Mwanzo 3:8-13
Mwanzo 3:8-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Jioni, wakati wa kupunga upepo, huyo mwanamume na mkewe wakasikia hatua za Mwenyezi-Mungu akitembea bustanini, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, “Uko wapi?” Naye akamjibu, “Nimesikia hatua zako bustanini, nikaogopa na kujificha, maana nilikuwa uchi.” Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?” Huyo mwanamume akajibu, “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza huyo mwanamke, “Umefanya nini wewe?” Mwanamke akamjibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”
Mwanzo 3:8-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone. BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nilisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.
Mwanzo 3:8-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone. BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.
Mwanzo 3:8-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo yule mwanaume na mkewe, waliposikia sauti ya BWANA Mungu alipokuwa akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka mbele za BWANA Mungu katikati ya miti ya bustani. Lakini BWANA Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?” Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.” Mungu akamuuliza, “Ni nani aliyekuambia ya kuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?” Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa sehemu ya tunda kutoka kwenye huo mti, nami nikala.” Ndipo BWANA Mungu akamuuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”