Wagalatia 3:19-22
Wagalatia 3:19-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Ya nini basi, sheria? Iliongezwa hapo ili kuonesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja. Je, sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uhai, basi, tungeweza kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria. Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi aliyotoa Mungu, kwa kumwamini Yesu Kristo.
Wagalatia 3:19-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hadi aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe. Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja. Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, hakika haki ingalipatikana kwa sheria. Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo.
Wagalatia 3:19-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe. Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja. Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria. Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo.
Wagalatia 3:19-22 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kwa nini basi iwepo Torati? Torati iliwekwa kwa sababu ya makosa hadi atakapokuja yule Mzao wa Ibrahimu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Torati iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja. Je basi, Torati inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama Torati iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kupitia kwa Torati. Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kupitia kwa imani katika Isa Al-Masihi yapate kupewa wale wanaoamini.