Mwanzo 33:4-11
Mwanzo 33:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Esau akaenda mbio kumlaki Yakobo, akamkumbatia na kumbusu shingoni, na wote wawili wakalia. Esau alipotazama na kuwaona wale kina mama na watoto, akauliza, “Ni kina nani hawa ulio nao?” Yakobo akamjibu, “Hawa ni watoto ambao Mungu, kwa neema yake, amenijalia mimi mtumishi wako.” Kisha wale wajakazi wakakaribia pamoja na watoto wao, wakainama kwa heshima. Hali kadhalika Lea akaja pamoja na watoto wake, akainama kwa heshima. Hatimaye, Raheli na Yosefu wakaja, wakainama kwa heshima. Ndipo Esau akauliza, “Nini maana ya kundi hili nililokutana nalo njiani?” Yakobo akamjibu, “Nilitumaini kupata fadhili kwako ee bwana wangu.” Lakini Esau akasema, “Nina mali ya kutosha ndugu yangu. Mali yako na iwe yako mwenyewe.” Yakobo akamwambia, “La! Kama kweli umekubali kunipokea, basi, nakusihi uipokee zawadi yangu. Hakika, kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa vile ulivyonipokea kwa wema mkubwa. Basi, nakuomba uikubali zawadi niliyokuletea, kwa sababu hata mimi pia Mungu amenineemesha, nami ninayo mali nyingi.” Ndivyo Yakobo alivyomshawishi Esau, naye akaipokea zawadi yake.
Mwanzo 33:4-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia. Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake. Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama. Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama. Akasema, Kundi hili lote nililokutana nalo, maana yake ni nini? Akasema, Ili kunipatia kibali machoni pa bwana wangu. Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, hifadhi uliyo nayo yawe yako. Yakobo akasema, Sivyo; nakuomba kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, Hakika, kuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu – maana umenipokea kwa kibali kama chake. Tafadhali pokea zawadi yangu iliyoletwa kwako, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote. Akamsihi sana, naye akapokea.
Mwanzo 33:4-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia. Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake. Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama. Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama. Akasema, Kundi hili lote nililolikuta, maana yake ni nini? Akasema, Kunipatia kibali machoni pa bwana wangu. Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo nayo na yawe yako. Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami. Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote Akamshurutisha, naye akapokea.
Mwanzo 33:4-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini Esau akamkimbilia Yakobo kumlaki na kumkumbatia, akamwangukia shingoni na kumbusu. Nao wakalia. Esau akainua macho akawaona wale wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa uliofuatana nao ni nani?” Yakobo akamjibu, “Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.” Kisha wale watumishi wa kike na watoto wao wakakaribia na kusujudu. Kisha Lea na watoto wake wakaja na kusujudu. Mwisho wa wote wakaja Yosefu na Raheli, nao pia wakasujudu. Esau akauliza, “Una maana gani kuhusu makundi hayo yote niliyokutana nayo?” Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.” Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.” Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako, ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa takabali kubwa. Tafadhali ukubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.