Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 45:1-28

Mwanzo 45:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Hapo Yosefu akashindwa kujizuia mbele ya wote walioandamana naye, akawaamuru watoke nje. Hivyo Yosefu alikuwa peke yake alipojitambulisha kwa ndugu zake. Lakini alilia kwa sauti kubwa hata Wamisri wakamsikia, hali kadhalika na watu wa jamaa ya Farao nao wakamsikia. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu. Je, baba yangu angali hai?” Lakini ndugu zake wakapigwa na bumbuazi mbele yake, hata wakashindwa kumjibu. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, sogeeni karibu nami.” Walipomkaribia, akawaambia, “Mimi ndiye ndugu yenu Yosefu, mliyemwuza Misri. Lakini sasa msifadhaike wala kujilaumu kwa kuniuza. Mungu ndiye aliyenileta huku niwatangulie, ili niyaokoe maisha ya watu. Huu ni mwaka wa pili tu wa njaa nchini, na bado kuna miaka mitano zaidi ambapo watu hawataweza kulima wala kuvuna mavuno. Mungu alinileta huku niwatangulie, ili kusalimisha maisha yenu mbaki hai nchini na kuwakomboa kwa ukombozi mkubwa. Kwa hiyo, si nyinyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Ndiye aliyenifanya kama baba kwa Farao, msimamizi wa nyumba yake yote na mtawala wa nchi yote ya Misri. Basi, fanyeni haraka, mwende kwa baba na kumwambia, ‘Yosefu, mwana wako, anasema: Mungu amenifanya kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri. Basi, usikawie kuja kwangu. Utakaa karibu nami katika eneo la Gosheni: Wewe, wana wako na wajukuu wako, mifugo yako na mali yako yote. Utakapokuwa Gosheni, mimi nitakutunza wewe, jamaa yako pamoja na mifugo yako ili msije mkafa njaa, kwani bado miaka mitano zaidi ya njaa.’” Kisha Yosefu akasema, “Nyinyi wenyewe mmeona kwa macho yenu na hata ndugu yangu Benyamini ameona kwa macho yake kwamba ni mimi mwenyewe Yosefu ninayezungumza nanyi. Ni lazima kumwambia baba yangu juu ya fahari yangu huku Misri na yote mliyoyaona. Basi, fanyeni haraka, mkamlete baba yangu huku.” Kisha Yosefu akamkumbatia Benyamini, nduguye, akalia; Benyamini naye akalia, huku wamekumbatiana. Akiwa bado analia, Yosefu akawakumbatia ndugu zake na kuwabusu. Hapo ndipo ndugu zake walipoweza kuzungumza naye. Habari hizo zilipofika ikulu ya mfalme, kwamba ndugu za Yosefu wamekuja, zikamfurahisha sana Farao na watumishi wake. Kwa hiyo, Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako wawapakie punda wao mizigo, warudi nchini Kanaani, wamlete hapa baba yao na jamaa zao wote. Mimi nitawapa sehemu nzuri kabisa ya nchi ya Misri, ambako wataweza kufurahia matunda yote ya nchi hii. Waambie pia wachukue kutoka hapa magari ya kukokotwa ya kuwaleta watoto wao wachanga na wake zao na wala wasikose kumleta baba yao. Waambie wasijali juu ya mali zao maana sehemu nzuri kuliko zote katika nchi ya Misri itakuwa yao.” Basi, wana wa Israeli wakafanya kama walivyoagizwa. Yosefu akawapa magari kulingana na maagizo ya Farao na chakula cha njiani. Aliwapa kila mmoja wao mavazi ya kubadili, lakini akampa Benyamini vipande 300 vya fedha na mavazi matano ya kubadili. Tena alimpelekea baba yake zawadi hizi kwa ajili ya safari yake: Punda kumi waliobeba bidhaa bora za Misri, punda jike kumi waliobeba nafaka, mikate na vyakula vingine. Basi, Yosefu akaagana na ndugu zake. Walipokuwa wanaondoka aliwaonya akisema, “Msigombane njiani!” Basi, wakatoka Misri na kurudi nyumbani kwa baba yao Yakobo, nchini Kanaani. Wakamwambia baba yao, “Yosefu yu hai! Yeye ndiye mtawala wa nchi yote ya Misri!” Hapo baba yao akapigwa na bumbuazi, kwani hakuweza kuyasadiki maneno yao. Lakini, walipomsimulia yote waliyoagizwa na Yosefu na alipoyaona magari aliyopelekewa na Yosefu kumchukua, moyo wake ukajaa furaha kupita kiasi. Israeli akasema, “Sasa nimeridhika; mwanangu Yosefu yu hai! Nitakwenda nimwone kabla sijafa.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 45

Mwanzo 45:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinituma mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo ya kulima wala kuvuna. Mungu alinituma mbele yenu kuwahifadhia mabaki katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. Basi si ninyi mlionileta huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri. Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu, Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie. Nawe utakaa katika nchi ya Gosheni, utakuwa karibu nami, wewe, na wanao, na wana wa wanao, na wanyama wako, ng'ombe wako, na yote uliyo nayo. Nami nitakulisha huko; maana bado imesalia miaka mitano ya njaa; usije ukaingia katika uhitaji, wewe, na nyumba yako, na yote uliyo nayo. Na tazama, macho yenu yanaona, na macho ya ndugu yangu Benyamini, ya kwamba ni kinywa changu mimi kinachosema nanyi. Nanyi mtamwarifu baba yangu habari za fahari yangu yote katika Misri, na za vyote mlivyoviona; mkafanye haraka kumleta huku baba yangu. Akaanguka shingoni mwa ndugu yake Benyamini, akalia; Benyamini naye akalia shingoni mwake. Akawabusu ndugu zake wote, akalia nao, baada ya hayo, nduguze wakazungumza naye. Habari ikasikika nyumbani mwa Farao kusema, Ndugu zake Yusufu wamekuja. Ikawa vema machoni pa Farao, na machoni pa watumishi wake. Farao akamwambia Yusufu, Uwaambie ndugu zako, Fanyeni hivi; wabebesheni mizigo wanyama wenu, mwondoke mwende nchi ya Kanaani; kisha mkamtwae baba yenu, na watu wa nyumbani mwenu, mkanijie; nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi. Nawe umeamriwa; fanyeni hivi, mjitwalie magari katika nchi ya Misri kwa watoto wenu wadogo na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. Wala msivisumbukie vyombo vyenu, maana mema ya nchi yote ya Misri ni yenu. Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Na baba yake akampelekea vifuatavyo: punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda majike kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula cha njiani kwa babaye. Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani. Wakatoka Misri, wakafika nchi ya Kanaani kwa Yakobo, baba yao. Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki. Wakamwambia maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyotuma Yusufu, ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka. Israeli akasema, Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa.

Shirikisha
Soma Mwanzo 45

Mwanzo 45:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri. Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu, Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie. Nawe utakaa katika nchi ya Gosheni, utakuwa karibu nami, wewe, na wanao, na wana wa wanao, na wanyama wako, ng’ombe zako, na yote uliyo nayo. Nami nitakulisha huko; maana bado imesalia miaka mitano ya njaa; usije ukaingia katika uhitaji, wewe, na nyumba yako, na yote uliyo nayo. Na tazama, macho yenu yanaona, na macho ya ndugu yangu Benyamini, ya kwamba ni kinywa changu mimi kinachosema nanyi. Nanyi mtamwarifu baba yangu habari za fahari yangu yote katika Misri, na za vyote mlivyoviona; mkafanye haraka kumleta huku baba yangu. Akaanguka shingoni mwa ndugu yake Benyamini, akalia; Benyamini naye akalia shingoni mwake. Akawabusu ndugu zake wote, akalia nao, baada ya hayo, nduguze wakazungumza naye Habari ikasikika nyumbani mwa Farao kusema, Ndugu zake Yusufu wamekuja. Ikawa vema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake. Farao akamwambia Yusufu, Uwaambie ndugu zako, Fanyeni hivi; wachukuzeni mizigo wanyama wenu, mwondoke mwende nchi ya Kanaani; kisha mkamtwae baba yenu, na watu wa nyumbani mwenu, mkanijie; nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi. Nawe umeamriwa; fanyeni hivi, mjitwalie magari katika nchi ya Misri kwa watoto wenu wadogo na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. Wala msivisumbukie vyombo vyenu, maana mema ya nchi yote ya Misri ni yenu. Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani. Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani. Wakatoka Misri, wakafika nchi ya Kanaani kwa Yakobo, baba yao. Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki. Wakamwambia maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyoyapeleka Yusufu, ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka. Israeli akasema, Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa.

Shirikisha
Soma Mwanzo 45

Mwanzo 45:1-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hapo Yosefu hakuweza kujizuia zaidi mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye, akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwepo mtu yeyote pamoja na Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake. Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake. Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimuuza Misri! Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna. Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu. “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote. Sasa rudini haraka kwa baba yangu na mwambieni, ‘Hili ndilo mwanao Yosefu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa bwana wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie. Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami, wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na vyote ulivyo navyo. Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulio nao mtakuwa fukara.’ “Mnaweza kujionea wenyewe, hata ndugu yangu Benyamini, kwamba hakika ni mimi ninayezungumza nanyi. Mwambieni baba yangu juu ya heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.” Ndipo akamkumbatia Benyamini ndugu yake na kulia, naye Benyamini akamkumbatia akilia. Pia akawabusu ndugu zake wote, huku akilia. Baada ya hayo ndugu zake wakazungumza naye. Habari zilipofika kwenye jumba la Farao kwamba ndugu zake Yosefu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi. Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi mpaka nchi ya Kanaani, mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri nanyi mtafurahia unono wa nchi.’ “Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri, kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. Msijali kamwe kuhusu mali zenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’ ” Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yosefu akawapa magari ya kukokotwa, kama Farao alivyoagiza, pia akawapa mahitaji kwa ajili ya safari yao. Kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli 300 za fedha, na jozi tano za nguo. Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliochukua vitu vizuri vya Misri, punda wake kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari. Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!” Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani. Wakamwambia baba yao, “Yosefu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuazi; hakuwasadiki. Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yosefu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yosefu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa. Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yosefu bado yu hai. Nitakwenda nikamwone kabla sijafa.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 45