Mwanzo 39:2-6
Mwanzo 39:2-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, akamfanikisha sana. Yosefu akawa anakaa katika nyumba ya bwana wake, Mmisri. Huyo bwana wake akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, na kwamba ndiye aliyeyafanikisha mambo yote aliyofanya Yosefu. Basi, Yosefu akapendeka sana mbele ya Potifa, hata akawa ndiye mtumishi wake binafsi; alimfanya msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake yote. Tokea wakati Potifa alipomfanya Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake, Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya huyo Mmisri kwa ajili ya Yosefu. Baraka za Mwenyezi-Mungu zikawa juu ya kila alichokuwa nacho, nyumbani na shambani. Kwa sababu hiyo Potifa alimpa Yosefu mamlaka juu ya mambo yake yote, naye Potifa akaacha kushughulika na chochote isipokuwa tu chakula chake mwenyewe. Yosefu alikuwa kijana mzuri na wa kupendeza.
Mwanzo 39:2-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Baraka za BWANA zikawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu chochote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri.
Mwanzo 39:2-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri.
Mwanzo 39:2-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA alikuwa pamoja na Yosefu, naye akastawi, Yosefu akaishi nyumbani kwa bwana wake Mmisri. Potifa alipoona kuwa BWANA alikuwa pamoja na Yosefu na kwamba BWANA alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya, Yosefu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamkabidhi kuwa mwangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba na mali zake zote alizokuwa nazo, BWANA aliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yosefu. Baraka ya BWANA ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani. Kwa hiyo Potifa akamwachia Yosefu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho, Yosefu alipokuwa katika uongozi, Potifa hakuwa na sababu ya kujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula. Yosefu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia