Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 7:1-28

Ezra 7:1-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya mambo haya, wakati wa utawala wa Artashasta mfalme wa Uajemi, Ezra mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia, mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu, mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi, mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki, mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani mkuu Aroni. Huyu Ezra alipanda kutoka Babeli. Alikuwa mwalimu mwenye ujuzi mzuri katika sheria ya Mose, ambayo BWANA, Mungu wa Israeli, alikuwa ametoa. Mfalme alikuwa amempa Ezra kila kitu alichoomba, kwa maana BWANA Mungu wake alikuwa pamoja naye. Pia baadhi ya Waisraeli, wakiwemo makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu na watumishi wa Hekalu, nao walikuja Yerusalemu mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta. Ezra aliwasili Yerusalemu mwezi wa tano wa mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta. Ezra alianza safari yake kutoka Babeli tangu siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akawasili Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kwa maana mkono wa neema wa Mungu wake ulikuwa juu yake. Kwa maana Ezra alikuwa amejitoa kwa moyo wote kujifunza na kushika sheria ya BWANA na kuwafundisha watu wa Israeli amri na sheria zake. Hii ni nakala ya barua ambayo Mfalme Artashasta alikuwa amempa Ezra aliyekuwa kuhani na mwalimu, mtu aliyeelimika katika mambo yahusuyo maagizo na amri za BWANA kwa Israeli. Artashasta, mfalme wa wafalme, Kwa Ezra kuhani, mwalimu wa Sheria ya Mungu wa mbinguni: Salamu. Sasa naamuru kwamba mtu yeyote Mwisraeli katika ufalme wangu, pamoja na makuhani na Walawi, ambaye anataka kwenda Yerusalemu pamoja nawe aweza kwenda. Unatumwa na mfalme na washauri wake saba kuchunguza kuhusu Yuda na Yerusalemu kulingana na Sheria ya Mungu wako, iliyoko mkononi mwako. Zaidi ya hayo, uchukue pamoja nawe fedha na dhahabu ambazo mfalme na washauri wake wamempa Mungu wa Israeli kwa hiari, Mungu ambaye maskani yake yako Yerusalemu, pia fedha na dhahabu zote unazoweza kupata kutoka jimbo la Babeli, pamoja na sadaka za hiari watakazotoa watu na makuhani kwa ajili ya Hekalu la Mungu wao katika Yerusalemu. Hakikisha kwamba fedha hizi zimetumika kununua mafahali, kondoo dume na wana-kondoo pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, uvitoe dhabihu juu ya madhabahu ya Hekalu la Mungu wenu katika Yerusalemu. Kisha wewe na Wayahudi ndugu zako mnaweza kufanya lolote linaloonekana jema sana kwa fedha na dhahabu zilizosalia, kulingana na mapenzi ya Mungu wenu. Uvitoe kwa Mungu wa Yerusalemu vyombo vyote ulivyokabidhiwa kwa ajili ya ibada katika Hekalu la Mungu wako. Kitu kingine chochote kinachohitajika kwa ajili ya Hekalu la Mungu wenu ambacho unatakiwa kukitoa, waweza kukitoa kutoka hazina ya mfalme. Mimi, Mfalme Artashasta, sasa naagiza watunza hazina wote wa Ngʼambo ya Mto Frati kutoa kwa bidii chochote kwa Ezra kuhani na mwalimu wa Sheria ya Mungu wa mbinguni atakachohitaji kwenu, talanta 100 za fedha, ngano kori 100, divai bathi 100, mafuta ya zeituni bathi 100, na chumvi kiasi chochote. Chochote ambacho Mungu wa mbinguni ameagiza, kifanyike kwa ukamilifu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wa mbinguni. Kwa nini pawepo ghadhabu dhidi ya utawala wa mfalme na wanawe? Pia ninyi fahamuni kuwa hamna mamlaka ya kuwatoza kodi, ushuru au ada makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu, watumishi wa Hekalu au wafanyakazi wengine kwenye nyumba ya Mungu. Nawe Ezra, kufuatana na hekima ya Mungu wenu uliyo nayo, weka mahakimu na waamuzi wote wanaozifahamu sheria za Mungu wenu ili watoe haki kwa watu wote wa Ngʼambo ya Mto Frati. Nawe inakupasa umfundishe yeyote ambaye hazifahamu. Yeyote ambaye hataitii sheria ya Mungu wenu pia sheria ya mfalme, hakika lazima aadhibiwe kwa kuuawa, kuhamishwa, kunyangʼanywa mali au kufungwa gerezani. Sifa ziwe kwa BWANA, Mungu wa baba zetu, Mungu ambaye kwa njia hii ameweka ndani ya moyo wa mfalme kuipa heshima nyumba ya BWANA iliyoko Yerusalemu, kwa namna hii ambaye ameniongezea kibali chake mbele ya mfalme, washauri wake na maafisa wote wa mfalme wenye uwezo. Kwa kuwa mkono wa BWANA Mungu wangu ulikuwa pamoja nami, nilijipa moyo nikakusanya watu walio viongozi kutoka Israeli wakwee pamoja nami.

Shirikisha
Soma Ezra 7

Ezra 7:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Baadaye, wakati wa utawala wa mfalme Artashasta wa Persia, palikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Ezra. Ezra alikuwa mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia, mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu, mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi, mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki, mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Aroni, kuhani mkuu. Ezra aliondoka Babuloni, yeye alikuwa mwandishi mwenye ujuzi mwingi sana katika sheria ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alikuwa amempatia Mose. Na kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, mfalme alimpatia Ezra kila kitu alichohitaji. Mnamo mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Artashasta, Ezra alifunga safari kutoka Babuloni kwenda Yerusalemu. Baadhi ya watu wa Israeli, makuhani, Walawi, waimbaji, walinda malango na wahudumu wa hekalu walikwenda pamoja naye. Waliwasili mjini Yerusalemu mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Artashasta. Mwenyezi-Mungu aliifanikisha sana safari yao waliyokuwa wameianza siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. Ezra alikuwa amejitoa kwa moyo wote kujifunza sheria ya Mwenyezi-Mungu, kuitii na kuwafundisha watu wa Israeli maagizo na amri zake. Ifuatayo ni barua ambayo Artashasta alimpa Ezra, kuhani na mwandishi, na mwenye ujuzi katika amri na masharti ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli. “Kutoka kwa Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani na mtu mwenye ujuzi katika sheria ya Mungu wa mbinguni; Wasalaam!” “Ninaamuru kwamba katika utawala wangu, Mwisraeli yeyote, au kuhani wao, au Mlawi, akitaka kurudi Yerusalemu kwa hiari yake, anaweza kwenda pamoja nawe. “Mimi pamoja na washauri wangu saba, tunakutuma uende ufanye uchunguzi huko Yuda na Yerusalemu kuona kama sheria ya Mungu wako ambayo umekabidhiwa inafuatwa kikamilifu. Utachukua fedha na dhahabu ambayo mimi na washauri wangu tumemtolea kwa hiari Mungu wa Israeli ambaye hekalu lake limo mjini Yerusalemu. Utachukua pia fedha na dhahabu yote utakayokusanya katika mkoa wote wa Babuloni, pamoja na matoleo ya hiari waliyotoa Waisraeli na makuhani wao kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu. Fedha hiyo utaitumia kwa uangalifu sana kununua mafahali, kondoo dume, wanakondoo na tambiko ya nafaka na divai, na kuvitoa madhabahuni katika nyumba ya Mungu wenu iliyoko Yerusalemu. Fedha na dhahabu itakayobaki unaweza kuitumia pamoja na wananchi wenzako kama mtakavyopenda, kufuatana na mapenzi ya Mungu. Vyombo ambavyo umekabidhiwa kwa ajili ya ibada ya nyumba ya Mungu wako, utamtolea Mungu wa Yerusalemu. Ukihitaji kitu kingine chochote kwa ajili ya nyumba ya Mungu wako unaweza kukipata kutoka katika hazina ya mfalme. Mimi mfalme Artashasta, natoa amri kwa waweka hazina wote katika mkoa wa magharibi ya mto Eufrate kwamba chochote atakachohitaji Ezra, kuhani na mwandishi wa sheria ya Mungu wa mbinguni, mtampa, tena bila kusita, fedha kiasi atakacho mpaka kufikia kilo 3,400, ngano kilo 10,000, divai lita 2,000, mafuta lita 2,000, na chumvi kiasi chochote atakachohitaji. Kila kitu alichoagiza Mungu wa mbinguni kwa ajili ya nyumba yake, ni lazima kitekelezwe kikamilifu, asije akaukasirikia ufalme wangu au wanangu. Tunawafahamisheni pia kuwa ni marufuku kuwadai kodi ya mapato, ushuru au ada makuhani, Walawi, waimbaji, walinda mlango, wafanyakazi au watumishi wengine wa nyumba hii ya Mungu. Nawe Ezra, kwa kutumia hekima aliyokupa Mungu wako, hiyo uliyonayo, chagua mahakimu, na waamuzi watakaowaongoza wakazi wote wa mkoa wa magharibi ya Eufrate ambao wanaishi kufuatana na sheria ya Mungu wako. Na yule ambaye haijui sheria hiyo, mfundishe. Mtu yeyote ambaye hatatii sheria ya Mungu wako na ya mfalme, na ahukumiwe mara moja: Kufa, kuhamishwa, kunyanganywa mali yake au kufungwa.” Ezra akasema, “Na asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zetu; ambaye amempatia mfalme moyo wa kutia mapambo nyumba ya Mwenyezi-Mungu iliyoko Yerusalemu. Kwa fadhili zake Mungu, nimepata msaada wa mfalme na maofisa wake wenye uwezo mkuu. Nilijipa moyo kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, alikuwa pamoja nami, hata niliwakusanya viongozi wa Israeli ili warudi pamoja nami.”

Shirikisha
Soma Ezra 7

Ezra 7:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa baada ya mambo hayo, wakati wa kutawala kwake Artashasta, mfalme wa Uajemi, Ezra, mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia, mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu, mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi, mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki, mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, kuhani mkuu; huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika Sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa BWANA, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa BWANA, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye. Nao wakakwea baadhi ya wana wa Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini, ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta. Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme. Maana alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake ulivyokuwa pamoja naye. Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya BWANA, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli. Basi hii ndiyo nakala ya barua, ambayo mfalme Artashasta alimpa Ezra, kuhani, mwandishi, mjuzi wa amri za BWANA, na sheria zake alizowapa Waisraeli. Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani, mwandishi wa Torati ya Mungu wa mbinguni, wasalamu; na kadhalika. Natoa amri ya kwamba watu wote walio wa Israeli, na makuhani wao, na Walawi, katika ufalme wangu, wenye nia ya kwenda Yerusalemu kwa hiari yao wenyewe, waende pamoja nawe. Kwa kuwa umetumwa na mfalme, na washauri wake saba, ili kuuliza habari za Yuda na Yerusalemu, kwa sheria ya Mungu wako iliyo mkononi mwako; na kuichukua fedha na dhahabu, ambayo mfalme, na washauri wake, kwa hiari yao, wamemtolea Mungu wa Israeli, akaaye Yerusalemu; na fedha yote na dhahabu utakayoona katika wilaya ya Babeli, pamoja na vitu watakavyotoa watu kwa hiari yao, na vitu vya makuhani walivyotoa kwa hiari yao, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu. Kwa sababu hiyo ujitahidi kununua kwa fedha hiyo mafahali, kondoo dume, wana-kondoo, pamoja na sadaka zao za unga, na sadaka zao za kinywaji; nawe utazitoa juu ya madhabahu ya nyumba ya Mungu wenu, iliyoko Yerusalemu. Na jambo lolote mtakaloona vema kulitenda, wewe na ndugu zako, kwa ile fedha na dhahabu itakayobaki, hilo litendeni, kama apendavyo Mungu wenu. Na vile vyombo upewavyo kwa huduma ya nyumba ya Mungu wako, virejeshe mbele za Mungu wa Yerusalemu. Na chochote kitakachohitajiwa zaidi, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wako, kitakachokupasa kukitoa, kitoe katika nyumba ya hazina ya mfalme. Na mimi, naam mimi, mfalme Artashasta, nawapa amri watunza hazina wote, walio ng'ambo ya Mto, ya kwamba, kila neno ambalo Ezra, kuhani, mwandishi wa Torati ya Mungu wa mbinguni, atalitaka kwenu, na litendeke kwa bidii nyingi, hata kiasi cha talanta mia moja za fedha, na vipimo mia vya ngano, na bathi mia moja za divai, na bathi mia moja za mafuta na chumvi ya kiasi chochote kile. Kila neno litakaloamriwa na Mungu wa mbinguni, na litendeke kikamilifu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wa mbinguni. Kwa nini itokee ghadhabu juu ya ufalme wa mfalme na wanawe? Tena tunawaarifu ya kuwa katika habari ya makuhani, na Walawi, na waimbaji, na mabawabu na Wanethini, au watumishi wa nyumba hii ya Mungu, si halali kuwatoza kodi, wala ada, wala ushuru. Na wewe, Ezra, kwa kadiri ya hekima ya Mungu wako iliyo mkononi mwako, waweke mahakimu na majaji, watakaowaamua watu wote walio ng'ambo ya Mto, yaani, wote wenye kuzijua amri za Mungu wako; na ukamfundishe yeye asiyezijua. Na kila mtu asiyekubali kuitenda sheria ya Mungu wako, na sheria ya mfalme, na apatilizwe hukumu kali, iwe ni kuuawa, au ni kuhamishwa, au kunyang'anywa mali yake, au kufungwa. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa baba zetu, aliyetia neno kama hilo katika moyo wa mfalme, kuipamba nyumba ya BWANA iliyoko Yerusalemu. Naye amenifikishia rehema zake mbele ya mfalme, na washauri wake, na mbele ya wakuu wote wa mfalme wenye mamlaka. Nami nikatiwa nguvu, kwa kadiri mkono wa BWANA, Mungu wangu, ulivyokuwa pamoja nami, nikawakusanya wakuu wote katika Israeli, ili wakwee pamoja nami.

Shirikisha
Soma Ezra 7

Ezra 7:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa baada ya mambo hayo, wakati wa kutawala kwake Artashasta, mfalme wa Uajemi, Ezra, mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia, mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu, mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi, mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki, mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, kuhani mkuu; huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa BWANA, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa BWANA, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye. Nao wakakwea baadhi ya wana wa Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini, ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta. Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme. Maana alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake ulivyokuwa pamoja naye. Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya BWANA, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli. Basi hii ndiyo nakala ya waraka, mfalme Artashasta aliyompa Ezra, kuhani, mwandishi, naam, mwandishi wa maneno ya amri za BWANA, na wa sheria zake alizowapa Israeli. Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani, mwandishi wa torati ya Mungu wa mbinguni, salamu kamili; wakadhalika. Natoa amri ya kwamba wote walio wa watu wa Israeli, na makuhani wao, na Walawi, katika ufalme wangu, wenye nia ya kwenda Yerusalemu kwa hiari yao wenyewe, waende pamoja nawe. Kwa kuwa umetumwa na mfalme, na washauri wake saba, ili kuuliza habari za Yuda na Yerusalemu, kwa sheria ya Mungu wako iliyo mkononi mwako; na kuichukua fedha na dhahabu, ambayo mfalme, na washauri wake, kwa hiari yao, wamemtolea Mungu wa Israeli, akaaye Yerusalemu; na fedha yote na dhahabu utakayoona katika wilaya ya Babeli, pamoja na vitu watakavyotoa watu kwa hiari yao, na vitu vya makuhani walivyotoa kwa hiari yao, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu. Kwa sababu hiyo ujitahidi kununua kwa fedha hiyo mafahali, kondoo waume, wana-kondoo, pamoja na sadaka zao za unga, na sadaka zao za kinywaji; nawe utazitoa juu ya madhabahu ya nyumba ya Mungu wenu, iliyoko Yerusalemu. Na neno lo lote mtakaloona vema kulitenda, wewe na ndugu zako, kwa ile fedha na dhahabu itakayobaki, hilo litendeni, kama apendavyo Mungu wenu. Na vile vyombo upewavyo kwa huduma ya nyumba ya Mungu wako, virejeze mbele za Mungu wa Yerusalemu. Na cho chote kitakachohitajiwa zaidi, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wako, kitakachokupasa kukitoa, kitoe katika nyumba ya hazina ya mfalme. Na mimi, naam mimi, mfalme Artashasta, nawapa amri wote wenye kutunza hazina, walio ng’ambo ya Mto, ya kwamba, kila neno ambalo Ezra, kuhani, mwandishi wa torati ya Mungu wa mbinguni, atalitaka kwenu, na litendeke kwa bidii nyingi, hata kiasi cha talanta mia za fedha, na vipimo mia vya ngano, na bathi mia za divai, na bathi mia za mafuta, na chumvi bila kuuliza kiasi chake. Kila neno litakaloamriwa na Mungu wa mbinguni, na litendeke halisi kwa ajili ya nyumba ya Mungu wa mbinguni. Kwa nini itokee ghadhabu juu ya ufalme wa mfalme na wanawe? Tena twawaarifuni ya kuwa katika habari ya makuhani, na Walawi, na waimbaji, na mabawabu na Wanethini, au watumishi wa nyumba hii ya Mungu, si halali kuwatoza kodi, wala ada, wala ushuru. Na wewe, Ezra, kwa kadiri ya hekima ya Mungu wako iliyo mkononi mwako, waweke waamuzi na makadhi, watakaowahukumu watu wote walio ng’ambo ya Mto, yaani, wote wenye kuzijua amri za Mungu wako; ukamfundishe yeye asiyezijua. Na kila mtu asiyekubali kuitenda sheria ya Mungu wako, na sheria ya mfalme, na apatilizwe hukumu kwa bidii, kwamba ni kuuawa, au kwamba ni kuhamishwa, au kuondolewa mali yake, au kufungwa. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa baba zetu, aliyetia neno kama hilo katika moyo wa mfalme, kuipamba nyumba ya BWANA iliyoko Yerusalemu. Naye amenifikilizia rehema zake mbele ya mfalme, na washauri wake, na mbele ya wakuu wote wa mfalme wenye mamlaka. Nami nikatiwa nguvu, kwa kadiri mkono wa BWANA, Mungu wangu, ulivyokuwa pamoja nami, nikawakusanya wakuu wote katika Israeli, ili wakwee pa

Shirikisha
Soma Ezra 7

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha