Wagalatia 3:21-29
Wagalatia 3:21-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Je, sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uhai, basi, tungeweza kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria. Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi aliyotoa Mungu, kwa kumwamini Yesu Kristo. Kabla ya kujaliwa imani, sheria ilitufanya wafungwa, tukingojea imani hiyo ifunuliwe. Basi, hiyo sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani tufanywe waadilifu mbele yake Mungu. Lakini kwa vile ile imani imekwisha fika, sisi hatuko tena chini ya mlezi. Kwa njia ya imani, nyinyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu kwa kuungana na Kristo. Nyinyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja kwa kuungana na Kristo Yesu. Ikiwa nyinyi ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu.
Wagalatia 3:21-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, hakika haki ingalipatikana kwa sheria. Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hakuna Myahudi wala Mgiriki. Hakuna mtumwa wala huru. Hakuna mwanamume wala mwanamke. Maana ninyi nyote mmekuwa wamoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Abrahamu, na warithi kulingana na ahadi.
Wagalatia 3:21-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria. Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.
Wagalatia 3:21-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria. Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini. Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria. Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.