Mwanzo 28:1-9
Mwanzo 28:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Hivyo Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akisema, “Usioe mwanamke yeyote Mkanaani. Nenda Padan-aramu, nyumbani kwa babu yako Bethueli, ukaoe mmojawapo wa binti za mjomba wako Labani. Mungu mwenye nguvu na akubariki upate wazawa wengi na kuongezeka, ili uwe jamii kubwa ya watu. Akubariki wewe pamoja na wazawa wako kama alivyombariki Abrahamu, upate kuimiliki nchi ambamo unakaa kama mgeni; nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu!” Basi, Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mwaramu, kaka yake Rebeka, mama yao Yakobo na Esau. Esau alitambua kwamba Isaka alikuwa amembariki Yakobo na kumtuma aende kuoa huko Padan-aramu, na ya kuwa alipombariki, alimkataza asioe mwanamke Mkanaani. Alitambua pia kuwa Yakobo alimtii mama yake na baba yake, akaenda Padan-aramu. Basi, Esau akafahamu kwamba baba yake hapendezwi na wanawake wa Kanaani. Hivyo, mbali na wale wake zake wengine, Esau akaenda kwa Ishmaeli, mwana wa Abrahamu, akamwoa Mahalathi binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi.
Mwanzo 28:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani. Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako. Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mtu wa watu wengi. Akupe baraka ya Abrahamu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Abrahamu. Basi Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mshami, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau. Esau akaona ya kwamba Isaka amembariki Yakobo na kumtuma Padan-aramu, ili ajitwalie mke huko, na katika kumbariki akamwagiza, akasema, Usioe mke wa binti za Kanaani, na ya kuwa Yakobo amewatii babaye na mamaye, akaenda Padan-aramu. Esau akaona ya kuwa binti za Kanaani hawakumpendeza Isaka, baba yake. Basi Esau akaenda kwa Ishmaeli akamtwaa Mahalathi, binti Ishmaeli mwana wa Abrahamu, ndugu wa Nebayothi, kuwa mkewe pamoja na wakeze aliokuwa nao.
Mwanzo 28:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani. Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako. Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mkutano wa makabila. Akupe mbaraka wa Ibrahimu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Ibrahimu. Basi Isaka akampeleka Yakobo, naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mshami, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau. Esau akaona ya kwamba Isaka amembariki Yakobo na kumpeleka Padan-aramu, ili ajitwalie mke huko, na katika kumbariki akamwagiza, akasema, Usitwae mke wa binti za Kanaani, na ya kuwa Yakobo amewatii babaye na mamaye, akaenda Padan-aramu. Esau akaona ya kuwa binti za Kanaani hawakumpendeza Isaka, baba yake. Basi Esau akaenda kwa Ishmaeli akamtwaa Mahalathi, binti Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, ndugu wa Nebayothi, kuwa mkewe pamoja na wakeze aliokuwa nao.
Mwanzo 28:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi Isaki akamwita Yakobo, akambariki na akamwamuru, akisema, “Usioe mwanamke wa Kikanaani. Nenda mara moja mpaka Padan-Aramu, kwenye nyumba ya Bethueli baba wa mama yako. Uchukue mke kati ya binti za Labani ambaye ni ndugu wa mama yako. Mungu Mwenyezi na akubariki uwe na uzao uongezeke idadi yako upate kuwa jamii kubwa ya watu. Na akupe wewe na uzao wako baraka aliyopewa Abrahamu, upate kumiliki nchi unayoishi sasa kama mgeni, nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu.” Kisha Isaki akamuaga Yakobo, naye akaenda Padan-Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, ndugu wa Rebeka, aliyekuwa mama wa Yakobo na Esau. Sasa Esau akajua kuwa Isaki amembariki Yakobo na kumtuma kwenda Padan-Aramu ili achukue mke huko na kwamba alipombariki alimwamuru akisema, “Usioe mke katika binti za Wakanaani,” tena kwamba Yakobo amewatii baba yake na mama yake naye amekwenda Padan-Aramu. Esau akatambua jinsi ambavyo baba yake Isaki anavyowachukia binti za Wakanaani. Ndipo Esau akaenda kwa Ishmaeli, akamwoa Mahalati, ndugu wa Nebayothi na binti wa Ishmaeli mwana wa Abrahamu, kuongezea wale wake wengine aliokuwa nao.