Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 3:6-29

Wagalatia 3:6-29 Biblia Habari Njema (BHN)

Chukueni kwa mfano habari za Abrahamu: Yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu. Sasa basi, jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu. Maandiko Matakatifu yalionesha kabla kwamba Mungu atawafanya watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia Abrahamu Habari Njema: “Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa.” Basi, wale walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini. Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na sheria, wako chini ya laana. Maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Yeyote asiyeshika na kutimiza yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria, yuko chini ya laana.” Ni dhahiri kwamba sheria haiwezi kumfanya mtu kuwa mwadilifu; maana Maandiko yasema: “Mwadilifu kwa imani ataishi.” Lakini sheria haitegemei imani, ila Maandiko yasema: “Mwenye kutimiza yanayotakiwa na sheria ataishi.” Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: “Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa.” Jambo hili lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu alituahidia. Ndugu, nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka kando au kuuongezea kitu. Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: “Na wazawa wake,” yaani wengi, bali yasema, “Na mzawa wake,” yaani mmoja, naye ndiye Kristo. Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake, akalithibitisha; sheria ambayo ilitokea miaka 430 baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi. Maana, kama zawadi ya Mungu inategemea sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi. Ya nini basi, sheria? Iliongezwa hapo ili kuonesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja. Je, sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uhai, basi, tungeweza kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria. Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi aliyotoa Mungu, kwa kumwamini Yesu Kristo. Kabla ya kujaliwa imani, sheria ilitufanya wafungwa, tukingojea imani hiyo ifunuliwe. Basi, hiyo sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani tufanywe waadilifu mbele yake Mungu. Lakini kwa vile ile imani imekwisha fika, sisi hatuko tena chini ya mlezi. Kwa njia ya imani, nyinyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu kwa kuungana na Kristo. Nyinyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja kwa kuungana na Kristo Yesu. Ikiwa nyinyi ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu.

Wagalatia 3:6-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kama vile Abrahamu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki. Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Abrahamu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiria Abrahamu Habari Njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Abrahamu aliyekuwa mwenye imani. Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Abrahamu iwafikie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani. Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno. Basi ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazawa, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo. Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi. Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa njia ya ahadi. Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hadi aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe. Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja. Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, hakika haki ingalipatikana kwa sheria. Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hakuna Myahudi wala Mgiriki. Hakuna mtumwa wala huru. Hakuna mwanamume wala mwanamke. Maana ninyi nyote mmekuwa wamoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Abrahamu, na warithi kulingana na ahadi.

Wagalatia 3:6-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki. Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani. Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani. Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno. Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo. Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi. Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi. Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe. Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja. Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria. Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.

Wagalatia 3:6-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu. Maandiko yakitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, alitangulia kumtangazia Abrahamu Injili akisema kwamba, “Kwa kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.” Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani. Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.” Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.” Lakini sheria haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.” Alitukomboa ili kwamba baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho. Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa wazao,” likimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako,” yaani mtu mmoja, ndiye Kristo. Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka 430 baadaye, haitangui Agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile. Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kwa njia ya ahadi. Kwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa mpaka atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja. Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria. Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini. Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria. Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.