Mwanzo 39:7-23
Mwanzo 39:7-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu chochote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nimkosee Mungu? Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala kuwa naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani afanye kazi yake, na hapakuwa na mtu yeyote kati ya wale wa nyumbani karibu; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje. Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje, akawaita watu wa nyumbani mwake, akasema nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia kwangu ili alale nami, nikalia kwa sauti kuu. Ikawa, aliposikia ya kuwa nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo yake kwangu, akakimbia, akatoka nje. Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana wake aje nyumbani. Naye akamwambia maneno yayo hayo, akisema, Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kwangu anidhihaki. Ikawa nilipopaza sauti yangu, nikalia, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje. Ikawa bwana wake aliposikia maneno aliyoambia na mkewe, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo kama haya, hasira yake ikawaka. Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani, mahali wafungwa wa mfalme walimokuwa wamefungiwa, naye akawa humo gerezani. Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliokuwemo gerezani; na yote yaliyofanywa humo, yeye ndiye aliyeyafanya. Wala mkuu wa gereza hakufuatilia kazi liliyokuwa mikononi mwa Yusufu; kwa kuwa BWANA alikuwa pamoja naye. BWANA akayafanikisha yote aliyoyafanya.
Mwanzo 39:7-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, baada ya muda fulani, mke wa Potifa akamtamani Yosefu na kumwambia, “Lala na mimi”. Lakini Yosefu akakataa na kumwambia huyo bwana wake, “Kamwe! Bwana wangu amenipa mamlaka juu ya kila kitu hapa nyumbani na, kwa vile niko, hajishughulishi na kitu chochote tena. Hapa nyumbani yeye hana madaraka kuliko mimi. Yeye hakunikataza kushika chochote isipokuwa wewe tu kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu mbaya kama huo, na kumkosea Mungu.” Huyo mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, lakini Yosefu hakumsikiliza wala kukubali kulala naye kamwe. Siku moja, Yosefu aliingia nyumbani kufanya kazi yake kama kawaida, na wafanyakazi wengine hawakuwamo nyumbani. Basi, mke wa Potifa alimshika joho lake na kumwambia, “Lala na mimi!” Lakini Yosefu akamwachia vazi lake mikononi mwake, akakimbilia nje. Hapo, yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu ameliacha vazi lake mikononi mwake na kukimbilia nje, akawaita watumishi wa nyumbani mwake na kuwaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania tuliyeletewa anatuaibisha. Alikuja kwangu akitaka kunishika kwa nguvu, lakini nikapiga kelele. Aliposikia napiga kelele, aliliacha vazi lake, akakimbilia nje!” Basi, yule mwanamke akaliweka vazi hilo mpaka mumewe aliporudi nyumbani. Akamsimulia kisa kile akisema, “Huyu mtumishi Mwebrania uliyemleta kwetu alinijia ili kuniaibisha. Lakini mara tu nilipopiga kelele, aliliacha vazi lake na kukimbilia nje.” Basi, bwana wake Yosefu alipoyasikia maneno ya mkewe, kwamba ndivyo mtumishi wake alivyomtendea, akawaka hasira, akamchukua Yosefu na kumtia gerezani, mahali walipofungwa wahalifu wa mfalme. Lakini hata humo gerezani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu akimfadhili hata kumfanya apendeke mbele ya mkuu wa gereza. Hivyo mkuu wa gereza alimweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa wote humo gerezani; kila kitu kilichofanyika humo kilifanywa kwa mamlaka yake. Huyo mkuu wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote alichokabidhiwa Yosefu kwa maana Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu na kufanikisha kila kitu alichofanya.
Mwanzo 39:7-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu? Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje. Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje, akawaita watu wa nyumbani mwake, akasema nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia kwangu, ili alale nami, nikalia kwa sauti kuu. Ikawa, aliposikia ya kuwa nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo yake kwangu, akakimbia, akatoka nje. Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana wake aje nyumbani. Naye akamwambia kama maneno hayo, akisema, Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kwangu anidhihaki. Ikawa nilipopaza sauti yangu, nikalia, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje. Ikawa bwana wake aliposikia maneno ya mkewe aliyomwambia, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo kama haya, hasira yake ikawaka. Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani, mahali walipofungwa wafungwa wa mfalme, naye akawamo humo gerezani. Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya. Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu; kwa kuwa BWANA alikuwa pamoja naye. BWANA akayafanikisha yote aliyoyafanya.
Mwanzo 39:7-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
baada ya kitambo mke wa Potifa akamtamani Yosefu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!” Lakini Yosefu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa katika uongozi, bwana wangu hahusiki na kitu chochote katika nyumba hii, kila kitu alicho nacho amenikabidhi. Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu chochote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?” Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, Yosefu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye. Siku moja Yosefu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwepo na mfanyakazi yeyote ndani ya nyumba. Mke wa Potifa akashika vazi Yosefu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yosefu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia. Yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu amemwachia vazi lake mkononi na kukimbilia nje ya nyumba, akawaita watumishi wake wa nyumbani, akawaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania ameletwa hapa kutudhihaki! Aliingia hapa ndani ili akutane nami kimwili, lakini nikapiga kelele. Aliposikia kelele za kuomba msaada, akaacha vazi lake kando yangu akakimbilia nje.” Yule mwanamke akaliweka lile vazi karibu naye mpaka Potifa aliporudi nyumbani. Ndipo akamweleza kisa hiki, akisema: “Yule mtumwa wa Kiebrania uliyetuletea alinijia ili kunidhihaki. Lakini mara nilipopiga kelele kuomba msaada, akaliacha vazi lake kando yangu akakimbia nje ya nyumba.” Potifa aliposikia kisa hiki mkewe alichomweleza, akisema, “Hivi ndivyo mtumwa wako alivyonitenda.” Hasira ya Potifa ikawaka. Potifa akamchukua Yosefu na kumweka gerezani, mahali ambapo wahalifu wa mfalme walikuwa wamefungwa. Lakini wakati Yosefu alipokuwa huko gerezani, BWANA alikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza. Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani. Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yosefu, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja na Yosefu akimfanikisha kwa kila alichofanya.