Mwanzo 1:14-23
Mwanzo 1:14-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu akasema, “Mianga na iweko angani, itenge mchana na usiku, ioneshe nyakati, majira, siku na miaka, na ingae angani na kuiangazia dunia.” Ikawa hivyo. Basi, Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka mianga hiyo angani iiangazie dunia, ipate kutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akaona kuwa ni vyema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya nne. Mungu akasema, “Maji na yatoe makundi ya viumbe hai na ndege waruke angani.” Basi, Mungu akaumba wanyama wakubwa sana wa baharini na aina zote za viumbe vyote hai viendavyo na kujaa majini; akaumba na aina zote za ndege wote. Mungu akaona kuwa ni vyema. Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni, muongezeke, muyajaze maji ya bahari; nao ndege waongezeke katika nchi.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tano.
Mwanzo 1:14-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili ya kuonesha majira, siku na miaka; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo. Mungu akaumba mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne. Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na viumbe vyenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano.
Mwanzo 1:14-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne. Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano.
Mwanzo 1:14-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne. Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.