ninyi Waisraeli watabariki, wakisema, Mungu na akufanye kama Efraimu na kama Manase. Akamweka Efraimu mbele ya Manase. Israeli akamwambia Yusufu, Angalia, mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, naye atawarudisha mpaka nchi ya baba zenu. Nami nimekupa wewe sehemu moja zaidi kuliko ndugu zako, niliyoitwaa katika mikono ya Waamori, kwa upanga wangu na upinde wangu.

Shirikisha
Soma Mwanzo 48

Mwanzo 48:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya muda Yosefu akaambiwa kwamba, “Baba yako ni mgonjwa.” Kwa hiyo akawachukua wanawe wawili Manase na Efraimu, pamoja naye. Yakobo alipoambiwa, “Mwanao Yosefu amekujia kukuona,” Israeli akakusanya nguvu zake, akaketi kitandani. Yakobo akamwambia Yosefu, “Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu katika nchi ya Kanaani, huko akanibariki, naye akaniambia, ‘Nitakufanya ustawi na kuongezeka hesabu yako, nitakufanya kuwa jamii ya mataifa, nami nitakupa nchi hii uimiliki milele wewe na wazao wako baada yako.’ “Sasa basi, wanao wawili waliozaliwa kwako huku Misri kabla sijaja hapa kwako watahesabiwa kuwa ni wangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama vile Reubeni na Simeoni walivyo wangu. Lakini watoto utakaowazaa baada yao watakuwa wako. Katika nchi watakayoirithi, watatambuliwa kwa jina la ndugu zao. Nilipokuwa ninarudi kutoka Padani, katika huzuni yangu Raheli alifariki katika nchi ya Kanaani tulipokuwa tungali tukisafiri, tukiwa karibu kufika Efrathi. Kwa hiyo nilimzika huko, kando ya njia iendayo Efrathi” (yaani Bethlehemu). Wakati Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akauliza, “Hawa ni nani?” Yosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.” Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.” Basi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yosefu akawaleta wanawe karibu na baba yake, Israeli akawabusu na akawakumbatia. Israeli akamwambia Yosefu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.” Ndipo Yosefu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli naye akasujudu hadi nchi. Yosefu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao. Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa ndiye mdogo, na mkono wake wa kushoto akaukatisha, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase alikuwa ndiye mzaliwa wa kwanza. Ndipo akambariki Yosefu akisema, “Mungu ambaye baba zangu Abrahamu na Isaki walimtii, Mungu ambaye amekuwa mchungaji wa maisha yangu yote mpaka leo hii, Malaika ambaye aliniokoa kutoka madhara yote, yeye na awabariki vijana hawa. Na waitwe kwa jina langu na kwa majina ya baba zangu Abrahamu na Isaki, wao na waongezeke kwa wingi katika dunia.” Yosefu alipoona baba yake akiweka mkono wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, hakupendezwa, kwa hiyo akauchukua mkono wa baba yake kutoka kichwa cha Efraimu na kuuweka juu ya kichwa cha Manase. Yosefu akamwambia, “Hapana, baba yangu, huyu ndiye mzaliwa wa kwanza; uweke mkono wako wa kuume juu ya kichwa chake.” Lakini baba yake akakataa, akasema, “Ninajua, mwanangu, ninajua. Yeye pia atakuwa taifa, naye pia atakuwa mkuu. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, nao wazao wake watakuwa kundi la mataifa.” Akawabarikia siku ile na kusema, “Kwa jina lenu Israeli watatamka baraka hii: ‘Mungu na awafanye kama Efraimu na Manase.’ ” Kwa hiyo akamtanguliza Efraimu mbele ya Manase. Ndipo Israeli akamwambia Yosefu, “Mimi ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu. Kwako wewe, kama aliye juu ya ndugu zako, ninakupa sehemu moja zaidi ya ndugu zako, lile eneo nililoteka kwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 48