Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 1:1-24

Wagalatia 1:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Mimi Paulo niliye mtume si kwa mamlaka ya binadamu, wala si kwa nguvu ya mtu, bali kwa uwezo wa Yesu Kristo na wa Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu, na ndugu wote walio pamoja nami tunayasalimu makanisa ya Galatia. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. Kristo alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na mapenzi ya Mungu wetu na Baba, ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu mbaya wa sasa. Kwake yeye uwe utukufu milele na milele! Amina. Nashangaa kwamba muda mfupi tu umepita, nanyi mnamwasi Mungu aliyewaita kwa neema ya Kristo, na mnafuata injili ya namna nyingine. Lakini hakuna injili nyingine. Ukweli ni kwamba wako watu wanaowavurugeni, watu wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. Lakini, hata kama mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni, atawahubirieni injili tofauti na ile tuliyowahubirieni sisi, basi huyo na alaaniwe! Tulikwisha sema, na sasa nasema tena: Kama mtu yeyote anawahubirieni injili ya aina nyingine, tofauti na ile mliyokwisha pokea, huyo na alaaniwe! Sasa nataka kibali cha nani: Cha binadamu, ama cha Mungu? Au je, nataka kuwapendeza watu? Kama ningefanya hivyo, mimi singekuwa kamwe mtumishi wa Kristo. Ndugu, napenda mfahamu kwamba ile Injili niliyoihubiri si ujumbe wa kibinadamu. Wala mimi sikuipokea kutoka kwa binadamu, wala sikufundishwa na mtu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia. Bila shaka mlikwisha sikia jinsi nilivyokuwa ninaishi zamani kwa kuzingatia dini ya Kiyahudi, na jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kupita kiasi na kutaka kuliharibu kabisa. Naam, mimi niliwashinda wengi wa wananchi wenzangu wa rika langu katika kuizingatia dini ya Kiyahudi, nikajitahidi sana kuyashika mapokeo ya wazee wetu. Lakini Mungu, kwa neema yake, alikuwa ameniteua hata kabla sijazaliwa, akaniita nimtumikie. Mara tu alipoamua kunifunulia Mwanawe kusudi niihubiri Habari Njema yake kwa watu wa mataifa mengine, bila kutafuta maoni ya binadamu, na bila kwenda kwanza Yerusalemu kwa wale waliopata kuwa mitume kabla yangu, nilikwenda kwanza Arabia, kisha nikarudi tena Damasko. Ilikuwa tu baada ya miaka mitatu, ndipo nilipokwenda Yerusalemu kuonana na Kefa; nilikaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. Haya ninayowaandikieni, Mungu anajua; sisemi uongo. Baadaye nilikwenda katika tarafa za Siria na Kilikia. Wakati huo, mimi binafsi sikujulikana kwa jumuiya za Wakristo kule Yudea. Walichokuwa wanajua ni kile tu walichosikia: “Mtu yule aliyekuwa akitutesa hapo awali, sasa anaihubiri imani ileile aliyokuwa anajaribu kuiangamiza.” Basi, wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.

Wagalatia 1:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia; Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu. Utukufu una yeye milele na milele, Amina. Nashangaa kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia Injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza Injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiria ninyi Injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiria, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiria ninyi Injili yoyote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo. Kwa maana, ndugu zangu, Injili hiyo niliyowahubiria, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo. Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba nililitesa kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami niliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubirie Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nilikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski. Kisha, baada ya miaka mitatu, nilipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana. Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo. Baadaye nilikwenda pande za Shamu na Kilikia. Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Yudea yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetutesa hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.

Wagalatia 1:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia; Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu. Utukufu una yeye milele na milele, Amina. Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo. Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo. Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski. Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana. Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo. Baadaye nalikwenda pande za Shamu na Kilikia. Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.

Wagalatia 1:1-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Paulo mtume: si mtume wa wanadamu wala aliyetumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo na Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu; na ndugu wote walio pamoja nami: Kwa makanisa ya Galatia: Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyejitoa kwa ajili ya dhambi zetu ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu wa sasa ulio mbaya, sawasawa na mapenzi yake yeye aliye Mungu na Baba yetu. Utukufu una yeye milele na milele. Amen. Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata Injili nyingine, ambayo kwa kweli si Injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri Injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele! Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu yeyote atawahubiria Injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele! Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Kristo. Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu. Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo. Ninyi mmekwisha kusikia juu ya maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kwa nguvu na kujaribu kuliangamiza. Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika yangu maana nilijitahidi sana katika desturi za baba zangu. Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake, alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu yeyote, wala sikupanda kwenda Yerusalemu kuwaona hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilikwenda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski. Kisha baada ya miaka mitatu nilipanda kwenda Yerusalemu kuonana na Kefa na nilikaa naye siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine yeyote isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. Nawahakikishia mbele za Mungu kuwa ninayowaandikia si uongo. Baadaye nilikwenda sehemu za Syria na Kilikia. Lakini mimi binafsi sikujulikana kwa makanisa ya huko Uyahudi yaliyo katika Kristo. Wao walisikia habari tu kwamba, “Mtu yule ambaye hapo kwanza alikuwa akitutesa sasa anahubiri imani ile ile aliyokuwa akijaribu kuiangamiza.” Nao wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.