Mwanzo 32:1-12
Mwanzo 32:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye. Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu. Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu. Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng’ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako. Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye. Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliopo pamoja naye, na kondoo, na ng’ombe, na ngamia, wawe matuo mawili. Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka. Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, BWANA, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema; mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili. Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana. Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi.
Mwanzo 32:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Yakobo aliendelea na safari yake. Basi, malaika wa Mungu wakakutana naye. Yakobo alipowaona, akasema, “Hili ni jeshi la Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali hapo Mahanaimu. Yakobo aliwatuma wajumbe wamtangulie kwenda kwa nduguye Esau, huko Seiri, katika nchi ya Edomu. Aliwapa maagizo haya, “Mtamwambia bwana wangu Esau hivi: Mtumishi wako Yakobo asema hivi, ‘Nimekaa ugenini kwa Labani mpaka sasa. Nina ng'ombe, punda, makundi ya kondoo na watumishi wa kiume na wa kike. Ninakutumia ujumbe huu, bwana wangu, ili nipate fadhili mbele yako.’” Hao wajumbe walikwenda, kisha wakarudi na kumwambia Yakobo, “Tumefika kwa ndugu yako Esau, naye yuko njiani kuja kukulaki, akiwa na watu 400.” Basi, Yakobo akaogopa sana na kufadhaika. Akawagawa katika makundi mawili watu waliokuwa pamoja naye, kondoo, mifugo mingine na ngamia, akifikiri, “Kama Esau akija na kuliangamiza kundi moja, basi, kundi litakalosalia litaponyoka.” Kisha Yakobo akamwomba Mungu akisema, “Ee Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaka! Ewe Mwenyezi-Mungu uliyeniambia nirudi katika nchi yangu kwa jamaa yangu, ukaniahidi kunitendea mema, sistahili hata kidogo fadhili ulizonipa kwa uaminifu mimi mtumishi wako. Nilipovuka mto Yordani, sikuwa na kitu ila fimbo; lakini sasa ninayo makundi haya mawili. Nakuomba uniokoe sasa kutoka kwa ndugu yangu Esau, maana nina hofu kuwa atatushambulia na kutuua sote, akina mama pamoja na watoto. Wewe uliniahidi kunitendea mema na kuwafanya wazawa wangu wawe wengi kama mchanga wa bahari ambao hauhesabiki kwa wingi wake.”
Mwanzo 32:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye. Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu. Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu. Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng'ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako. Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye. Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliokuwa pamoja naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe makundi mawili. Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka. Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, na Mungu wa baba yangu Isaka, BWANA, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema; mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nilivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa makundi mawili. Uniokoe sasa kutoka kwa mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi ninamwogopa, asije akaniua, na kina mama pamoja na watoto. Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi.
Mwanzo 32:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yakobo pia akaondoka akaenda zake, nao malaika wa Mungu wakakutana naye. Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu. Yakobo akatuma wajumbe kumtangulia kwa Esau ndugu yake huko Seiri, katika nchi ya Edomu. Akawaagiza akisema: “Hili ndilo mtakalomwambia bwana wangu Esau: ‘Mtumishi wako Yakobo anasema, nimekuwa nikiishi pamoja na Labani na nimekuwako huko mpaka sasa. Ninao ngʼombe na punda, kondoo na mbuzi, watumishi wa kiume na wa kike. Sasa ninatuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili nipate kibali machoni pako.’ ” Wajumbe waliporudi kwa Yakobo, wakamwambia, “Tulikwenda kuonana na ndugu yako Esau, naye sasa anakuja kukulaki akifuatana na wanaume 400.” Kwa hofu kuu na huzuni, Yakobo akagawanya watu aliokuwa nao katika makundi mawili, pia akagawanya makundi ya kondoo na mbuzi, na vilevile ngʼombe na ngamia. Yakobo alifikiri, “Kama Esau akija na kushambulia kundi moja, kundi lililobaki litaweza likanusurika.” Ndipo Yakobo akaomba, “Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaki, Ee BWANA, ambaye uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi,’ mimi sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa ninayo makundi mawili. Nakuomba, uniokoe na mkono wa ndugu yangu Esau, kwa maana ninaogopa kuwa atakuja kunishambulia, pia mama pamoja na watoto wao. Lakini umeshasema, ‘Hakika nitakufanya ustawi na kuufanya uzao wako kuwa mwingi kama mchanga wa baharini ambao hauwezi kuhesabika!’ ”