Mwanzo 38:12-30
Mwanzo 38:12-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha binti Shua, mkewe Yuda, akafariki. Yuda alipomaliza kufanya matanga akaondoka na rafiki yake Hira, Mwadulami, wakaenda Timna kwa wakata-manyoya ya kondoo wake. Tamari aliposikia kwamba baba mkwe wake alikuwa njiani kwenda Timna kukata manyoya ya kondoo wake, alivua mavazi yake ya ujane na kujifunika shela kisha akaketi penye lango la kuingilia Enaimu, kijiji kilichokuwa njiani kwenda Timna. Alifanya hivyo kwa vile aliona kwamba Shela alikwisha kuwa mtu mzima, lakini yeye Tamari hakuozwa awe mkewe. Basi, Yuda alipomkuta Tamari hapo, alimdhania kuwa mwanamke malaya, kwani alikuwa amejifunika uso. Hapo, bila kujua kwamba huyo alikuwa mke wa mwanawe, akamwendea pale kando ya njia, akamwambia, “Napenda kulala nawe.” Tamari akamwuliza, “Utanipa nini nikikubali?” Yuda akamjibu, “Nitakupa mwanambuzi kutoka kundi langu.” Tamari akamwambia, “Weka rehani kuthibitisha utaniletea huyo mwanambuzi.” Yuda akamwuliza, “Unataka nikupe nini kama rehani?” Naye akamjibu, “Nipe hiyo pete na kamba yake pamoja na hiyo fimbo unayoshika.” Basi, Yuda akampa vitu hivyo vyote, akalala naye. Tamari akapata mimba yake. Basi, Tamari akarudi nyumbani akavua ile shela aliyojifunika, akavaa tena mavazi yake ya ujane. Wakati Yuda alipomtuma yule rafiki yake, Mwadulami, ampelekee yule mwanamke mwanambuzi ili arudishiwe rehani aliyomwachia, Hira hakumpata. Hira akawauliza wenyeji wa Enaimu, “Yuko wapi yule mwanamke kahaba aliyekuwa kando ya njia karibu na hapa?” Wakamjibu, “Hapa hapajawa na mwanamke kahaba.” Basi, huyo rafiki akarudi kwa Yuda, akamwambia, “Sikumpata! Tena wenyeji wa huko wameniambia kwamba hapajawa na mwanamke kahaba yeyote huko.” Yuda akasema, “Acha avichukue vitu hivyo, la sivyo atatufanya tuchekwe. Wewe mwenyewe umeona kwamba nilimpelekea mwanambuzi, lakini wewe hukumpata.” Baada ya miezi mitatu, Yuda akapata habari, “Tamari, mke wa mwanao amekuwa kahaba, tena amepata mimba kwa kufanya ukahaba.” Basi, Yuda akaamuru, “Mtoeni nje achomwe moto!” Walipokuwa wakimtoa nje, Tamari akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake, akisema, “Mwenye vitu hivi ndiye aliyenipa mimba. Kwa hiyo, nakuomba umtambue mwenye pete hii na kamba yake, na fimbo hii.” Yuda alivitambua vitu hivyo, akasema, “Tamari ni mwadilifu kuliko mimi. Ni kweli, maana sikumwoza kwa mwanangu Shela.” Tokea siku hiyo Yuda hakulala tena na Tamari. Wakati wa kujifungua kwake Tamari ulipofika, ikafahamika kuwa alikuwa na mimba ya mapacha. Basi, alipopata uchungu wa kuzaa pacha mmojawapo alitoa mkono nje, naye mkunga akaufunga kwa uzi mwekundu, akisema, “Huyu ndiye aliyezaliwa kwanza.” Lakini huyo mtoto alipourudisha mkono wake ndani, ndugu yake akazaliwa wa kwanza. Mkunga akasema, “Mbona wewe umepita kwa nguvu?” Kwa hiyo akaitwa Peresi. Baadaye ndugu yake akazaliwa akiwa na ule uzi mwekundu mkononi, naye akaitwa Zera.
Mwanzo 38:12-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku nyingi zikapita, akafa binti Shua, mkewe Yuda. Yuda akafarijika, akaenda kwa watu wake wawakatao kondoo manyoya huko Timna, yeye na mwenzake Hira, Mwadulami. Huyo Tamari akapewa habari, kusema, Mkweo anakwenda Timna, akate manyoya ya kondoo wake. Basi akavua nguo za ujane wake, akajivika utaji, akajifunika uso, akakaa mlangoni pa Enaimu, karibu na njia ya kuendea Timna. Maana aliona ya kwamba Shela amekuwa mtu mzima, ijapokuwa hakuozwa awe mkewe. Yuda alipomwona alimdhania kuwa ni kahaba, maana amejifunika uso. Akamgeukia kando ya njia, akasema, Niruhusu niingie kwako. Maana hakujua ya kuwa ni mkwewe. Akamwuliza, Utanipa nini, ukiingia kwangu? Akasema, Nitakuletea mwana-mbuzi kutoka kundini. Naye akamwuliza, Je! Utanipa rehani hata utakapomleta? Akasema, Nikupe rehani gani? Akamjibu, Pete yako ya mhuri, na kamba yake, na fimbo yako iliyo mkononi mwako. Basi akampa, akaingia kwake, naye akapata mimba. Akaondoka, akaenda zake, akavua utaji wake, na kuvaa mavazi ya ujane wake. Yuda akapeleka yule mwana-mbuzi kwa mkono wa rafiki yake Mwadulami, ili aipate rehani mkononi mwa huyo mwanamke lakini hakumkuta. Akauliza watu wa mji ule, akisema, Yuko wapi yule kahaba aliyekuwapo Enaimu kando ya njia? Wakasema, Hakuwako hapa kahaba. Akamrudia Yuda akasema, Sikumwona; hata na watu wa mahali hapo walisema, Hakuwako kahaba. Yuda akasema, Na aichukue yeye, tusije tukatiwa aibu; tazama, nimempelekea mbuzi huyu, wala hukumkuta. Ikawa baada ya miezi mitatu Yuda akapewa habari kwamba, Mke wa mwana wako, Tamari, amefanya uzinifu, naye ana mimba ya haramu. Yuda akasema, Mtoeni ateketezwe. Alipotolewa, alituma watu kwa mkwewe, akisema, Mimi nimepewa mimba na mtu mwenye vitu hivi. Akasema, Tambua basi, vitu hivi ni vya nani, pete hii, na kamba hii, na fimbo hii. Yuda akavikiri, akasema, Yeye ni mwenye haki kuliko mimi, kwa kuwa sikumpa Shela, mwanangu. Wala hakumjua tena baada ya hayo. Ikawa, wakati wake wa kuzaa walikuwapo mapacha tumboni mwake. Ikawa alipokuwa akizaa, mtoto mmoja akatoa mkono, mkunga akautwaa uzi mwekundu akaufunga mkononi mwake, huku akisema, Huyu ametoka kwanza. Ikawa aliporudisha mkono wake, tazama, ndugu yake akatoka. Akasema, Mbona umepita kwa nguvu wewe? Mambo ya nguvu na yakuandame. Kwa hiyo jina lake likaitwa Peresi Akatoka ndugu yake baadaye, ana uzi mwekundu mkononi mwake; naye akaitwa jina lake Zera.
Mwanzo 38:12-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku nyingi zikapita, akafa binti Shua, mkewe Yuda. Yuda akafarijika, akaenda kwa watu wake wawakatao manyoya kondoo huko Timna, yeye na mwenzake Hira, Mwadulami. Huyo Tamari akapewa habari, kusema, Mkweo anakwenda Timna, akate manyoya ya kondoo zake. Basi akavua nguo za ujane wake, akajivika utaji, akajifunika uso, akakaa mlangoni pa Enaimu, karibu na njia ya kuendea Timna. Maana aliona ya kwamba Shela amekuwa mtu mzima, wala hakuozwa awe mkewe. Yuda alipomwona alimdhania kuwa ni kahaba, maana amejifunika uso. Akamgeukia kando ya njia, akasema, Niruhusu niingie kwako. Maana hakujua ya kuwa ni mkwewe. Akamwuliza, Utanipa nini, ukiingia kwangu? Akasema, Nitakuletea mwana-mbuzi wa kundini. Naye akamwuliza, Je! Utanipa rehani hata utakapomleta? Akasema, Nikupe rehani gani? Akamjibu, Pete yako ya muhuri, na kamba yake, na fimbo yako iliyo mkononi mwako. Basi akampa, akaingia kwake, naye akapata mimba. Akaondoka, akaenda zake, akavua utaji wake, na kuvaa mavazi ya ujane wake. Yuda akapeleka yule mwana-mbuzi kwa mkono wa rafiki yake Mwadulami, ili aipate rehani mkononi mwa huyo mwanamke lakini hakumkuta. Akauliza watu wa mahali pale, akisema, Yuko wapi yule kahaba aliyekuwapo Enaimu kando ya njia? Wakasema, Hakuwako hapa kahaba. Akamrudia Yuda akasema, Sikumwona; hata na watu wa mahali hapo walisema, Hakuwako kahaba. Yuda akasema, Na aichukue yeye, tusije tukatiwa aibu; tazama, nimempelekea mbuzi huyu, wala hukumkuta. Ikawa baada ya miezi mitatu Yuda akapewa habari kwamba, Mkweo, Tamari, amefanya uzinifu, naye ana mimba ya haramu. Yuda akasema, Mtoeni ateketezwe. Alipotolewa, alipeleka watu kwa mkwewe, akisema, Mimi nimepewa mimba na mtu mwenye vitu hivi. Akasema, Tambua basi, vitu hivi ni vya nani, pete hii, na kamba hii, na fimbo hii. Yuda akavikiri, akasema, Yeye ni mwenye haki kuliko mimi, kwa kuwa sikumpa Shela, mwanangu. Wala hakumjua tena baada ya hayo. Ikawa, wakati wake wa kuzaa walikuwapo mapacha tumboni mwake. Ikawa alipokuwa akizaa, mtoto mmoja akatoa mkono, mzalisha akautwaa uzi mwekundu akaufunga mkononi mwake, huku akisema, Huyu ametoka kwanza. Ikawa aliporudisha mkono wake, tazama, ndugu yake akatoka. Akasema, Mbona umepita kwa nguvu wewe? Mambo ya nguvu na yakuandame. Kwa hiyo jina lake likaitwa Peresi. Akatoka ndugu yake baadaye, ana uzi mwekundu mkononi mwake; naye akaitwa jina lake Zera.
Mwanzo 38:12-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya muda mrefu mke wa Yuda binti wa Shua akafariki. Baada ya msiba, Yuda alikwenda Timna, kwa watu waliokuwa wakikata kondoo wake manyoya, naye alifuatana na rafiki yake Hira Mwadulami. Tamari alipoambiwa, “Baba mkwe wako yuko njiani kwenda Timna kukata kondoo wake manyoya,” alivua mavazi yake ya ujane, akajifunika kwa shela ili asifahamike, akaketi kwenye mlango wa Enaimu, ambao upo njiani kuelekea Timna. Akafanya hivyo kwa sababu aliona kwamba, ingawa Shela amekua, lakini alikuwa hajakabidhiwa kwake kuwa mkewe. Yuda alipomwona alifikiri ni kahaba, kwa sababu alikuwa amefunika uso wake. Pasipo kutambua kwamba alikuwa mkwe wake, akamwendea kando ya njia na kumwambia, “Njoo sasa, nikutane na wewe kimwili.” Yule mkwewe akamuuliza, “Utanipa nini nikikutana nawe kimwili?” Akamwambia, “Nitakutumia mwana-mbuzi kutoka kundi langu.” Akamuuliza, “Utanipa kitu chochote kama amana mpaka utakapompeleka?” Akamuuliza, “Nikupe amana gani?” Akamjibu, “Pete yako na kamba yake pamoja na fimbo iliyo mkononi mwako.” Kwa hiyo akampa vitu hivyo kisha akakutana naye kimwili, naye akapata mimba yake. Tamari akaondoka, akavua shela yake akavaa tena nguo zake za ujane. Wakati ule ule, Yuda akamtuma rafiki yake Mwadulami apeleke yule mwana-mbuzi ili arudishiwe amana yake kutoka kwa yule mwanamke, lakini yule rafiki yake hakumkuta yule mwanamke. Akawauliza watu wanaoishi mahali pale, “Yuko wapi yule kahaba wa mahali pa kuabudia miungu aliyekuwa kando ya barabara hapa Enaimu?” Wakamjibu, “Hajawahi kuwepo mwanamke yeyote kahaba wa mahali pa kuabudia miungu hapa.” Kwa hiyo akamrudia Yuda na kumwambia, “Sikumpata. Zaidi ya hayo, watu wanaoishi mahali pale walisema ‘Hapakuwahi kuwepo mwanamke yeyote kahaba wa mahali pa kuabudia miungu hapa.’ ” Kisha Yuda akasema, “Mwache avichukue vitu hivyo, ama sivyo tutakuwa kichekesho. Hata hivyo, nilimpelekea mwana-mbuzi, lakini hukumkuta.” Baada ya miezi mitatu Yuda akaambiwa, “Tamari mkweo ana hatia ya kuwa kahaba, na matokeo yake ana mimba.” Yuda akasema, “Mtoeni nje na achomwe moto hadi afe!” Alipokuwa akitolewa nje, akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake kusema, “Nina mimba ya mtu mwenye vitu hivi.” Akaongeza kusema, “Angalia kama utatambua kwamba pete hii na kamba yake pamoja na fimbo hii ni vya nani.” Yuda akavitambua na kusema, “Yeye ana haki kuliko mimi, kwa kuwa sikumkabidhi kwa mwanangu Shela ili awe mkewe.” Tangu hapo hakukutana naye kimwili tena. Wakati ulipofika wa kujifungua, kukawa na wana mapacha tumboni mwake. Alipokuwa akijifungua, mmoja akatoa mkono wake nje, kwa hiyo mkunga akachukua uzi mwekundu na kuufunga mkononi mwa yule mtoto, akasema, “Huyu ametoka kwanza.” Lakini alipourudisha mkono wake ndugu yake akaanza kutoka, naye akasema, “Hivi ndivyo ulivyotoka kwa nguvu!” Akaitwa Peresi. Kisha ndugu yake, aliyekuwa na uzi mwekundu mkononi, akatoka, naye akaitwa Zera.