Mwanzo 17:9-14
Mwanzo 17:9-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Mungu akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wako, wewe utalishika agano langu, wewe binafsi, wazawa wako na vizazi vyao vyote. Hili ndilo agano utakaloshika kati yangu na wewe na wazawa wako: Kila mwanamume miongoni mwenu lazima atahiriwe. Mtatahiriwa kwa kukata magovi yenu, na hii itakuwa ndiyo alama ya agano kati yangu nanyi. Kila mtoto wa kiume wa siku nane miongoni mwenu ni lazima atahiriwe. Kila mwanamume katika vizazi vyenu, awe mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwenu au aliyenunuliwa kwa fedha zenu kutoka kwa mgeni asiye mzawa wako; naam, kila mmoja wao aliyezaliwa katika nyumba yako na hata aliyenunuliwa kwa fedha zako ni lazima atahiriwe. Hiyo ni alama ya agano langu katika miili yenu, agano la milele. Mwanamume yeyote asiyetahiriwa atatengwa na watu, kwani atakuwa amevunja agano langu.”
Mwanzo 17:9-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mungu akamwambia Abrahamu, Nawe ulishike agano langu, wewe, uzao wako na vizazi vyao. Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati yangu nawe, na uzao wako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi. Katika vizazi vyako vyote, kila mtoto wa kiume miongoni mwenu atatahiriwa akiwa na umri wa siku nane, awe mtumishi aliyezaliwa katika nyumba yako au uliyemnunua kwa fedha zako japo hakuwa wa uzao wako. Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele. Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.
Mwanzo 17:9-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako. Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi. Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako. Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele. Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.
Mwanzo 17:9-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Mungu akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wako, lazima ushike Agano langu, wewe na wazao wako kwa ajili ya vizazi vijavyo. Hili ni Agano langu na wewe pamoja na wazao wako baada yako, Agano mtakalolishika: Kila mwanaume miongoni mwenu atatahiriwa. Mtafanyiwa tohara na hii itakuwa ni alama ya Agano kati yangu na ninyi. Kwa vizazi vijavyo, kila mwanaume miongoni mwenu mwenye siku nane ni lazima atahiriwe, pamoja na watakaozaliwa nyumbani mwako au walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, wale ambao sio watoto wako. Awe amezaliwa nyumbani mwako au amenunuliwa kwa fedha yako, ni lazima watahiriwe. Agano langu katika mwili wako litakuwa ni Agano la milele. Kila mwanaume asiyetahiriwa, ambaye hajapata tohara ya mwilini, atatengwa na watu wake, amelivunja Agano langu.”