Mwanzo 19:30-38
Mwanzo 19:30-38 Biblia Habari Njema (BHN)
Loti aliogopa kuishi mjini Soari, kwa hiyo akauhama mji huo, yeye pamoja na binti zake wawili, wakaenda kuishi pangoni, milimani. Wakiwa huko, binti mkubwa akamwambia dada yake, “Baba yetu ni mzee, na hakuna mwanamume nchini wa kutuoa tupate watoto. Basi, tumlevye baba kwa divai, ili tupate kulala naye na kudumisha uzawa kwa kupata watoto kwake.” Usiku huo wakamlevya baba yao kwa divai, na yule binti wa kwanza akaenda akalala naye. Lakini baba yake hakujua wakati bintiye alipolala naye, wala alipoondoka. Kesho yake, yule binti wa kwanza akamwambia yule mdogo, “Jana usiku mimi nililala na baba; leo pia tumlevye kwa divai, kisha wewe utalala naye, na hivyo sote tutadumisha uzao kwa kupata watoto.” Basi, usiku huo pia wakamlevya baba yao kwa divai, kisha yule binti mdogo akaenda akalala naye. Lakini baba yake hakujua wakati bintiye alipolala naye, wala alipoondoka. Hivyo, binti wote wawili wa Loti wakapata mimba kutokana na baba yao. Yule binti wa kwanza akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Moabu. Huyo ndiye baba wa Wamoabu hadi leo. Yule mdogo pia akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Ben-ami. Huyo ndiye baba wa Waamoni hadi leo.
Mwanzo 19:30-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye na binti zake wawili. Yule mkubwa akamwambia mdogo, Baba yetu ni mzee, wala hakuna mwanamume katika nchi atuingilie kama ilivyo desturi ya dunia yote. Haya, na tumnyweshe baba yetu mvinyo, tukalale naye, ili tumhifadhie baba yetu uzao. Wakamnywesha baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka huyo mkubwa akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. Ikawa siku ya pili, mkubwa akamwambia mdogo, Tazama, nimelala jana na baba yangu, tumnyweshe mvinyo tena usiku huu, ukaingie ukalale naye ili tupate uzao kwa baba yetu. Wakamnywesha tena baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka mdogo akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. Basi hao binti wote wawili wa Lutu wakapata mimba kwa baba yao. Yule mkubwa akazaa mwana, akamwita jina lake Moabu; huyo ndiye baba wa Wamoabi, hata leo. Na yule mdogo naye akazaa mwana akamwita jina lake Benami; huyo ndiye baba wa Waamoni hata leo.
Mwanzo 19:30-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye na binti zake wawili. Yule mkubwa akamwambia mdogo, Baba yetu ni mzee, wala hakuna mtu mume katika nchi atuingilie kama ilivyo desturi ya dunia yote. Haya, na tumnyweshe baba yetu mvinyo, tukalale naye, ili tumhifadhie baba yetu uzao. Wakamnywesha baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka huyo mkubwa akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. Ikawa siku ya pili, mkubwa akamwambia mdogo, Tazama, nimelala jana na baba yangu, tumnyweshe mvinyo tena usiku huu, ukaingie ukalale naye. Wakamnywesha tena baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka mdogo akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. Basi hao binti wote wawili wa Lutu wakapata mimba kwa baba yao. Yule mkubwa akazaa mwana, akamwita jina lake Moabu; huyo ndiye baba wa Wamoabi, hata leo. Na yule mdogo naye akazaa mwana akamwita jina lake Benami; huyo ndiye baba wa Waamoni hata leo.
Mwanzo 19:30-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Loti na binti zake wawili waliondoka Soari na kufanya makao yao kule milimani, kwa maana aliogopa kukaa Soari. Yeye na binti zake wawili waliishi katika pango. Siku moja binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Baba yetu ni mzee na hakuna mwanaume mahali hapa atakayekutana na sisi kimwili, kama ilivyo desturi ya mahali pote duniani. Tumnyweshe baba yetu mvinyo kisha tukutane naye kimwili ili tuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.” Usiku ule walimnywesha baba yao mvinyo, alipolewa binti yake mkubwa akaingia na kukutana naye kimwili. Baba yao hakujua wakati binti yake alipoingia kulala naye wala alipotoka. Siku iliyofuata binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Usiku uliopita mimi nilikutana kimwili na baba yangu. Tumnyweshe divai tena, usiku huu nawe ukutane naye kimwili ili tuweze kuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.” Kwa hiyo wakamnywesha baba yao mvinyo tena usiku ule, naye binti yake mdogo akaingia, akakutana naye kimwili. Kwa mara nyingine baba yao hakujua binti yake alipolala naye wala alipoondoka. Hivyo binti wawili wa Loti wakapata mimba kwa baba yao. Binti mkubwa akamzaa mwana, akamwita jina lake Moabu; ndio baba wa Wamoabu hata leo. Binti mdogo naye pia akamzaa mwana, naye akamwita Benami; ndiye baba wa Waamoni hata leo.