Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 3:1-14

Wagalatia 3:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Enyi Wagalatia, mmekuwa wajinga kweli! Ni nani aliyewaroga? Habari juu ya kusulubiwa kwake Yesu Kristo ilielezwa waziwazi mbele ya macho yenu. Napenda kujua tu kitu kimoja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa sababu ya kutimiza matakwa ya sheria ama kwa sababu ya kuisikia na kuiamini Injili? Je, nyinyi ni wajinga kiasi hicho? Nyinyi mlianza yote kwa msaada wa Roho, je, mnataka sasa kumaliza kwa nguvu zenu wenyewe? Je, mambo yale yote yaliyowapata nyinyi yamekuwa bure tu? Haiwezekani! Je, Mungu huwajalia Roho na kutenda miujiza kati yenu ati kwa sababu mnatimiza yanayotakiwa na sheria, ama kwa sababu mnasikia Injili na kuiamini? Chukueni kwa mfano habari za Abrahamu: Yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu. Sasa basi, jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu. Maandiko Matakatifu yalionesha kabla kwamba Mungu atawafanya watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia Abrahamu Habari Njema: “Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa.” Basi, wale walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini. Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na sheria, wako chini ya laana. Maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Yeyote asiyeshika na kutimiza yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria, yuko chini ya laana.” Ni dhahiri kwamba sheria haiwezi kumfanya mtu kuwa mwadilifu; maana Maandiko yasema: “Mwadilifu kwa imani ataishi.” Lakini sheria haitegemei imani, ila Maandiko yasema: “Mwenye kutimiza yanayotakiwa na sheria ataishi.” Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: “Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa.” Jambo hili lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu alituahidia.

Wagalatia 3:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulubiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili? Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli. Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Kama vile Abrahamu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki. Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Abrahamu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiria Abrahamu Habari Njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Abrahamu aliyekuwa mwenye imani. Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Abrahamu iwafikie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.

Wagalatia 3:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili? Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli. Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki. Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani. Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.

Wagalatia 3:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa. Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia? Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu. Maandiko yakitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, alitangulia kumtangazia Abrahamu Injili akisema kwamba, “Kwa kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.” Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani. Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.” Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.” Lakini sheria haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.” Alitukomboa ili kwamba baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.