Mwanzo 46:26-34
Mwanzo 46:26-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nafsi zote waliokuja pamoja na Yakobo mpaka Misri waliotoka viunoni mwake, bila wake za wanawe Yakobo, nafsi zote walikuwa sitini na sita. Na wana wa Yusufu aliozaliwa katika Misri walikuwa nafsi wawili. Nafsi zote za nyumba ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini. Yakobo akampeleka Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni. Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionyesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake kitambo kizima. Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai. Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia. Na watu hao ni wachungaji, maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng’ombe zao, na yote waliyo nayo. Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini? Semeni, Watumwa wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.
Mwanzo 46:26-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Jumla ya wazawa wa Yakobo aliokwenda nao Misri, bila kuwahesabu wake za wanawe, ilikuwa watu sitini na sita. Huko nchini Misri Yosefu alikuwa amepata wana wawili. Kwa hiyo watu wote wa jamaa ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini. Yakobo akamtanguliza Yuda kwa Yosefu kumwomba waonane huko Gosheni; nao wakafika katika eneo la Gosheni. Yosefu akapanda gari lake la farasi, akaenda kumlaki Israeli, baba yake, huko Gosheni. Alipomfikia baba yake, alimkumbatia na kulia kwa kitambo kirefu. Israeli akamwambia Yosefu, “Hata nikifa sasa si kitu kwa kuwa nimeuona uso wako na kujua kwamba wewe u hai!” Yosefu akawaambia ndugu zake na jamaa yote ya baba yake, “Nakwenda kumwarifu Farao kwamba ndugu zangu na jamaa yote ya baba yangu waliokuwa katika nchi ya Kanaani wamekuja kwangu. Nitamweleza kwamba nyinyi ni wachungaji kwani mmekuwa mkichunga mifugo, na kwamba mmewasili pamoja na mbuzi, kondoo, ng'ombe na mali yenu yote. Basi, Farao akiwaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’ Semeni: ‘Bwana, sisi watumishi wako, ni wafugaji wa mifugo tangu utoto wetu mpaka leo, kwani ndivyo walivyokuwa babu zetu’; semeni hivyo ili mruhusiwe kukaa katika eneo la Gosheni.” Yosefu alisema hivyo kwa sababu kwa Wamisri wachungaji wote wa kondoo ni chukizo.
Mwanzo 46:26-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Watu wote waliokuja pamoja na Yakobo mpaka Misri, waliokuwa wazawa wake, bila wake za wanawe, walikuwa watu sitini na sita. Na wana wa Yusufu aliozaliwa katika Misri walikuwa wawili. Watu wote wa nyumba ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini. Yakobo akamtuma Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni. Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake kitambo kirefu. Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai. Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia. Na watu hao ni wachungaji, maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo. Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini? Semeni, Watumishi wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.
Mwanzo 46:26-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wote waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe zake, walikuwa watu sitini na sita. Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yosefu huko Misri, jumla yote ya jamaa ya Yakobo, waliokwenda Misri, walikuwa sabini. Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yosefu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni, gari kubwa zuri la Yosefu liliandaliwa, naye akaenda Gosheni kumlaki baba yake Israeli. Mara Yosefu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu. Israeli akamwambia Yosefu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.” Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu. Watu hao ni wachunga mifugo, huchunga mifugo, wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ngʼombe pamoja na kila kitu walicho nacho.’ Farao atakapowaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’ Mjibuni, ‘Watumwa wako wamekuwa wachunga mifugo tangu ujana wetu mpaka sasa, kama baba zetu walivyofanya.’ Ndipo mtakaporuhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wachunga mifugo wote ni chukizo kwa Wamisri.”