Mwanzo 46:1-7
Mwanzo 46:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Israeli akaanza safari yake pamoja na mali yake yote. Alipofika Beer-sheba, akamtolea tambiko Mungu wa Isaka, baba yake. Mungu akaongea na Israeli katika maono usiku, akamwita, “Yakobo! Yakobo!” Yakobo akaitika, “Naam nasikiliza.” Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu, Mungu wa baba yako. Usiogope kwenda Misri; utakapokuwa huko, nitakufanya uwe taifa kubwa. Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe huko Misri na kukurudisha huku. Utakapofariki, mkono wa Yosefu ndio utakaoyafumba macho yako.” Basi, Yakobo akaondoka Beer-sheba. Wanawe wakamchukua yeye, watoto wao wachanga pamoja na wake zao katika magari ambayo Farao alipeleka kumchukua. Walichukua pia mifugo na mali yao yote waliyokuwa wamechuma katika nchi ya Kanaani, wakaenda Misri. Yakobo aliwachukua wazawa wake wote: Wanawe, wajukuu wake wa kiume na wa kike, wote akawaleta Misri.
Mwanzo 46:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Israeli Akasafiri, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye. Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako. Yakobo akaondoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyotuma Farao ili kumchukua. Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamepata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye. Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri.
Mwanzo 46:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akasafiri Israeli, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye. Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako. Yakobo akaondoka kutoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyoyapeleka Farao ili kumchukua. Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye. Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri.
Mwanzo 46:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hivyo Israeli akaondoka na vyote vilivyokuwa mali yake, naye alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaki baba yake. Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!” Akajibu, “Mimi hapa.” Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako, usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa. Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yosefu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.” Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao aliyokuwa amempelekea kumsafirisha. Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani, Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri. Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote mpaka Misri.