Mwanzo 21:1-13
Mwanzo 21:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimkumbuka Sara, akamtendea kama alivyoahidi. Basi, Abrahamu akiwa mzee, Sara akapata mimba, akamzalia mtoto wa kiume, wakati uleule Mungu alioutaja. Abrahamu akampa huyo mwanawe ambaye Sara alimzalia jina Isaka. Isaka alipotimiza umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri kama alivyoamriwa na Mungu. Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 100 wakati mwanawe Isaka alipozaliwa. Naye Sara akasema, “Mungu amenipatia kicheko; yeyote atakayesikia habari hizi, atacheka pamoja nami.” Kisha akaongeza, “Ni nani angeweza kumwambia Abrahamu kwamba mimi Sara nitanyonyesha watoto? Tena nimemzalia mtoto wa kiume katika uzee wake!” Isaka akaendelea kukua, na siku alipoachishwa kunyonya, Abrahamu akafanya sherehe kubwa. Baadaye Sara alimwona Ishmaeli, mtoto wa Abrahamu aliyezaliwa na Hagari, Mmisri, akicheza na Isaka mwanawe. Basi, Sara akamwambia Abrahamu, “Mfukuzie mbali mjakazi huyu na mwanawe. Haiwezekani kabisa mtoto wa mjakazi kurithi pamoja na mwanangu Isaka.” Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa kuwa Ishmaeli pia alikuwa mtoto wake. Lakini Mungu akamwambia Abrahamu, “Usihuzunike kwa sababu ya mtoto huyu, wala huyo mtumwa wako wa kike. Lolote akuambialo Sara lifanye; kwa kweli wazawa wako watatokana na Isaka. Na kuhusu huyo mwana wa mjakazi wako, nitamfanya awe baba wa taifa kubwa kwa kuwa yeye pia ni mtoto wako.”
Mwanzo 21:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Abrahamu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Abrahamu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Abrahamu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Abrahamu alikuwa mtu wa miaka mia moja, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, Ni nani angemwambia Abrahamu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Abrahamu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Abrahamu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Abrahamu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Abrahamu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Abrahamu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.
Mwanzo 21:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, N’nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.
Mwanzo 21:1-13 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Wakati huu Mwenyezi Mungu akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, na Mwenyezi Mungu akamtendea Sara kama alivyoahidi. Sara akapata mimba, na akamzalia Ibrahimu mwana katika uzee wake, katika majira yale Mungu alikuwa amemwahidi. Ibrahimu akampa huyo mwana ambaye Sara alimzalia jina Isaka. Isaka alipokuwa na umri wa siku nane, Ibrahimu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru. Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka mia moja Isaka mwanawe alipozaliwa. Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, na kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.” Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Ibrahimu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Lakini nimemzalia mwana katika uzee wake.” Mtoto akakua na akaachishwa kunyonya. Siku ile Isaka aliyoachishwa kunyonya, Ibrahimu alifanya sherehe kubwa. Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hajiri Mmisri alimzalia Ibrahimu alikuwa anadhihaki. Hivyo Sara akamwambia Ibrahimu, “Mwondoe mjakazi huyu mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mjakazi huyo kamwe hatarithi na mwanangu Isaka.” Jambo hili lilimhuzunisha sana Ibrahimu kwa sababu lilimhusu mwanawe. Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana huyo na mjakazi wako. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka. Nitamfanya huyu mwana wa mjakazi wako kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”