Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 9:1-15

Ezra 9:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya mambo haya kutendeka, viongozi walinijia na kusema, “Watu wa Israeli, wakiwemo makuhani na Walawi, hawakujitenga na majirani zao katika kufanya machukizo, kama yale ya Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi, Waamoni, Wamoabu, Wamisri na Waamori. Wamewaoa baadhi ya binti zao kuwa wake zao na wake za wana wao, nao wamechanganya taifa takatifu na watu waliowazunguka. Nao viongozi na maafisa wamekuwa mstari wa mbele katika njia hii potovu.” Niliposikia jambo hili nilirarua koti langu na joho langu, nikazingʼoa nywele za kichwa changu na ndevu zangu na kuketi nikishangaa. Kisha kila mmoja aliyetetemeshwa na maneno ya Mungu wa Israeli alikusanyika kunizunguka kwa sababu ya upotovu huu wa hao watu waliorudi kutoka utumwani. Nami niliketi pale nikishangaa mpaka wakati wa dhabihu ya jioni. Ndipo wakati wa kutoa dhabihu ya jioni nikainuka kutoka kujidhili kwangu nikiwa na koti na joho langu lililoraruka, nikapiga magoti mikono yangu ikiwa imeinuliwa kwa BWANA Mungu wangu. Nami nikaomba: “Ee Mungu wangu, natahayari na kuona aibu kukuinulia uso wangu Mungu wangu, kwa sababu dhambi zetu zimejikusanya hata kupita juu ya vichwa vyetu na hatia yetu imefika mbinguni. Tokea siku za babu zetu mpaka sasa, hatia yetu imekuwa kubwa. Kwa sababu ya dhambi zetu, sisi na wafalme wetu na makuhani wetu tumekabiliwa na vita, utumwa, kutekwa na kudhiliwa katika mikono ya wafalme wa kigeni, kama ilivyo leo. “Lakini sasa, kwa muda mfupi, BWANA Mungu wetu amekuwa na neema kwa kutuachia mabaki na kutupa mahali imara katika mahali pake patakatifu, hivyo Mungu wetu atupa mwanga machoni petu na unafuu katika utumwa wetu. Ingawa tu watumwa, Mungu wetu hajatuacha katika kufungwa kwetu. Ametuonyesha huruma mbele ya wafalme wa Uajemi: Ametujalia maisha mapya kwa kujenga upya nyumba ya Mungu wetu na kukarabati magofu yake, naye ametupa ukuta wa ulinzi katika Yuda na Yerusalemu. “Lakini sasa, Ee Mungu wetu, tunaweza kusema nini baada ya hili? Kwa maana tumedharau maagizo uliyoyatoa kupitia watumishi wako manabii uliposema: ‘Nchi mnayoiingia kuimiliki ni nchi iliyochafuliwa na uovu wa watu wake. Kwa matendo yao ya machukizo wameijaza nchi kwa unajisi wao kutoka mwisho mmoja hadi mwingine. Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wowote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’ “Yale yaliyotupata ni matokeo ya matendo yetu mabaya, pia hatia yetu kubwa. Hata hivyo, wewe Mungu wetu, umetuadhibu kidogo kuliko dhambi zetu zilivyostahili na umetupa mabaki kama haya. Je, tutavunja maagizo yako tena na kuoana na watu ambao hufanya mambo ya machukizo? Je, hutakuwa na hasira ya kutosha juu yetu na kutuangamiza, bila kutuachia mabaki wala atakayenusurika? Ee BWANA, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki! Leo hii tumeachwa kama mabaki. Tupo hapa mbele zako na hatia yetu, ingawa katika hali hii hakuna hata mmoja wetu anayeweza kusimama mbele zako.”

Shirikisha
Soma Ezra 9

Ezra 9:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya mambo haya yote kutendeka, viongozi walinijia na kunipa taarifa ifuatayo: “Watu wa Israeli, makuhani na Walawi hawajajitenga na wakazi wa nchi ambao wanatenda machukizo: Waamoni, Wamoabu na Wamisri, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi na Waamori. Wayahudi wanaoa wanawake wa kigeni na kuwaoza wavulana wao pia. Hivyo, taifa takatifu la Mungu limechanganyika na watu wa mataifa mengine Isitoshe, maofisa na wakuu ndio wa kwanza kutenda maovu hayo.” Nilipoyasikia maelezo hayo, nilizirarua nguo zangu na joho langu, nikazingoa nywele zangu na ndevu zangu kwa huzuni kubwa na kuketi chini kwa hofu. Ndipo watu wote walioshikwa na hofu kwa sababu ya maneno aliyosema Mungu wa Israeli kuhusu makosa ya wale waliorudi kutoka uhamishoni walipoanza kukusanyika karibu nami hali nikikaa katika hofu hadi jioni, wakati wa kutoa tambiko. Jioni, wakati wa kutoa tambiko ulipofika, niliinuka mahali hapo nilipokuwa nimekaa kwa huzuni huku nguo zangu zimeraruka pamoja na joho, nikapiga magoti na kumnyoshea mikono yangu Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, na kuomba, nikisema, “Ee Mungu wangu, naona aibu kubwa sana kukiinua kichwa changu mbele yako. Dhambi zetu zimerundikana kupita hata vichwa vyetu; naam, makosa yetu yanafika hata mbinguni. Tangu nyakati za babu zetu hadi sasa, sisi watu wako tumekukosea sana. Na kwa sababu ya dhambi zetu, sisi, wafalme wetu na makuhani wetu tumetiwa mikononi mwa wafalme wa nchi za kigeni, tukauawa, tukachukuliwa mateka na kunyanganywa mali zetu. Na hadi hivi leo, tumetiwa haya kupita kiasi. Lakini sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa muda mfupi umetuonesha huruma yako na kuwawezesha baadhi yetu kuponyoka kutoka utumwani na kuishi kwa usalama mahali hapa patakatifu. Badala ya utumwa, umetupa furaha na maisha mapya. Hukutuacha tuishi utumwani ingawa tulikuwa tu watumwa Uliwafanya wafalme wa Persia wawe wema kwetu na kuturuhusu tuishi na kuijenga nyumba yako iliyokuwa imebomoka, ukatufanya tukae salama hapa Yuda na Yerusalemu. “Lakini sasa, ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo yote? Maana, tumeziasi amri zako ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii ukisema: ‘Nchi mnayoiendea na ambayo itakuwa mali yenu ni nchi iliyo najisi yenye uchafu wa wakazi toka nchi mbalimbali, kwa machukizo yao, wameijaza unajisi tele kila mahali. Kwa hiyo, msiwaoze watu hao binti zenu, wala msiwaruhusu wavulana wenu kuwaoa binti zao. Pia, msishughulikie usalama au mafanikio yao, ili nyinyi wenyewe muweze kuwa na nguvu, na mfaidi mema ya nchi hiyo na kuwaachia watoto wenu kama urithi milele.’ Hata baada ya yote yaliyotupata kwa sababu ya maovu yetu na makosa yetu mengi, tunajua kwamba adhabu uliyotupa, ee Mungu wetu, ni ndogo ikilinganishwa na makosa yetu, na umewaacha baadhi yetu hai. Je, tutavunja amri zako tena na kuoana na watu hawa watendao maovu haya? Je, hutatukasirikia na kutuangamiza kabisa, asibaki hata mmoja wetu hai wala yeyote wa kutoroka? Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki na umetuacha tubaki kama tulivyo hivi leo. Tunaungama makosa yetu mbele yako, tukijua kuwa hakuna aliye na haki yoyote ya kuja mbele yako kwa ajili ya makosa haya.”

Shirikisha
Soma Ezra 9

Ezra 9:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na mambo hayo yalipotendeka, wakuu wakanikaribia, wakisema, Watu wa Israeli, na makuhani, na Walawi, hawakujitenga na watu wa nchi hizi, na machukizo yao, yaani, ya Wakanaani, na Wahiti, na Waperizi, na Wayebusi, na Waamoni, na Wamoabi, na Wamisri, na Waamori. Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao, na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na viongozi umetangulia katika kosa hili. Nami niliposikia hayo, nikararua nguo yangu na joho langu, nikang'oa nywele za kichwa changu, na ndevu zangu, nikaketi kwa mshangao. Ndipo wakanikusanyikia watu wote walioyatetemekea maneno ya Mungu wa Israeli, kwa sababu ya lile kosa la watu wa uhamisho; nami nikaketi kwa mshangao hadi wakati wa sadaka ya jioni. Na wakati wa sadaka ya jioni nikainuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho langu zimeraruliwa, nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za BWANA, Mungu wangu; nikasema, Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu; kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni. Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hadi leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang'anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo. Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na BWANA, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu. Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali ametufikishia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili kutupa maisha mapya, kuisimamisha nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka, na atulinde katika Yuda na Yerusalemu. Na sasa, Ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo? Maana tumeziacha amri zako, ulizoziamuru kwa midomo ya watumishi wako, manabii, ukisema, Nchi ile, mnayoiendea ili kuimiliki, ni nchi ya uchafu, kwa sababu ya uchafu wa watu wa nchi zile, kwa ajili ya machukizo yao, yaliyoijaza tangu upande huu mpaka upande huu, kwa uchafu wao. Basi, msiwape wana wao binti zenu, wala msitwae binti zao kuwa wake za wana wenu, wala msiwatakie amani wala kufanikiwa milele; ili mpate kuwa hodari, na kula wema wa nchi hiyo, na kuwaachia watoto wenu iwe urithi wa milele. Na baada ya hayo yote yaliyotupata kwa sababu ya matendo yetu mabaya, na kwa sababu ya hatia yetu iliyo kuu, ikiwa wewe Mungu wetu hukutuadhibu kama tulivyostahili kwa maovu yetu, maana umetupa mabaki; je! Tuzivunje tena amri zako, tukajiunge na watu wanaotenda machukizo hayo, kwa kuoana nao? Je! Usingekasirika nasi hata kutuangamiza kabisa, pasisalie mabaki yoyote, wala mtu wa kuokoka? Ee BWANA, Mungu wa Israeli, wewe ndiwe mwenye haki, maana sisi tumesalia, mabaki yaliyookoka, kama hivi leo; tazama, sisi tupo hapa wenye hatia mbele zako; maana hapana mtu awezaye kusimama mbele zako kwa sababu ya jambo hili.

Shirikisha
Soma Ezra 9

Ezra 9:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na mambo hayo yalipokwisha kutendeka, wakuu wakanikaribia, wakisema, Watu wa Israeli, na makuhani, na Walawi, hawakujitenga na watu wa nchi hizi, wamefanya sawasawa na machukizo yao, yaani, ya Wakanaani, na Wahiti, na Waperizi, na Wayebusi, na Waamoni, na Wamoabi, na Wamisri, na Waamori. Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao, na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na mashehe umetangulia katika kosa hili. Nami niliposikia hayo, nikararua nguo yangu na joho yangu, nikang’oa nywele za kichwa changu, na ndevu zangu, nikaketi kwa mshangao. Ndipo wakanikusanyikia watu wote walioyatetemekea maneno ya Mungu wa Israeli, kwa sababu ya lile kosa la watu wa uhamisho; nami nikaketi kwa mshangao hata wakati wa sadaka ya jioni. Na wakati wa sadaka ya jioni nikainuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu zimeraruliwa, nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za BWANA, Mungu wangu; nikasema, Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu; kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni. Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang’anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo. Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na BWANA, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu. Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili kutuburudisha, kuisimamisha nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka, atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu. Na sasa, Ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo? Maana tumeziacha amri zako, ulizoziamuru kwa midomo ya watumishi wako, manabii, ukisema, Nchi ile, mnayoiendea ili kuimiliki, ni nchi ya uchafu, kwa sababu ya uchafu wa watu wa nchi zile, kwa ajili ya machukizo yao, yaliyoijaza tangu upande huu mpaka upande huu, kwa uchafu wao. Basi, msiwape wana wao binti zenu, wala msitwae binti zao kuwa wake za wana wenu, wala msiwatakie amani wala kufanikiwa milele; ili mpate kuwa hodari, na kula wema wa nchi hiyo, na kuwaachia watoto wenu iwe urithi wa milele. Na baada ya hayo yote yaliyotupata kwa sababu ya matendo yetu mabaya, na kwa sababu ya hatia yetu iliyo kuu, ikiwa wewe Mungu wetu hukutuadhibu kama tulivyostahili kwa maovu yetu, tena umetupa mabaki; je! Tuzivunje tena amri zako, tukajiunge na watu wanaotenda machukizo hayo, kwa kuoana nao? Je! Usingekasirika nasi hata kutuangamiza kabisa, pasisalie mabaki yo yote, wala mtu wa kuokoka? Ee BWANA, Mungu wa Israeli, wewe ndiwe mwenye haki, maana sisi tumesalia, mabaki yaliyookoka, kama hivi leo; tazama, sisi tupo hapa wenye hatia mbele zako; maana hapana mtu awezaye kusimama mbele zako kwa sababu ya jambo hili. i.

Shirikisha
Soma Ezra 9

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha