Mwanzo 30:1-13
Mwanzo 30:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Raheli alipoona ya kuwa hamzalii Yakobo mwana, Raheli alimwonea ndugu yake wivu. Akamwambia Yakobo, Nipe wana; kama sivyo, nitakufa mimi. Yakobo akamghadhibikia Raheli, akasema, Je! Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia uzao wa mimba? Akasema, Yuko mjakazi wangu, Bilha, uingie kwake ili kwamba azae juu ya magoti yangu, nami nipate uzao kwa yeye. Basi akampa Bilha mjakazi wake kuwa mkewe. Yakobo akaingia kwake. Naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. Raheli akasema, Mungu amenipa haki yangu, naye amesikia sauti yangu, akanipa mwana. Kwa hiyo akamwita jina lake Dani. Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Raheli akasema, Kwa mashindano makuu nimeshindana na ndugu yangu, nikashinda. Akamwita jina lake Naftali. Lea alipoona ya kuwa ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, akampa Yakobo kuwa mkewe. Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana. Lea akasema, Bahati njema! Akamwita jina lake Gadi. Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Lea akasema, Ni heri mimi, maana wanawake wataniita heri. Akamwita jina lake Asheri.
Mwanzo 30:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Raheli alipoona kwamba hajamzalia Yakobo watoto, alimwonea wivu Lea, dada yake, akamwambia Yakobo, “Nipatie watoto, la sivyo, nitakufa.” Yakobo akamkasirikia Raheli sana na kumwambia, “Je, mimi nimekuwa badala ya Mungu aliyekuzuia kupata watoto?” Raheli akamjibu, “Mjakazi wangu Bilha yupo. Lala naye ili azae watoto badala yangu, nami pia nipate watoto kutokana naye.” Kwa hiyo Raheli akampa Yakobo mtumishi wake, Bilha, awe mkewe, naye akalala naye. Bilha akapata mimba na kumzalia Yakobo mtoto wa kiume. Raheli akasema, “Mungu amenitendea sawa, amekisikia kilio changu na kunipa mtoto wa kiume.” Akamwita mtoto huyo Dani. Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume. Hapo Raheli akasema, “Nimepigana miereka mikali na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Naftali. Lea alipoona ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, na kumpa Yakobo ili awe mkewe. Zilpa akamzalia Yakobo mtoto wa kiume. Lea akasema, “Bahati njema.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Gadi. Zilpa, mtumishi wa Lea, alimzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume. Lea akasema, “Bahati njema! Sasa wanawake wataniita heri.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Asheri.
Mwanzo 30:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Raheli alipoona ya kuwa hamzalii Yakobo mwana, Raheli alimwonea dada yake wivu. Akamwambia Yakobo, Nipe wana; kama sivyo, nitakufa mimi. Yakobo akamghadhibikia Raheli, akasema, Je! Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia uzao wa mimba? Akasema, Yuko mjakazi wangu, Bilha, uingie kwake ili kwamba azae kwa niaba yangu, nami nipate uzao kwa yeye. Basi akampa Bilha mjakazi wake kuwa mkewe. Yakobo akaingia kwake. Naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. Raheli akasema, Mungu amenipa haki yangu, naye amesikia sauti yangu, akanipa mwana. Kwa hiyo akamwita jina lake Dani. Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Raheli akasema, Kwa mashindano makuu nimeshindana na dada yangu, nikashinda. Akamwita jina lake Naftali. Lea alipoona ya kuwa ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, akampa Yakobo kuwa mkewe. Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana. Lea akasema, Bahati njema! Akamwita jina lake Gadi. Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Lea akasema, Ni heri mimi, maana wanawake wataniita heri. Akamwita jina lake Asheri.
Mwanzo 30:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea ndugu yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!” Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia usizae watoto?” Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mtumishi wangu wa kike. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto na kwa kupitia yeye mimi pia niweze kuwa na uzao.” Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili, Bilha akapata mimba, naye akamzalia Yakobo mwana. Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu, amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa sababu hiyo akamwita Dani. Bilha mtumishi wa kike wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na ndugu yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita Naftali. Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mtumishi wake wa kike Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake. Mtumishi wa Lea yaani Zilpa, akamzalia Yakobo mwana. Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita Gadi. Mtumishi wa kike wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili. Ndipo Lea aliposema, “Jinsi gani nilivyo na furaha! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita Asheri.