Mwanzo 47:13-22
Mwanzo 47:13-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wala hapakuwa na chakula katika nchi yote, kwa kuwa njaa ilikuwa nzito sana, hata nchi ya Misri, na nchi ya Kanaani zikataabika, kwa sababu ya njaa. Yusufu akakusanya fedha zote zilizoonekana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, kwa nafaka waliyoinunua. Yusufu akazileta zile fedha nyumbani mwa Farao. Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha. Yusufu akasema, Toeni wanyama wenu, nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu, kama fedha zenu zimekwisha. Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula badala ya farasi, na badala ya kondoo, na badala ya ng’ombe, na badala ya punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule. Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele ya bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu. Kwa nini tufe mbele ya macho yako, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu kwa chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao; kisha utupe mbegu, tuishi wala tusife, wala nchi yetu isipotee. Basi Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri; maana Wamisri waliuza kila mtu shamba lake; kwa sababu njaa ilikuwa imewazidi sana, nchi ikawa mali yake Farao. Akawahamisha hao watu, akawaweka katika miji, tangu upande huu wa Misri hata upande huu. Ila nchi ya makuhani hakuinunua; maana makuhani walikuwa na posho yao kutoka kwa Farao, wakala posho yao waliyopewa na Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao.
Mwanzo 47:13-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hata hivyo, hapakuwepo chakula katika sehemu yote kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana; Misri na Kanaani zote zikaharibiwa kwa sababu ya njaa. Yosefu akakusanya fedha zote zilizopatikana kutoka mauzo ya nafaka huko Misri na Kanaani, akazileta kwenye jumba la kifalme la Farao. Fedha za watu wa Misri na Kanaani zilipokwisha, Wamisri wote wakamjia Yosefu na kumwambia, “Tupatie chakula. Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Fedha zetu zimekwisha.” Yosefu akawaambia, “Basi leteni mifugo yenu, nitawauzia chakula kwa kubadilisha na mifugo yenu, kwa kuwa fedha zenu zimekwisha.” Kwa hiyo wakaleta mifugo yao kwa Yosefu, naye akawapa chakula kwa kubadilishana na farasi zao, kondoo na mbuzi zao, ngʼombe na punda zao. Katika mwaka huo wote Yosefu akawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote. Mwaka ule ulipokwisha, wakamjia mwaka uliofuata na kumwambia, “Hatuwezi kuficha ukweli mbele za bwana wetu kwamba, kwa kuwa fedha zetu zimekwisha na wanyama wetu ni mali yako, sasa hakuna chochote kilichosalia kwa ajili ya bwana wetu isipokuwa miili yetu na ardhi yetu. Kwa nini tuangamie mbele ya macho yako, sisi pamoja na nchi yetu? Utununue sisi pamoja na ardhi yetu ili kubadilishana kwa chakula. Nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao. Tupe sisi mbegu ili tuweze kuishi wala tusife, nchi yetu isije ikawa ukiwa.” Kwa hiyo Yosefu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri. Wamisri, mmoja baada ya mwingine, waliuza mashamba yao, kwa sababu njaa ilikuwa kali sana kwao. Nchi ikawa mali ya Farao, naye Yosefu akawafanya watu watumike kama watumwa, kuanzia upande mmoja wa Misri hadi upande mwingine. Hata hivyo, hakununua nchi ya makuhani, kwa sababu walikuwa wanapata mgawo wao wa kawaida kutoka kwa Farao, nao walikuwa na chakula cha kuwatosha kutokana na mgawo waliopewa na Farao. Hii ndiyo sababu hawakuuza ardhi yao.
Mwanzo 47:13-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadaye chakula kiliadimika kabisa nchini kote. Njaa ilikuwa kali sana hata ikawafanya watu wote katika nchi ya Misri na ya Kanaani kudhoofika. Yosefu akakusanya fedha yote ya nchi ya Misri na Kanaani kutokana na nafaka waliyonunua, akaipeleka fedha hiyo ikulu kwa Farao. Baada ya watu wote wa nchi ya Misri na Kanaani kutumia fedha yao yote Wamisri wote walimjia Yosefu na kumwambia, “Tupe chakula! Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Tazama, sasa fedha yetu imekwisha!” Yosefu akawaambia, “Kama fedha yenu imekwisha, basi nipeni mifugo yenu, nami nitawapa nafaka.” Ndipo wakamletea Yosefu mifugo yao: Farasi, ng'ombe, kondoo, mbuzi na punda, naye akawapa chakula. Mwaka huo Yosefu akawa anawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote. Mwaka uliofuata wakamjia tena na kumwambia, “Bwana, ukweli ni kwamba fedha yetu yote imekwisha, na wanyama wetu wamekuwa mali yako. Sasa, bwana, sisi watumishi wako hatuna chochote tunachoweza kukupa isipokuwa miili yetu na mashamba yetu. Ya nini sisi tufe mbele ya macho yako na mashamba yetu yaharibike? Utununue sisi pamoja na mashamba yetu, tuwe watumwa wa Farao, mradi tu utupe chakula. Tupe nafaka, tusije tukafa; utupe na mbegu kwa ajili ya mashamba yetu.” Hivyo Yosefu akainunua nchi yote ya Misri iwe mali ya Farao. Kila Mmisri alilazimika kuuza shamba lake, kwa jinsi njaa ilivyokuwa kali. Nchi yote ikawa mali ya Farao, na Yosefu akawafanya watu kuwa watumwa, kutoka pembe moja hadi pembe nyingine ya nchi ya Misri. Ardhi ambayo Yosefu hakuinunua ni ile iliyomilikiwa na makuhani. Hao hawakulazimika kuiuza ardhi yao kwani waliishi kwa posho maalumu waliyopewa na Farao.
Mwanzo 47:13-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baadaye hapakuwa na chakula katika nchi yote, kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana, hata nchi ya Misri na nchi ya Kanaani zikataabika, kwa sababu ya njaa. Yusufu akakusanya fedha zote zilizoonekana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, kwa nafaka waliyoinunua. Yusufu akazileta zile fedha nyumbani mwa Farao. Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha. Yusufu akasema, Toeni wanyama wenu, nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu, kama fedha zenu zimekwisha. Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula kwa kubadilisha na farasi, kondoo, ng'ombe na punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule. Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele za bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu. Kwa nini tufe mbele ya macho yako, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu kwa chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao; kisha utupe mbegu, tuishi wala tusife, wala nchi yetu isipotee. Basi Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri; maana Wamisri waliuza kila mtu shamba lake; kwa sababu njaa ilikuwa imewazidi sana, nchi ikawa mali yake Farao. Akawahamisha hao watu, akawaweka katika miji, tangu upande huu wa Misri hata upande huu. Ila nchi ya makuhani hakuinunua; maana makuhani walikuwa na posho yao kutoka kwa Farao, wakala posho yao waliyopewa na Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao.