Mwanzo 14:11-16
Mwanzo 14:11-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, wale walioshinda, wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora, kadhalika na mazao yao, wakaenda zao. Walimteka hata Loti, mwana wa nduguye Abramu aliyekuwa anakaa Sodoma, pamoja na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka, akaenda kumwarifu yule Mwebrania Abramu ambaye alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mwamori Mamre. Mamre alikuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri. Wote walikuwa wamefanya agano na Abramu. Abramu alipopata habari kwamba mpwa wake amechukuliwa mateka, akatoka na watu wake stadi 318 waliozaliwa katika nyumba yake, akawafuatia adui mpaka Dani. Huko, akaligawa jeshi lake katika makundi. Usiku, akawashambulia adui zake, akawashinda na kuwafukuza hadi Hoba, kaskazini mwa Damasko. Basi, Abramu akaikomboa mali yote iliyotekwa na adui, na kumkomboa Loti mpwa wake, mali yake, pamoja na wanawake na watu wengine.
Mwanzo 14:11-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; aliyekuwa akikaa karibu na mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu. Abramu aliposikia ya kwamba nduguye amechukuliwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.
Mwanzo 14:11-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu. Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.
Mwanzo 14:11-16 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Wale wafalme wanne wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora pamoja na vyakula vyao vyote, kisha wakaenda zao. Pia walimteka Lutu, mwana wa ndugu yake Abramu, pamoja na mali yake, kwa kuwa alikuwa akiishi Sodoma. Mtu mmoja aliyekuwa ametoroka akaja kumpa Abramu Mwebrania taarifa. Abramu alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mamre Mwamori, ndugu ya Eshkoli na Aneri, ambao wote walikuwa wameungana na Abramu. Abramu alipopata habari kwamba jamaa yake amechukuliwa mateka, akawaita watu mia tatu na kumi na nane (318) wa nyumbani mwake waliokuwa wamefunzwa kupigana vita, wakawafuatilia hadi Dani. Wakati wa usiku, Abramu aliwapanga watu wake katika vikosi, wakawashambulia na kuwashinda, wakawafukuza hadi Hoba, kaskazini mwa Dameski. Abramu akarudisha mali yote, na akamrudisha Lutu jamaa yake na mali yake, pamoja na wanawake na watu wengine.