Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 23:1-20

Mwanzo 23:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Sara aliishi miaka 127. Hiyo ndiyo iliyokuwa miaka ya maisha yake Sara. Alifia huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Abrahamu akaomboleza na kumfanyia matanga Sara mkewe. Abrahamu akaiacha maiti ya mkewe, akatoka kwenda kuzungumza na Wahiti, akawaambia, “Mimi ninaishi kama mgeni miongoni mwenu. Nipatieni sehemu ya ardhi ya kaburi, ili nipate kumzika marehemu mke wangu.” Wahiti wakamjibu, “Ee bwana wetu, tusikilize; wewe ni kiongozi maarufu miongoni mwetu. Mzike marehemu mkeo katika kaburi lolote utakalojichagulia; hakuna yeyote miongoni mwetu atakayekunyima kaburi lake, wala kukuzuia kumzika marehemu mkeo.” Hapo Abrahamu akasimama na kuinama kwa heshima mbele ya wananchi Wahiti, akawaambia, “Ikiwa mnaniruhusu nimzike marehemu mke wangu, tafadhali mwombeni Efroni mwana wa Sohari, kwa niaba yangu, aniuzie lile pango lake la Makpela lililo mpakani mwa shamba lake. Msihini aniuzie nilifanye makaburi yangu; anipatie kwa bei ya haki papa hapa mbele yenu.” Efroni mwenyewe alikuwa miongoni mwa Wahiti hao waliokuwa wamekutanika penye lango la mji. Basi, Efroni Mhiti, akamjibu Abrahamu, mbele ya Wahiti wote hapo langoni, “La, bwana; tafadhali unisikilize. Ninakupa shamba lote na pango lililomo humo; tena ninakupa mbele ya wananchi wenzangu. Mzike humo marehemu mkeo.” Abrahamu akainama tena kwa heshima mbele ya wananchi, akamwambia Efroni, wananchi wote wakisikia, “Nakuomba, tafadhali unisikilize. Nitakulipa bei kamili ya shamba lako, na ninakuomba upokee malipo haya, ili nipate kumzika humo marehemu mke wangu.” Efroni akamjibu Abrahamu, “Bwana, nisikilize; shamba lenye thamani ya shekeli 400 tu za fedha ni nini kati yako na mimi? Mzike marehemu mke wako.” Abrahamu akakubaliana na Efroni, akampimia kiasi cha fedha alichotaja mbele ya Wahiti wote, fedha shekeli 400, kadiri ya vipimo vya wafanyabiashara wa wakati huo. Basi, shamba la Efroni lililoko huko Makpela, mashariki ya Mamre, pango na miti yote iliyokuwamo pamoja na eneo zima, likawa lake Abrahamu mbele ya Wahiti wote waliokutanika penye lango la mji. Baada ya hayo, Abrahamu akamzika Sara mkewe katika pango hilo lililokuwamo katika shamba la Makpela, mashariki ya Mamre (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani. Shamba na pango lililokuwamo humo lilithibitishwa na Wahiti liwe mali yake Abrahamu apate kuzika humo wafu wake.

Shirikisha
Soma Mwanzo 23

Mwanzo 23:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi umri wake Sara ulikuwa miaka mia moja na ishirini na saba, ndio umri wake Sara. Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Abrahamu akamlilia na kumwombolezea Sara. Akaondoka Abrahamu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na wazawa wa Hethi, akinena, Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu. Wazawa wa Hethi wakamjibu Abrahamu, wakamwambia, Utusikie, Ee bwana, ndiwe mtu mkuu sana kwetu, uzike maiti wako katika kaburi lile utakalochagua katika makaburi yetu. Hapana mtu kwetu atakayekuzuilia kaburi lake, usizike maiti wako. Abrahamu akaondoka, akainama mbele ya watu wa nchi, mbele ya hao wazawa wa Hethi. Naye akazungumza nao, akisema, Ikiwa nia yenu nimzike maiti wangu atoke mbele yangu, mnisikie, mkaniombee kwa Efroni mwana wa Sohari, ili kwamba anipe pango la Makpela, iliyo katika mpaka wa shamba lake, na anipe kwa kima kilicho kamili, katikati yenu, iwe milki yangu ya kuzikia. Basi Efroni alikuwa akiketi kati ya wazawa wa Hethi. Efroni Mhiti akamjibu Abrahamu, na wazawa wa Hethi wanasikiliza, hata watu wote waingiao mlango wa mji wake, akisema, Sivyo, bwana wangu, unisikilize. Lile shamba nakupa, na pango lililomo nakupa; mbele ya wana wa watu wangu nakupa, uzike maiti wako. Abrahamu akainama mbele ya watu wa nchi. Akamwambia Efroni, na watu wa nchi wanasikiliza, akisema, Tafadhali unisikilize; nitatoa kima cha shamba, nawe ukipokee kwangu, nami nitamzika humo maiti wangu. Efroni akamjibu Abrahamu, akamwambia, Bwana wangu, unisikilize. Sehemu ya nchi, ambayo thamani yake ni shekeli za fedha mia nne, ni nini hii baina yako na yangu? Basi uzike maiti wako. Abrahamu akakubali maneno ya Efroni. Abrahamu akampimia Efroni ile fedha aliyotaja masikioni mwa wazawa wa Hethi, shekeli za fedha mia nne za namna inayotumika na wenye biashara. Basi shamba la Efroni lililokuwa katika Makpela kuelekea Mamre, shamba, na pango lililokuwemo, na miti yote iliyokuwamo shambani, iliyokuwa katika mipaka yake pande zote, vyote viliyakinishwa kuwa mali yake Abrahamu, mbele ya wazawa wa Hethi, mbele ya watu wote waingiao katika mlango wa mji wake. Basi baada ya hayo Abrahamu akamzika Sara mkewe katika pango la shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Na lile shamba, na pango lililomo, iliyakinishwa kuwa mali yake Abrahamu na wazawa wa Hethi, kuwa mahali pa kuzikia.

Shirikisha
Soma Mwanzo 23

Mwanzo 23:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi umri wake Sara ulikuwa miaka mia na ishirini na saba ndio umri wake Sara. Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia Sara na kumwombolezea. Akaondoka Ibrahimu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na wazawa wa Hethi, akinena, Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu. Wazawa wa Hethi wakamjibu Ibrahimu, wakamwambia, Utusikie, Ee bwana, ndiwe mtu mkuu sana kwetu, uzike maiti wako katika kaburi lile utakalochagua katika makaburi yetu. Hapana mtu kwetu atakayekuzuilia kaburi lake, usizike maiti wako. Ibrahimu akaondoka, akainama mbele ya watu wa nchi, mbele ya hao wazawa wa Hethi. Naye akazungumza nao, akisema, Ikiwa nia yenu nimzike maiti wangu atoke mbele yangu, mnisikie, mkaniombee kwa Efroni bin Sohari, ili kwamba anipe pango ya Makpela, iliyo katika mpaka wa shamba lake, na anipe kwa kima kilicho kamili, katikati yenu, iwe milki yangu ya kuzikia. Basi Efroni alikuwa akiketi kati ya wazawa wa Hethi. Efroni Mhiti akamjibu Ibrahimu, na wazawa wa Hethi wanasikiliza, hata watu wote waingiao mlango wa mji wake, akisema, Sivyo, bwana wangu, unisikilize. Lile shamba nakupa, na pango iliyomo nakupa; mbele ya wana wa watu wangu nakupa, uzike maiti wako. Ibrahimu akainama mbele ya watu wa nchi. Akamwambia Efroni, na watu wa nchi wanasikiliza, akisema, Tafadhali unisikilize; nitatoa kima cha shamba, nawe ukipokee kwangu, nami nitamzika humo maiti wangu. Efroni akamjibu Ibrahimu, akamwambia, Bwana wangu, unisikilize. Sehemu ya nchi, ambayo thamani yake ni shekeli za fedha mia nne, n’nini hii baina yako na yangu? Basi uzike maiti wako. Ibrahimu akakubali maneno ya Efroni. Ibrahimu akampimia Efroni ile fedha aliyotaja masikioni mwa wazawa wa Hethi, shekeli za fedha mia nne za namna inayotumika na wenye biashara. Basi shamba la Efroni lililokuwa katika Makpela kuelekea Mamre, shamba, na pango iliyokuwamo, na miti yote iliyokuwamo shambani, iliyokuwa katika mipaka yake pande zote, vyote viliyakinishwa kuwa mali yake Ibrahimu, mbele ya wazawa wa Hethi, mbele ya watu wote waingiao katika mlango wa mji wake. Basi baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe katika pango ya shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Na lile shamba, na pango iliyomo, iliyakinishwa kuwa mali yake Ibrahimu na wazawa wa Hethi, kuwa mahali pa kuzikia.

Shirikisha
Soma Mwanzo 23

Mwanzo 23:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Sara aliishi akawa na umri wa miaka mia na ishirini na saba. Sara akafa huko Kiriath-Arba (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani, Abrahamu akamwombolezea na kumlilia Sara. Ndipo Abrahamu akainuka kutoka pale penye maiti ya mke wake. Akazungumza na Wahiti, akasema, “Mimi ni mpitaji na mgeni miongoni mwenu. Niuzieni sehemu ya ardhi yenu ili niweze kumzika maiti wangu.” Wahiti wakamjibu Abrahamu, “Bwana, tusikilize. Wewe ni mtawala mkuu sana miongoni mwetu. Zika maiti wako katika kaburi unalolipenda kati ya makaburi yetu. Hakuna mtu wa kwetu atakayekuzuia kaburi lake ili kuzika maiti wako.” Abrahamu akainuka na akasujudu mbele ya wenyeji wa nchi, yaani Wahiti. Akawaambia, “Kama mnaniruhusu kumzika maiti wangu, basi nisikilizeni mkamsihi Efroni mwana wa Sohari kwa niaba yangu ili aniuzie pango la Makpela, lililo mali yake, nalo liko mwisho wa shamba lake. Mwambieni aniuzie kwa bei kamili atakayosema ili liwe mahali pangu pa kuzikia miongoni mwenu.” Efroni Mhiti alikuwa ameketi miongoni mwa watu wake, akamjibu Abrahamu mbele ya Wahiti wote waliokuwepo katika lango la mji. “La hasha, bwana wangu, nisikilize, nakupa shamba, pia nakupa pango lililomo ndani yake. Nakupa mbele ya watu wangu. Uzike maiti wako.” Abrahamu akasujudu tena, mbele ya wenyeji wa nchi, akamwambia Efroni wale watu wakiwa wanasikia, “Tafadhali nisikilize. Nitakulipa fedha za hilo shamba. Kubali kuzipokea ili niweze kumzika maiti wangu.” Efroni akamjibu Abrahamu, “Nisikilize, bwana wangu, thamani ya ardhi hiyo ni shekeli 400 za fedha, lakini hiyo ni nini kati yako na mimi? Mzike maiti wako.” Abrahamu akakubali masharti ya Efroni, akampimia ile fedha aliyotaja masikioni mwa Wahiti: Shekeli 400 za fedha kulingana na viwango vya uzito vilivyokuwa vikitumika wakati huo na wafanyabiashara. Hivyo shamba la Efroni huko Makpela karibu na Mamre, yaani shamba pamoja na pango lililokuwamo, nayo miti yote iliyokuwamo ndani ya mipaka ya shamba hilo, vilikabidhiwa, kwa Abrahamu kuwa mali yake mbele ya Wahiti wote waliokuwa wamekuja kwenye lango la mji. Baada ya hayo Abrahamu akamzika Sara mkewe kwenye pango ndani ya shamba la Makpela karibu na Mamre (huko Hebroni) katika nchi ya Kanaani. Hivyo Wahiti wakamkabidhi Abrahamu shamba pamoja na pango lililokuwa humo kuwa mahali pa kuzikia.

Shirikisha
Soma Mwanzo 23