Mwanzo 28:1-5
Mwanzo 28:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Hivyo Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akisema, “Usioe mwanamke yeyote Mkanaani. Nenda Padan-aramu, nyumbani kwa babu yako Bethueli, ukaoe mmojawapo wa binti za mjomba wako Labani. Mungu mwenye nguvu na akubariki upate wazawa wengi na kuongezeka, ili uwe jamii kubwa ya watu. Akubariki wewe pamoja na wazawa wako kama alivyombariki Abrahamu, upate kuimiliki nchi ambamo unakaa kama mgeni; nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu!” Basi, Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mwaramu, kaka yake Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.
Mwanzo 28:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani. Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako. Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mtu wa watu wengi. Akupe baraka ya Abrahamu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Abrahamu. Basi Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mshami, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.
Mwanzo 28:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani. Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako. Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mkutano wa makabila. Akupe mbaraka wa Ibrahimu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Ibrahimu. Basi Isaka akampeleka Yakobo, naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mshami, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.
Mwanzo 28:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi Isaki akamwita Yakobo, akambariki na akamwamuru, akisema, “Usioe mwanamke wa Kikanaani. Nenda mara moja mpaka Padan-Aramu, kwenye nyumba ya Bethueli baba wa mama yako. Uchukue mke kati ya binti za Labani ambaye ni ndugu wa mama yako. Mungu Mwenyezi na akubariki uwe na uzao uongezeke idadi yako upate kuwa jamii kubwa ya watu. Na akupe wewe na uzao wako baraka aliyopewa Abrahamu, upate kumiliki nchi unayoishi sasa kama mgeni, nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu.” Kisha Isaki akamuaga Yakobo, naye akaenda Padan-Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, ndugu wa Rebeka, aliyekuwa mama wa Yakobo na Esau.