Wagalatia 5:1-15
Wagalatia 5:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika uhuru huo Kristo alituweka huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidi neno. Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote. Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutotahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo. Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi. Chachu kidogo huchachua donge zima. Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewasumbua atachukua hukumu yake, awaye yote. Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Kwa kufanya hivyo kikwazo cha msalaba kimeondolewa! Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao! Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako. Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana.
Wagalatia 5:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa. Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote. Nasema tena wazi: Kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika sheria yote. Kama mnatazamia kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu. Kwa upande wetu, lakini, sisi tunangojea kwa matumaini kwa nguvu ya Roho tufanywe waadilifu kwa njia ya imani. Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo. Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi, aliyewazuia kuuzingatia ukweli? Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni. “Chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!” Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba nyinyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni – awe nani au nani – hakika ataadhibiwa. Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote. Laiti hao wanaowavurugeni wangejihasi wenyewe! Nyinyi ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo. Maana sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe!
Wagalatia 5:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno. Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote. Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo. Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi. Chachu kidogo huchachua donge zima. Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewafadhaisha atachukua hukumu yake, awaye yote. Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Hapo kwazo la msalaba limebatilika! Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao! Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako. Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana.
Wagalatia 5:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa. Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia chochote. Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote. Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu. Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki. Kwa maana ndani ya Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo. Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Ushawishi wa namna hiyo haukutokana na yule anayewaita. “Chachu kidogo huchachua donge zima.” Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe! Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.