Mwanzo 18:10-14
Mwanzo 18:10-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Mmoja wao akasema, “Hakika nitakurudia wakati kama huu mwakani, na mkeo Sara atakuwa na mtoto wa kiume.” Sara alikuwa huko nyuma mlangoni mwa hema, akisikiliza. Abrahamu na Sara walikuwa wakongwe, naye Sara mambo ya kawaida ya wanawake yalikuwa yamekoma kitambo. Kwa hiyo, Sara alicheka kimoyomoyo akisema, “Mimi ni mzee, na mume wangu hali kadhalika. Je, nikiwa mzee hivi, nitaweza kufurahi na kupata watoto?” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kujiuliza kama kweli itawezekana apate mtoto akiwa mzee? Je, kuna jambo lolote lisilowezekana kwa Mwenyezi-Mungu? Nitakurudia wakati uliopangwa, wakati kama huu mwakani, na Sara atakuwa na mtoto wa kiume.”
Mwanzo 18:10-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Abrahamu na Sara walikuwa wazee wenye umri mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? BWANA akamwambia Abrahamu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.
Mwanzo 18:10-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.
Mwanzo 18:10-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha BWANA akasema, “Hakika nitakurudia tena majira kama haya mwakani na Sara mkeo atakuwa ana mwana.” Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema, lililokuwa nyuma yake. Abrahamu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Hivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?” Ndipo BWANA akamwambia Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’ Je, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa BWANA? Nitakurudia mwakani majira kama haya, naye Sara atakuwa na mwana.”